Wakati wananchi wakilalamikia ongezeko la tozo za ushuru na kodi
mbalimbali katika bajeti ya Serikali ya 2013/14, imebainika kuwapo
misamaha ya ongezeko la thamani (VAT) kwa bidhaa mbichi za kilimo,
mifugo na mazao hupoteza mabilioni ya shilingi kila mwaka.
Uchunguzi unaoonyesha kuwa misamaha hiyo imekuwa
ikitolewa kwa miaka sita mfululizo na kuligharimu taifa wastani wa
Sh503bilioni, fedha ambazo zingetosha kwa bajeti ya wizara kumi za
Serikali kwa mwaka wa fedha 2013/2014
Bidhaa na vitu ambavyo vimekuwa vikipewa misamaha
hiyo ni pamoja mazao ya kilimo vikiwamo nafaka na mbogamboga pia wanyama
na ndege wa kufugwa na vitu hivyo vinapatikana kwa wingi hapa nchini.
Licha ya misamaha ya kodi kuwepo kisheria, lakini
imekuwa ikitumika vibaya, hata mazao ya kilimo na mifugo inayopatikana
kwa wingi pia nchini. Mazao haya yamekuwa yakisamehewa kodi hiyo, hivyo
kuathiri uzalishaji wa ndani.
Mmoja wa watumishi katika Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) aliliambia gazeti hili kuwa: “Hakuna uchambuzi wa bidhaa
hizo, wala kuzichuja; ni holela hasa maana ya kuwa holela. Utaratibu huu
ni mbaya wala hautufai kwa namna yeyote ile”.
Bajeti yake kuu ya Serikali kwa mwaka ujao wa
fedha iliyotangazwa juzi inaonyesha kusheheni kwa ongezeko la kodi na
ushuru katika baadhi ya bidhaa, zikiwamo mafuta, soda, vinywaji vikali,
simu na matumizi yake pamoja na leseni za magari, hatua inayolenga
kupata fedha za kugharimia shughuli zake mbalimbali.
Hata hivyo takwimu zilizopatikana kutoka ndani ya
TRA zinaonyesha kuwa kwa miaka sita; kati ya 2003 na 2008, Serikali
imesamehe kodi katika bidhaa hizo ikiwamo mboga, ambayo kama ingetozwa
kwa bidhaa hizo ingeliingizia taifa zaidi ya Sh503 bilioni.
Kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kikilinganishwa
na bajeti ya jumla ya Sh497.346 bilioni iliyopitishwa na Bunge kwa ajili
ya matumizi ya wizara kumi za Serikali kwa mwaka ujao wa fedha
(2013/14).
Wizara hizo na fedha zilizotengewa kwenye mabano
ni Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira (Sh55,682,428,000),
Wizara ya Maliasili na Utalii (Sh75,681,745,000), Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo (Sh30,328,045,000), Ushirikiano wa Afrika Mashariki
(Sh20,470,107,000) na Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi (Sh67,180,225,000).
Wizara nyingine ni Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia (Sh63,147,599,460), Ofisi ya Rais – Mipango (Sh
37,696,984,000), Kazi na Ajira (Sh14,958,896,000), Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto (23,870,448,700) na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi (Sh108,330,273,040).
Tangu Jumatano wiki hii gazeti hili lilizungumza
na Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA,
Richard Kayombo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, kuhusu misamaha
hiyo, lakini hadi jana jioni aliomba apewe muda zaidi kwa kile
alichosema kuwa ni kufanya ulinganisho wa takwimu.
0 comments:
Post a Comment