Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 9 June 2013

JK kuteta na Wabunge, Mawaziri Dodoma

                              

 Rais Jakaya Kikwete akizungumza na vyombo vya habari siku za hivi karibuni  
 
 Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwasili mjini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine atakutana na Kamati ya Bunge ya Bajeti ikiwa siku chache kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali itakayoainisha Mapato na Matumizi yake kwa mwaka wa fedha 2013/14, Juni 13.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge imekuwa na vikao karibu kila siku, wakati mwingine vikimalizika usiku ili ikijiweka sawa kabla ya
kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu ya Serikali.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Rais Kikwete akiwa mjini Dodoma atakutana na baraza lake la mawaziri na Kamati ya Bajeti ili kupata picha ya mwelekeo wa bajeti, ambayo sehemu kubwa imeelezwa kubanwa na upatikanaji wa fedha za kutosha kwa ajili ya kuziwezesha wizara na taasisi zake kwa shughuli za kawaida na maendeleo.
Hata hivyo, habari zinadai kuwa ugumu uliopo ni namna ya kupata fedha kwa asilimia 100 kwa ajili ya kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo na matumizi ya kawaida kwa wizara na Idara za Serikali.
Chanzo chetu kilieleza kuwa pamoja na 'kukuna kichwa' jinsi ya kupata fedha hizo, hata utekelezaji wa bajeti ya 2011/12 na 2012/13, ulikuwa mgumu kwa kuwa baadhi ya wizara na
taasisi zake zilipata nusu ya bajeti iliyopitishwa au asilimia 30 ya bajeti nzima.
Upatikanaji wa fedha hizo chini ya asilimia unatarajiwa kwa wizara na taasisi zake huku ikielezwa kuwa ni kutokana na kumegwa kwa asilimia za mafungu kulikosababishwa na kuongezeka kwa matumizi ya Serikali zikiwemo dharura.
Chanzo kilipasha kuwa, wakati hali ikiwa hivyo, hadi kufikia juzi kila Wizara ilishawasilisha taarifa zake mbele ya kamati hiyo iliyokuwa ikikutana katika Ukumbi wa Pius Msekwa mjini Dodoma, huku wizara nyingi mbali na kuwasilisha taarifa za mafungu yao ya bajeti kwa mwaka 2013/14, zimeomba kuongezewa kasima kama kuna uwezekano.
Itakumbukwa, wakati akiwasilisha bajeti ya mwaka 2012/13 Juni 14 mwaka jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema kuwa bajeti hiyo imelenga kukabiliana na changamoto za uchumi ikiwa ni pamoja na kuongeza fursa za kuuza, kushughulikia uhaba wa chakula nchini na kupambana na mfumuko wa bei.
Alisema pia kuwa mpango wa Serikali ni kuendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kusimamia matumizi, kushughulikia ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na kuwekeza katika miundombinu ya nishati ya umeme hasa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Kingine alichokisema ni ujenzi wa barabara, bandari na reli ya kati ili kupunguza gharama za kufanya biashara na kuongeza tija katika uzalishaji; pamoja na kulipa madeni ya ndani na nje.

0 comments:

Post a Comment