Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 4 July 2013

Prof. Maghembe aagiza wakulima wa mboga Ruaha watafutiwe maji




Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Prof. Jumanne Maghembe, amewaagiza wataalam wa wizara yake kuwatafutia maji mbadala wakulima wa mboga wanaoendesha shughuli zao katika ardhi chepechepe  ya Bonde la Mto Ruaha ili kunusuru mto huo kukauka.

Prof. Maghembe alitoa agizo hilo wakati akifungua mkutano wa tano wa mwaka wa bodi za maji nchini ulianza jana jijini Mbeya.

Alisema wakulima hao wanatumia maji yaliyo kwenye ardhi owevu ya Bonde la Mto Ruaha na kuathiri mtiririko wa maji ya mto huo, jambo ambalo pia linachangia uharibifu wa mazingira.

Hata hivyo, Prof. Maghembe alisema sio busara kuwaondoa wakulima hao kwenye maeneo yao ya kilimo kwa vile kazi wanazozifanya ni halali na mazao yao yanahitajika kwa ajili ya kuendelza uchumi wa taifa.

Badala yake alisema wakulima hao wanahitaji kutafutiwa maji mbadala ili waendelee na shughuli zao bila ya kuathiri mazingira na mtiririko wa maji ya mto Ruaha.

Alisema wakulima hao wanahitaji kuchimbiwa visima au kujengewa skimu za umwagiliaji waweze waendelee na shughuli zao kwani suala hilo liko ndani ya uwezo wa wataalam, hivyo akawaagiza walitekeleze haraka iwezekanavyo.

Awali, akimkaribisha Waziri Maghembe, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alisema kazi ya kuwaondoa wafugaji kwenye vyanzo vya maji ni ngumu, hivyo inahitaji mkakati wa kitaifa ili kuifanikisha.

Alisema mkakati huo ni lazima uwe wa kubadilisha fikra za wafugaji kuachana na tabia ya kumiliki mifugo mingi kuliko uwezo wa malisho na badala yake wafuge kisasa kwa kuwa na mifugo michache yenye manufaa makubwa kwao.

Mkutano wa tano wa mwaka wa bodi za mabonde nchini unafanyika kwa siku tatu jijini Mbeya ukiwa na kauli mbiu isemayo ‘Jitihada za pamoja katika kutunza vyanzo vya maji ni muhimu ili kuhakikisha upatikanaji wa maji’.

0 comments:

Post a Comment