Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Sunday, 23 June 2013

Lombero: Nazika viungo vyangu nikiwa hai

                                        
Kwa mtu uliyekutana naye miaka saba iliyopita wakati huo akiwa dereva wa magari makubwa aliyefanya kazi zake mchana na usiku huku akilazimika kunyanyua baadhi ya mizigo mizito, si rahisi kuamini kuwa mtu huyo leo hawezi hata kufungua mlango wa gari.
Huyo si mwingine bali ni Maka Lombero (39) mzaliwa wa Bukoba, mkazi wa jijini Dar es Salaam ambaye anaishi maisha duni baada ya kukumbana na masahibu yaliyosababisha kukatwa kiungo kimoja baada ya kingine na kumwacha akiwa hana viganja vya mikono yote miwili na mguu wa kushoto.
Nilikutana na Lombero saa mbili na nusu usiku eneo la Kigogo Luhanga akiwa amekaa nje ya duka, huku ameengemea fimbo yake ya kutembelea. Nilipomsalimia alionekana ni mtu mwenye furaha asiye na wasiwasi wowote. Aliinua mkono wake uliokatika nusu na kuuelekeza kwangu akitaka nimsalimu kwa kumpa mkono.
Nilimpa mkono naye kwa furaha akaniambia: “Karibu ndugu yangu.” Huku akisogea niweze kukaa lakini kwa kuwa nafasi ilikuwa ndogo nilimwomba tuingie katika mgahawa uliokuwa karibu ili kuweze kuzungumza. Alichukua magongo yake ya kutembelea, kisha taratibu tukaingia ndani.
Alipoanza kunisimulia historia ya maisha yake ghafla furaha aliyokuwa nayo ilitoweka huku machozi yakimlenga. Kwa kuwa nilihitaji sana kujua historia ya maisha yake nilibadilisha mada kwa kumuuliza angependa kula chakula gani.
“Mimi situmii mayai, kama kuna viazi (chipsi) na mishikaki itanitosha,” alisema Lombero.
Wakati tukisubiri chakula alinieleza namna anavyokula; “Ndugu yangu, nina kula kama mbwa au paka. Ninaweka mdomo wangu kwenye sahani ya chakula na kuanza kula. Ni mateso tu niliyonayo,” anasema.
Anadokeza kuwa anahisi matatizo ya kuoza kwa viungo kulikosababisha akatwe mikono na mguu kunatokana na vitendo vya kishirikina alivyofanyiwa, baada ya kumpiga msichana mmoja ambaye aligombana naye katika mtaa wa TRM barabara ya Dodoma, Iringa mjini. “Kuna msichana tulipishana kidogo kauli akanipiga na tofali mgongoni, nilimpiga sana siku chache baadaye matatizo yalianza,” alifafanua.

Historia yake
Lombero anasema kuwa alihitimu elimu yake ya msingi mwaka 1988 huko Bukoba. Mwaka 1990 alijiunga na shule ya sekondari ya Mnazi Mmoja ya Jijini Dar es Salaam, aliposoma kwa miaka miwili na kuamua kuacha masomo kisha kwenda Tunduru kuchimba madini ya vito.
Mwaka 1995 familia yake ilimpeleka Morogoro kwenda kujiunga na Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kilichopo Kihonda, ambako alifanikiwa kupata leseni ya kuendesha magari makubwa. Baada ya kuhitimu masomo alikaa mtaani kwa siku chache kabla ya kwenda Ifakara kwa baba yake ambako alipata kazi ya kuendesha lori katika kampuni ya Zaniri.
“Ile kampuni nilikaa nayo muda mfupi tu baadaye nilikuja Dar es Salaam nikapata kazi kwenye kampuni ya Mwarabu,” anasema na kuongeza kuwa kampuni hiyo alifanya nayo kazi muda mrefu ikilinganishwa na ile ya kwanza.

 

1 comments:

  1. kweli hujafa hujaumbika. ALLAH ampe subra kaka huyu katika mtihan anakumbana nayo asikufuru.

    ReplyDelete