Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday 29 June 2013

Idadi kubwa ya vijana nchini Ufaransa hawana ajira

Ripoti kutoka Ufaransa zinasema kuwa, idadi ya vijana wasio na ajira imeongezeka mno nchini humo. Ufaransa ambayo inapitia kipindi kibaya zaidi cha kuzorota uchumi katika historia ya nchi hiyo, kama zilivyo nchi nyingine za Ulaya inakabiliwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa vijana. Taasisi ya Taifa ya Takwimu ya Ufaransa na Utafiti wa Kiuchumi imetoa ripoti yake mwezi huu wa Juni na kubainisha kwamba, kiwango cha ukosefu wa ajira nchini humo kimefikia asilimia 10.8. Kwa mujibu wa taasisi hiyo ya takwimu, kiwango hicho ni kikubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa nchini Ufaransa katika kipindi cha miaka 14 iliyopita. Taarifa zaidi zinasema, hali ya ukosefu wa ajira kwa vijana ni mbaya zaidi ikilinganishwa na matabaka mengine ya jamii kwani mmoja kati ya kila vijana wanne wa Kifaransa, hana kazi na wala uwezo wa kuwa na chanzo cha kumpatia kipato. Kwa mujibu wa takwimu rasmi, takribani vijana milioni moja na laki tisa wenye umri kati ya miaka 15 hadi 29 nchini Ufaransa hawana kazi, hawasomi na wala hawajishughulishi na kozi au ufundi wa aina yoyote. Huku hayo yakiripotiwa kiwango cha vijana wasio na ajira katika Umoja wa Ulaya kilifikia milioni 24.4 mwezi Aprili mwaka huu.
 

0 comments:

Post a Comment