Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday 1 June 2013

MBIO ZA URAIS 2015 CCM MTO USIO ZIMIKA

                                 23Rajab,1434 Hijiriyah/ JUNY 02,2013 Miyladiyah


SIKU chache baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kumruka Waziri wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, akisema hahusiki na kundi lolote la mbio za urais mwaka 2013, Waziri Mark Mwandosya, naye ameruka akisema Ikulu bado ina mpangaji.
Wakati Profesa Mwandosya akimsuta Waziri Sitta, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja, amemshukia waziri huyo wa Afrika Mashariki kuwa ni msaliti na anapaswa kufukuzwa kwenye chama.
Viongozi hao waandamizi ndani ya CCM walitoa kauli hiyo kwa wakati tofauti mjini Dodoma na Mgeja akiitisha mkutano na wanahabari jijini Dar es Salaam.
Kauli za viongozi hao zimekuja baada ya Waziri Sitta hivi karibuni kuwataja mawaziri wenzake watatu akidai kuwa ni marafiki zake, wasafi, wasio walafi na wanaomuunga mkono katika vita dhidi ya ufisadi.
Sitta ambaye anatajwa kuwa mmoja wa makada wa CCM wanaotaka kuwania urais mwaka 2015, aliwataja marafiki zake hao wiki iliyopita kuwa ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Dk. Magufuli na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa wana mikono safi na si kama wengine walafi na waongo wanaowatumbukiza katika mikono ya Dowans na Richmond ambao si waadilifu na wazalendo.
Licha ya kutomtaja mtu kwa jina lakini wadadisi wa kisiasa wanasema kuwa alimlenga kada mwenzake, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa huo mwaka 2008 kutokana na kashfa ya Kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond.
Lowassa ni miongozi mwa vigogo wa CCM wanaopewa nafasi kubwa kuwania urais mwaka 2015 na kundi lake lenye nguvu linadaiwa kuwapa kiwewe wapinzani wake ndani ya chama.
Hata hivyo, siasa hizo za makundi na kuanza kurukana kwa wajumbe tajwa huenda zikamweka pabaya Sitta endapo atawania kiti hicho.
CCM imekuwa ikiwaonya makada wake wanaokusudia kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kutothubutu kufanya kampeni zozote kwani muda bado na kwamba atakayekiuka atakuwa amejiengua kwenye mchakato wakati ukifika.
Jambo kubwa litakalomweka pabaya Sitta katika siasa zake za kujiimarisha kuelekea mwaka 2015 ni kitendo cha marafiki aliowataja katika harambee hiyo kuwa ni washirika wake wanaomuunga mkono na kumchangia fedha kuanza kumkana.
Sitta ambaye ametangaza kutogombea tena ubunge, aliwasilisha zaidi ya sh milioni 25 ambazo alisema kati yake sh milioni tano zilitoka kwa Membe, sh milioni tano nyingine zilichangiwa na Dk. Mwakyembe na Dk. Magufuli huku yeye (Sitta) akichangia sh milioni tano.
Alitaja kuwa fedha zilizobaki ili kutimiza mchango wake wa sh milioni 25 zilichangwa na wabunge wanaowaunga mkono ambao ni Anne Kilango, Mary Nagu, William Ngeleja, Aden Rage na Catherine Majige.
Wengine ni James Lembeli, Mark Mwandosya pamoja na Victor Mwambalaswa ambao wote walimchangia sh 500,000 kila mmoja huku Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu akitoa sh milioni moja.
Hata hivyo, Magufuli amekuwa wa kwanza kukanusha kauli ya Sitta akisema hakuwahi kuchangia hata senti moja katika fedha zilizotajwa.
Katika mlolongo huo, Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na baadhi ya vigogo wa CCM waliotajwa kumchangia Waziri Sitta, likitaka kufahamu msimamo wao kama walifanya hivyo kimkakati kuelekea urais mwaka 2015 au la.
