Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Monday 1 July 2013

Museveni aonya Afrika kutegemea kilimo

                             22 shaaban,1434 Hijiriyah/ 01 july,2013 Miyladiyah
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amezionya nchi za Afrika kutoendelea kutegemea sekta ya kilimo kuwa ndiyo mkombozi wa maendeleo, badala yake amezishauri zigeukie maeneo mengine ikiwamo kujenga mtandao mpana wa kiviwanda kwani uzoefu unaonyesha kuwa nchi nyingi Afrika zinakabiliwa na tatizo la ardhi.
Rais Museveni ambaye alikuwa akizungumza katika Kongamano la Kimataifa linalohusu majadiliano ya wazi kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) alisema nchi nyingi za Afrika bado zinaendelea kuhubiri maendeleo yatokanayo ya sekta ya kilimo ilhali zikifahamika wazi kuhusiana na tatizo la ardhi.
Alisema utashi wake unamtuma kuamini kuwa iko siku bara la Afrika litajikuta katika hali ya kukosa mwelekeo kutokana na uhaba wa ardhi ambao alisema umeanza kujitokeza katika maeneo mengi.
Akitetea hoja yake hiyo, Museveni alitolea mfano hali ilivyo nchini Kenya ambako alisema kuwa moja ya tatizo kubwa linalojitokeza sasa ni kuhusiana na umiliki wa ardhi ambako idadi kubwa ya watu wanaendelea kulalamika kutokana na ardhi hiyo kuhodhiwa na wachache.
Pamoja na kutoa angalizo hilo, Rais Museveni alizishauri nchi za Afrika kuanza kufikiria njia nyingine za kujiletea maendeleo ikiwamo pia kuanzisha mikakati ya kuwa na viwanda vya kutosha. kwani bila kufanya hivyo dhana ya kuwa na maendeleo endelevu huenda isifikiwe kwa wakati.
“Lakini pia napenda niwasihi Waafrika wenzangu tunapaswa kutambua kuwa kuendelea kutegemea rasilimali pekee hakutatusaidia,” alisema
Kongamano hilo ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, ni jukwaa linalowakutanisha viongozi wa kiserikali, wanasiasa pamoja na wataalamu kwa ajili ya kuwa na majadiliano ya pamoja ambayo yanazingatia fursa sawa kwa pande zote.
Leo (Jumapili) viongozi wanahudhuria kongamano hilo ambalo linaendeshwa na Rais Jakaya Kikwete na wanatazamiwa kuendelea na majadiliano yatakayogusia maeneo ya ubora na viwango vya ufanyaji biashara, mahitaji yanayopaswa kuzingatiwa ili kuleta mageuzi kwa maisha ya wanawake kwenye sekta ya teknolojia na uendelezwaji wa rasilimali.
Wakati akifungua majadiliano hayo, Rais Jakaya Kikwete alizitaka nchi za Afrika kubadilika kwa kuendeleza wasomi, ili wawe chachu ya kubuni na kuibua vyanzo vya maendeleo.

0 comments:

Post a Comment