Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Monday, 1 July 2013

Air Force One; Ishara ya umaarufu

                              22 shaaban,1434 Hijiriyah/ 01 july,2013 Miyladiyah
Rais Obama akiwasiliana na wasaidizi wake safarini ndani ya Air Force One. Hiyo ni ishara ya kuwa ndege yake inajitofautisha na nyinginezo za abiria. Picha ya Maktaba.

 

Hakuna shaka  yoyote kuwa Rais wa Marekani akisafiri kokote duniani akitumia ndege ya kijeshi, basi hupewa jina la ‘Air Force One’.
Ukweli si ndege maalumu yenye jina hilo, lakini ndege inayopewa jina hili ni alama ya ndege ya rais wa nchi hiyo.
Jina hilo hutumika kwa ndege mbili kubwa  aina ya Boeing 747-200B  zenye namba 28000 na 29000, zinazotumiwa na rais akiwa safarini ndani na nje ya Marekani na moja anayosafiria ndiyo huitwa kwa jina hilo.
Ndege  zote hizo husimamiwa na Jeshi la Anga la nchi hiyo. Kwa jeshi la nchi hiyo ishara kwa ndege hizo ni VC-25A.
Air Force One ni moja ya ishara maarufu kwa urais wa Marekani na si kwa Marekani  pekee, bali imekuwa kwa ulimwengu mzima. Ndege zote zimeandikwa maandishi makubwa “United States of America,” bendera ya  nchi hiyo na nembo ya rais wa nchi hiyo.
Ndege hii tofauti na za kawaida zilizozoeleka, inao uwezo wa kujazwa mafuta ikiwa angani kwani haina kiwango ama urefu maalumu wa kusafiri unaweza kumfikisha rais huyo popote duniani kwa usalama wa hali ya juu.
Ndani ya ndege vifaa vya umeme vimetengenezwa kwa ugumu ambao haviwezi kusababisha hitilafu ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya abiria. Ina vifaa vizito vya mawasiliano vyenye teknolojia ya hali ya juu inayowezesha kufanya kazi kama sehemu ya kamandi ya kijeshi ikiwa angani kama kuna shambulio nchini mwao.
Ndani yake rais na abiria wengine wanafaidi nafasi kubwa ambayo ni kama futi 4,000 za mraba zilizo katika ghorofa tatu ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa kwa ajili ya Rais, yenye chumba cha kifahari cha kulala, ofisi, choo, chumba cha mikutano.
Pia, kuna sehemu ya matibabu ambayo ina chumba cha upasuaji na daktari angalau mmoja anatakiwa kuwa ndani wakati ndege hiyo ikiwa safarini, pamoja na wahudumu wengine wa afya. Kuna sehemu mbili za jiko ambazo zinaweza kutumika kuandaa chakula cha watu 100 kwa wakati mmoja.
Air Force One pia ina sehemu kwa ajili ya wasaidizi walinzi na watu wengine wanaoongozana na rais safarini ikiwamo waandishi wa habari ama wageni wengine.  Kuna ndege kadhaa za mizigo ambazo zinaongozana na ndege hiyo zikiwamo za kuongeza mafuta ili kuweza kumuhudumia Rais iwapo atakuwa angani kwa muda mrefu.
Air Force One inahudumiwa na Kikosi cha Safari za Rais ikiwa ni sehemu ya maofisa usalama wa Ikulu ya Marekani kilichoanzishwa mwaka 1944 chini ya Rais Franklin D. Roosevelt.


0 comments:

Post a Comment