Katika maelezo yake, Waziri Mwandosya ambaye alichuana na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005, alisema ana kundi moja liitwalo CCM.
“Niko nje ya nchi kwa hiyo sina taarifa ya hayo unayoyasema kwamba yamesemwa. Hata hivyo na kama ni kweli itanishangaza. Tuna kazi ya kutekeleza ilani na ahadi zetu kwa wananchi wa Tanzania. Magogoni (Ikulu) bado ina mpangaji.
“Nilisema wakati ukifika Mwenyezi Mungu akipenda, nitatoa uamuzi. Sihitaji msemaji wala kusemewa. Mungu ibariki CCM, Mungu ibariki Tanzania,” alisema Profesa Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (asiye na Wizara Maalumu).
Naye Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, alijibu kwa kifupi kuwa: “Mimi nilimchangia laki tano kama rafiki. Mengine siyajui.”
Mmoja wa mawaziri waliotajwa katika kundi hilo, alipotafutwa aliomba apewe muda ili aweze kutoa ufafanuzi baadaye.
Mwanzoni mwa wiki hii, Dk. Magufuli alikana madai ya Sitta akisema kuwa hajawahi kuwa na ushirikiano wa kumuunga mkono katika masuala ya kisiasa wala hajawahi kumtuma akaseme chochote.
Badala yake Magufuli alisema kuwa habari hizo ameshangaa kuzisoma kwenye vyombo vya habari wakati hajawahi kufanya makubaliano yoyote na Sitta wala kuunda kundi la mbio za urais mwaka 2015.
“Naapa sijawahi kuzungumza wala kuhudhuria mkutano wa kundi lolote la mgombea urais, naomba Mungu aogopwe, watu wasiwasingizie wengine. Mimi kundi langu ni CCM,” alisema.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Magufuli alisema kwa sasa Rais ni Jakaya Kikwete, hivyo ni makosa kuanza kampeni za urais wakati muda bado.
Mgeja naye amsuta Sitta
Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, amemshukia Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kuwa ni msaliti na anatakiwa afukuzwe kwenye chama.
Mgeja alisema Sitta amekuwa wakati wote akiisaliti CCM kutokana na kauli zake zenye utata na hata kudiriki kuanzisha chama ndani ya CCM cha CCJ.
Mgeja, mmoja wa wenyeviti wenye ushawishi CCM, alimshambulia Waziri Sitta kuwa amekuwa akiunda makundi ndani ya CCM, jambo ambalo alisema ni hatari sana.
“Chama kilishakataza kujitangaza, yeye kwa nini anapitapita makanisani na kujitangaza? Sasa kuna haja ya kuongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ili apige marufuku viongozi wa siasa kufanya mikutano ndani ya makanisa na misikitini,” alisema Mgeja.
Mgeja alisema anakusudia katika kikao kijacho cha Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kumshitaki Sitta ili ajadiliwe kama bado ana sifa ya kuwa kada wa CCM.
Mgeja alimshangaa Sitta kuendelea kulalamika kuenguliwa kwenye kuwania kiti cha spika, huku akimhusisha Rais Jakaya Kikwete kwamba alihusika katika mpango huo.
“Sitta amekuwa akimtuhumu hata Rais Kikwete kuhusika kumuengua kwenye uspika huku akisahau kuwa hata yeye nafasi hiyo aliipata kwa wao kumfanyia hila Pius Msekwa na kumtaka marehemu Juma Akukweti kwa wakati huo ajitoe katika kinyang’anyiro hicho ili spika awe Sitta.
“Nasema hivi msimuone Sitta amekuwa mtu wa kulalama, anakosa fadhila tu, sisi ndio tuliomuweka pale kwenye uspika wakati ule, maana hakuwa na ubavu wa kumuondoa Pius Msekwa, lakini leo hii kasahau, hakutakiwa kusahau, anatakiwa kuiga mfano wa Msekwa, maana amekaa kimya,” alisema Mgeja.

0 comments:

Post a Comment