Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 14 May 2013

MTUHUMIWA WA BOMU LA ARUSHA AFIKISHWA MAHAKAMANI

                          

 
Mtuhumiwa mmoja kati ya tisa waliotiwa mbaroni kuhusiana mlipuko wa bomu katika Kanisa la Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha na kusomewa mashtaka 21 yakiwamo ya mauaji na kujaribu kuua.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kamuzora, mtuhumiwa huyo, Victor Ambrose (20), dereva wa Bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa Mromboo, Arusha alisomewa mashtaka hayo yakiwamo matatu ya mauaji ya watu watatu waliofariki katika tukio hilo lililotokea Mei 5, mwaka huu.

Wakisoma kwa kupokezana hati ya mashtaka, Mawakili wa Serikali, Zachariah Elisaria na Haruna Matagane walidai Calist pia anatuhumiwa kwa makosa 18 ya kujaribu kuua.

Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kimyakimya akiwa chini ya ulinzi wa maofisa wa polisi na hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mashtaka yanayomkabili yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa tena na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.

Saa moja kabla ya Ambroce kupandishwa kizimbani saa nne asubuhi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliitisha mkutano na waandishi wa habari.

Waarabu (Waislamu) waachiwa huru

Polisi imewaachia huru raia wanne wa kigeni waliokuwa wakishikiliwa kuhusiana na tukio hilo baada ya uchunguzi uliofanywa na Polisi wa Tanzania, FBI na Polisi wa Kimataifa (Interpol) na kubaini hawakuhusika.

Kamanda Sabas aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana kuwa raia hao walikamatwa baada ya kutiliwa shaka walipoonekana wakitoka kwenye hoteli moja karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha, muda mfupi baada ya tukio hilo.

Raia watatu wa Falme za Kiarabu(UAE), walioshikiliwa na kuachiwa wamegundulika kuwa ni watumishi wa Serikali.

Kamanda Sabas aliwataja kuwa ni Abdul Azziz Mubarak (30), (Mamlaka ya Mapato), Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri (29), (Zimamoto) na Daeed Abdulla Saad (28), ambaye ni Askari wa Usalama Barabarani.

Raia hao pamoja na mwenzao, Al-Mahri Saeed Mohseen (29) kutoka Saudi Arabia, walikabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa iwapo waliingia nchini kihalali.

Pichani: Mtuhumiwa wa kurusha Bomu kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph,Parokia ya Olasiti ,Jimbo Kuu la Arusha,Victor Ambrose Calist akiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya kusomewa mashtaka 21 ya kuua na kujaribu kuua

0 comments:

Post a Comment