Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 13 June 2013

Shahidi aeleza jinsi wanyama hai walivyosafirishwa




 Shahidi wa tatu  katika kesi ya kusafirisha wanyama kwenda nje ya nchi  ametoa ushahidi wake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoani Kilimanjaro na kueleza namna wanyama hao walivyopakizwa kwenye gari aina ya Fuso.

Shahidi huyo, Edward Methew Lyimo, ambaye alikuwa ni dereva aliyekodishwa kwa ajili ya kazi hiyo kutoka kwa mmiliki wa gari hilo, Nicolaus Meena, alitoa ushahidi huo mbele ya Hakimu Mkazi, Simon Kobelo.

Alidai kuwa, Novemba 25, 2010 alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Massawe akitaka gari na ndipo alipompeleka kwa Meena kutokana na gari la Tanroads kutokuwa zima.

Lyimo alidai kuwa, baada ya kufika kwa Meena walifanya malipo na kisha  alipoondoka na Massawe hadi kwenye  Chuo cha Ufundi cha Arusha  na hapo walipakiza maboksi matatu yaliyotoka kwenye Pick Up iliyokuwa ikiwasubiri.

Alieleza kwamba, baada ya kupakia maboksi hayo aliondoka hadi Kwa Mrefu ambako kuna boma la wanyama ambapo aliingiza gari hadi ambapo Massawe alimwambia asubiri kutokana na mzigo unaotakiwa kupakizwa unaandaliwa.

“Nilisubiri hadi ilipofika saa moja ambapo alianza kupakiza maboksi ya mbao makubwa yakiwa na wanyama kwenye gari jingine lililokuwapo eneo hilo kwa kutumia mashine ya gari langu (winchi) na baadae kupakiza mzigo wa aina hiyo….nilibahatika kuona twiga na swala wakiwa wanaingizwa kwenye maboksi hayo….maboksi hayo yana muundo kama wa kabati” alidai shahidi huyo.

Shahidi huyo  ambaye ni mtumishi wa Wakala wa Barabara Mkoani Arusha, alieleza baada kupakiza maboksi hayo majira ya kati ya saa 8 na saa 9 za usiku walianza safari ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

“Tulipofika pale tulisachiwa sisi madereva lakini kuna askari aliyekuwepo getini yeye alizunguka magari yetu kwa kuyaangalia na baadae tuliruhusiwa kuyaingiza uwanjani hadi ilipotua ndege na hapo nikaanza kushusha yale maboksi toka kwenye lile Fuso lililokuwa mbele yangu na baadae nikashusha kwenye Fuso langu” alieleza.

Ilidai baada ya kumaliza kushusha maboksi hayo alimlalamikia Masawe juu ya ujira aliolipwa na ndipo alipoelezwa bosi wake ambaye ni mshitakiwa namba moja Kamran Mohamed raia wa Pakistani na kumpa Sh. 30,000 kama asante na kuamua kuondoka ambapo majira ya saa 10 alfajiri.

Pamoja na Kamran Mohamed, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni,  Hawa Hassan, Martin Methew na Michael Disha ambao wanakabiliwa na kosa la kusafirisha wanyama hai 136 kwenda  Doha kwa kutumia ndege aina ya C.17.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa tena Julai  17 na 18 mwaka huu ambapo mashahidi wengine wataendelea kutoa ushahidi wao.
 

0 comments:

Post a Comment