Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 13 June 2013

Bajeti ya Zanzibar: Kodi ya mchele, ngano chini



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (smz) imetangaza bajeti ya mwaka wa fedha 2013/14 na kufanya marekebisho ya sheria 11 za viwango vya kodi ili kuziba upungufu wa bajeti wa bilioni 41.9 mwaka huu.

Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na mipango ya maendeleo Omar Yusuph Mzee alipokuwa akiwasilisha makadirio na mapato katika kikao cha bajeti kilichoanza kufanyika jana huko Chukwani mjini Zanzibar.

Waziri huyo alisema Serikali inatarajia kutumia bilioni 658.5 ambapo bilioni 353.1 kwa ajili ya kazi za kawaida na shilingi bilioni 305.4 kwa kazi za maendeleo visiwani humo.
Hata hivyo alisema kwamba bajeti ya mwaka huu inakabiliwa na upungufu wa bilioni 41.9 na serikali kuamua kurekebisha viwango vya kodi na ada hatua hiyo itaiingizia serikali bilioni 16.9 kupunguza pengo la bajeti hiyo.

Alitaja sheria za kodi zitakazofanyiwa marekebisho ni sheria ya VAT namba 4 ya mwaka 1998, sheria ya kodi za hoteli namba 1 ya mwaka 1995, sheria ya ada za bandari, sheria ya ushuru wa stempu, sheria ya kodi za mafuta, sheria ya usafiri wa barabara na kanuni zake, sheria ya kodi ya mapato, sheria ya ardhi, sheria ya kuvutia na kulinda vitega uchumi na sheria ya usimamizi wa kodi na sheria ya rufaa ya kodi ya mwaka 2006.

Aidha alisema kwamba serikali imepunguza msamaha wa kodi kwa wawekezaji na jumuiya zisizokuwa za kiserikali na kuanzia sasa italazimika kulipa asilimia 80 na asilimia 100 itabakia kwa mabalozi na miradi inayofadhiliwa kwa washirika wa maendeleo ikiwemo vifaa na huduma zinazostahiki kunufaika na msamaha huo.

"Kwa taasisi zote zitastahili kulipa asilimia 80 na kiwango kilichobakia cha asilimia 20 kitalazimika kulipiwa kodi na wawekezaji pamoja na taasisi nyingine zisizokuwa za kiserikali" alisema Waziri Omar Yusuph Mzee.

Waziri huyo alisema serikali imeamua hoteli zinazotoa huduma za kuanzia dola 45 kwa mgeni zitaendelea kulipa kodi ya ongezeko la thamani(VAT), lakini imeongeza kiwango cha kodi kutoka dola 5 hadi dola 8 kwa siku kwa hoteli za daraja la chini pamoja na kuongeza ada ya uwanja wa ndege kutoka dola 35 hadi 40 kama viwango vinavyotumika kwa nchi za Afrika Mashariki.

Waziri Mzee alisema serikali imependekeza kushusha kiwango cha ushuru wa stempu kwa bidhaa za mchele na unga wa ngano kutoka asilimia 3 hadi asilimia 2 ili kuwapa unafuu wa ukali wa maisha wananchi, pamoja na kusimamia kwa karibu udhibiti wa mianya ya ukwepaji kodi kwa wawekezaji katika sekta ya utalii zanzibar.

Kuhusu leseni za udereva serikali imeamua kupandisha kutoka shilingi 15,000 hadi 20,000 kwa mwaka mmoja 25,000 hadi 30,00 kwa leseni ya miaka miwili na 40,000 kwa lesini ya miaka mitatu kutoka shilingi 35,000.

Hata hivyo alisema kwamba vyombo vya moto vitalazimika kusajiliwa na kulipiwa kabla ya kutoka bandarini lakini kwa vyombo ambavyo vinapita njia na kusafirishwa nje ya Zanzibar vitapewa namba maalum ili kudhibiti vitendo vya gari kutumika zanzibar bila ya kusajiliwa jambo ambalo ni hatari katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Hata hivyo alisema ada ya usajili itapanda kutoka 50,000 hadi 70,000 hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato ya serikali na ni marufuku kwa mtu yeyote kutembea na gari ambayo haijasajiliwa na kupewa namba.

Aidha alisema serikali inatarajia kurekebisha sheria ya mamlaka ya uwekezaji vitega uchumi zanzibar ZIPA kwa malengo ya kufuta misamaha ya kodi kwa vifaa vya ujenzi na vyenginevyo vinavyotumika katika miradi ya hoteli na migahawa na itaendelea kutoa misamaha kwa vifaa kama vile mashine na vifaa vyengine vikubwa vya uwekezaji.

Alisema kwamba mwelekeo wa serikali ni kuimarisha uwekezaji katika sekta ya viwanda na kilimo na kutawekwa uitaratibu maalum wa kutoa nafuu katika gharama za uwekezaji katika sekta hiyo.

Kuhusu kodi ya ardhi, Waziri huyo alisema kwamba wawekezaji watalazimika kuanza kulipia kodi mara tu baada ya kukodishwa ardhi badala ya kusubiri hadi mradi utakapokamilika na kuanza kazi.

Hata hivyo alisema kwamba SMZ imegundua kuna vitendo vya ukwepaji kodi vinavyofanywa na wawekezaji hasa katika sekta ya utalii ikiwemo kushusha thamani za vyumba kwa madhumuni ya kukwepa kulipa kodi inavyotakiwa na tayari serikali imeshaanza kuchukua mkakati wa kushirikiana na bodi ya mapato zanzibar na TRA kuhakikisha mchezo huo unadhibitiwa.

Alisema mbali na sekta hiyo pia serikali imekuwa ikipoteza mapato kutokana na kutumika kwa leseni bandia za gari na kuanzia sasa malipo ya matumizi ya barabara kila dereva atalipia shilingi 35 pesa ambazo zitatozwa katika kila lita moja ya mafuta atakayonunua muhusika yawe ya petrol au diesel.

Kuhusu hali ya uchumi alisema uchumi wa zanzibar umekuwa kwa silimia 7 kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 ambapo pato la taifa limefikia bilioni 1354 mwaka 2012 kutoka bilioni 1.1 mwaka 2011.

Aidha alisema mfumuko wa bei umepungua kutoka asilimia 14.7 hadi 9.4 kwa mwaka 2012 na hali hiyo imechangiwa uingizaji wa bidhaa kwa kasi na utulivu wa bei za chakula na mafuta.
Alisema kutokana na hali hiyo serikali inarajia kufanya marekebisho wa maslahi ya watumishi wake katika mwaka ujao wa fedha, ambapo imepanga kutumia bilioni 17.5 kurekebisha mishahara na kutoa ajira mpya kwa vijana visiwani Zanzibar.

Waziri Omar alisema vipaumbele vya bajeti ni kuimarisha kiwango cha ubora cha elimu, huduma za afya katika upatikanaji wa madawa, upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wa unguja na pemba.

Aidha alisema kwamba serikali tayari imeshasaini mkataba wa kununua meli ya abiria na mizigo na kampuni ya Kimataifa ya Daewoo ya nchini Korea ya Kusini itakayogharimu shilingi bilioni 50.5 inatarajiwa kujengwa kwa kipindi cha miaka miwili na itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1200 na tani 200 za mizigo.
 


0 comments:

Post a Comment