Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 18 June 2013

Polisi wawashukia Mbowe, Lema na Nape

                                 

Jeshi la Polisi limetishia kuwakamata Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na limesema litamhoji Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye baada ya wanasiasa hao kudai kufahamu watu waliohusika na tukio la kurushwa bomu mwishoni mwa wiki iliyopita.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Arusha jana, Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja aliwataka wanasiasa hao kuwasilisha ushahidi wa kile wanachofahamu kuhusu kulipuliwa kwa bomu hilo.

Juzi, Mbowe akiwa na Lema, alisema wana ushahidi wa picha za video zikiwahusisha polisi na kulipuliwa kwa bomu hilo katika Uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za udiwani kwa Chadema, Jumamosi iliyopita.
Mkwara wa Chagonja
Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kupeleka ushahidi ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
“Tunamtaka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa askari wetu kuhusika na tukio la bomu pale Soweto. 
 Wasipofanya hivyo tutatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo kwani yeyote mwenye ushahidi unaoweza kusaidia upelelezi wa kosa la jinai akikataa kuuwasilisha kwa vyombo husika anaweza kuchukuliwa hatua,” alisema.
Nape naye kuhojiwa
Kwa upande wake, polisi limesema litamhoji Nape ambaye alikaririwa jana akidai kuwa Chadema ndiyo waliohusika na urushaji wa bomu kwenye mkutano wao baada ya kuhisi kushindwa kwenye uchaguzi wa kata nne za Jiji la Arusha.
Kamishna Chagonja alisema watamhoji ili kusaidia kazi yao ya upelelezi. Nape aliihusisha Chadema kwa kauli alizoita za kutishia amani zilizowahi kutolewa siku za nyuma kabla ya uchaguzi wa kata za Arusha.
Watatu wakamatwa
Kamishna Chagonja alisema watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio la kulipuliwa kwa bomu mkoani Arusha.
Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na watafikishwa mahakamani muda wowote ushahidi wa kutosha utakapopatikana au kuachiwa huru wakigundulika kutokuhusika.

 

0 comments:

Post a Comment