Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 9 June 2013

Warioba: Serikali ya Muungano haitakopa fedha

                            

 Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema kama mfumo wa Serikali tatu utakubalika, Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha.
Amesema hata katika suala la uwakilishi wa nchi Kimataifa, Rais wa Muungano ndiye atakuwa na jukumu hilo na siyo Rais wa Tanzania bara (Tanganyika) au Zanzibar na kwamba Serikali hiyo ndiyo itakuwa na nguvu na itategemewa sana na Serikali nyingine.
Tangu Tume hiyo ilipotoa rasimu ya Katiba, watu wa kada mbalimbali wamekuwa wakitoa maoni yao, huku wakionyesha wasiwasi mkubwa juu ya uendeshwaji wa Serikali hizo, kwamba utakuwa wa gharama kubwa kuliko ilivyo sasa.
Katika mahojiano yake na waandishi waandamizi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayochapisha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, Sunday Citizen na Mwanaspoti, Tido Mhando ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL na Theophil Makunga, Meneja wa Uendelezaji wa Biashara wa MCL, Jaji Warioba alitoa ufafanuzi juu ya suala hilo.
Swali: Gharama za uendeshaji wa Serikali hizi utakuwaje, huoni kama Rais wa Muungano atategemea zaidi fedha na msaada kutoka Tanganyika na Zanzibar?
Warioba: Katika Katiba ya sasa mapato ya Muungano yanatokana na vyanzo vitatu, Kodi ya Mapato (income tax), Ushuru wa Forodha (custom duty) pamoja na ushuru wa bidhaa (excise duty).
Kodi ya mapato ndiyo inatoa fedha nyingi sana na inafuatiwa na kodi ya ushuru wa bidhaa na ushuru wa forodha. Kutokana na hesabu tulizopiga, tumeona matumizi katika Serikali ya Muungano yapo katika sehemu mbili, moja ni yale ya Muungano na ya pili ni yale ya Tanganyika ambayo yanachukua fedha nyingi.
Mwaka 2010/2011 mapato ya kodi ya mapato yalikuwa Sh2 trilioni na mapato ya ushuru wa bidhaa yalikuwa Sh1trilioni na mapato ya ushuru wa forodha yalikuwa Sh600 bilioni.
Ni kwamba matumizi ya mambo ya Muungano yalikuwa chini ya Sh1trilioni, ndiyo maana tumechagua ushuru wa bidhaa, kwani tukipata fedha zile zitaweza kumaliza matumizi yote ya Serikali ya Muungano.
Hivyo basi kama tukiendelea na utaratibu huu wa Serikali tatu, ni wazi kwamba Serikali ya Muungano haitakuwa na haja ya kukopa fedha kwa kuwa itakuwa nazo za kutosha, Serikali zitakazokopa ni hizo mbili.
Tulikuwa tukijua wazi kuwa Serikali ya Muungano lazima iwe na chanzo cha uhakika cha fedha, na kwa utaratibu huu Serikali hizo tatu ndizo zitakazokubaliana jinsi ya kukusanya fedha hizo.

0 comments:

Post a Comment