Watu wengi walikosoa upandishaji wa kodi na ushuru wa bidhaa na huduma kwamba utawadidimiza walalahoi.
Bajeti ya 2013/14 iliyotangazwa bungeni juzi na
Serikali, imesababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kila upande wa
nchi, huku baadhi ya wasomi, wanasiasa na wananchi wakiiponda kwamba
haiwezi kubadili hali ya maisha ya watu wa chini.
Wengi wanakosoa nyongeza ya kodi na ushuru
mbalimbali ambazo wanasema zinazidi kudhoofisha hali ya watu wa chini,
kwani gharama za maisha zitazidi kupanda na kwamba hali hiyo
inawaneemesha walionacho.
Katika maoni yao kuhusu bajeti hiyo iliyosomwa na
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, wapo waliokosoa vikali misamaha ya
kodi ambayo wameitaja kwamba inadhoofisha uchumi wa nchi.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Humphrey Moshi aliuambia mkutano wa wadau wa uchumi
ulioandaliwa na Kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu (KPMG) jana jijini Dar es
Salaam kwamba, Serikali imeshindwa kukusanya kodi kwa wawekezaji
wakubwa.
“Misamaha ya kodi inatolewa kwa wawekezaji wakubwa
na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) inasababisha mzigo kwa Serikali.
Hizi kampuni kama za simu na madini zinapokuja kuwekeza zinatafuta
faida, hakuna sababu ya kuzisamehe kodi,” alisema Profesa Moshi.
Mchumi huyo alikosoa upandishaji wa kodi kwenye
mafuta akisema kuwa itapandisha mfumuko wa bei kwa wananchi wa chini.
“Huwezi kupandisha kodi ya mafuta, kwani ni chanzo cha kukua kwa mfumuko
wa bei kwa kaya. Nilishafanya utafiti katika hilo… ni kweli mfumuko
umeshuka, lakini kwa ngazi ya kaya bado bei ya bidhaa haijashuka. Tuna
bahati tu mvua imenyesha mwaka huu,” alisema.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Tafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), Profesa Samuel Wangwe alisema ni
bajeti nzuri ambayo inalenga kuchochea maendeleo. Alisema ili
kuhakikisha mapato mengi yanakusanywa ni lazima kuendana na ukuaji wa
teknolojia yenye lengo la kuwabaini wanaokwepa kodi. “Wale ambao
hawataki kulipa kodi kwa kutumia mifumo mipya, TRA itawabaini na
kuongeza mapato ya taifa,” alisema Profesa Wangwe.
Wasomi wengine
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Mzumbe, Dk Prosper Ngowi alisema Serikali imeendeleza utaratibu aliouita
kuwa ni mbovu wa kutegemea kukusanya kodi kutoka vyanzo vya anasa.
“Unapoweka kodi katika sigara, vinywaji na kutuma
fedha kwa njia ya simu bado si sahihi, kwani vitu hivi vinawahusu watu
wa hali ya chini hivyo unaendelea kuwaumiza wananchi wenye hali ngumu ya
maisha,” alisema Dk Ngowi.
Naye Mwenyekiti wa Infotech Investment Group, Ali
Mufuruki alisema suala la matumizi linatakiwa kuangaliwa upya kwa sababu
hakuna tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
0 comments:
Post a Comment