Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday 29 June 2013

Tanzania, Sri lanka kushirikiana nyanja za uchumi, utalii

                          21 shaaban,1434 Hijiriyah/ 30 june,2013 Miyladiyah
Rais Jakaya Kikwete akimkaribisha rais wa Sri Lanka,Mahinda Rajapaksa kwenye hafla ya jioni Ikulu jijini Dar es Salaam juzi ambapo nchi hizo mbili zilitiliana saini ya mikataba ya ushirikiano Kiuchumi na Utalii.Picha na Emmanuel Herman.



Tanzania na Sri Lanka zimetiliana saini mikataba ya ushirikiano kwenye maeneo ya uchumi na utalii,huku Rais Jakaya Kikwete akiliombea amani taifa hilo ambalo linakabiliwa na hali mbaya ya kisiasa.
Makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ikulu mbele ya marais wote wawili Rais Kikwete na mgeni wake Mahinda Rajapaska yanahusu ushirikiano kwenye eneo la biashara kwa kuanzisha vitega uchumi vitavyowajumuisha wafanyabiashara wa pande zote mbili.
Pia makubaliano hayo yamelenga kuimarisha sekta ya utaliii,ambapo imekubaliwa kuwa kila upande utatumia rasilimali zake kuwavutia watalii na kwamba kwa kuanzia ujumbe wa Tanzania unatazamia kutembelea Sri Lanka baadaye mwaka huu kwa ajili ya kufanya tathimini.
Akizungumzia hatua ya kutiwa saini makubaliano hayo ambayo pia yanahusu eneo la utamaduni, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema nchi zote mbili zinategemea kunufaika hasa kwa kuzingatia kuwa makubaliano hayo yamefanyika kwa kuzingatia historia ya nchi zote.
“ Sasa tumefungua ukurasa mpya.. tunategemea kuona watanzania wakimiminika kwa wingi nchini Sri Lanka kwa ajili ya kutafuta fursa za kibiashara” alisema Membe.
Akizungumza kwenye hafla maalumu ya chakula cha jioni aliyomwandalia mgeni wake, Rais Jakaya Kikwete alipongeza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ya Sri Lanka kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wake ikiwemo pia kukabiliana na mawimbi mabaya ya kisiasa.
“ Ni matumaini yangu hali ngumu ya kisiasa inayojitokeza sasa itapatiwa ufumbuzi na hatimaye taifa hili litaendelea kuangaza. Naamini mtaendelea kupiga hatua kwenye maeneo ya uchumi na maendeleo kwa ujumla” alisema Rais Kikwete.
Kwa upande wake, Rais wa Sri Lanka Mahinda Rajapaska pamoja na kupongeza ushirikiano wa pande zote mbili lakini pia alielezea matumaini yake kuhusiana na hatua ya ukuzaji uchumi.
Alisema serikali zote zitaendelea kushirikiana kukabiliana na matukio yanayoendelea kutokea duniani ikiwemo pia kukabiliana na vitendo vya ugaidi.




0 comments:

Post a Comment