Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya leo amefungua rasmi Bunge la 11 la nchi
hiyo na kubainisha sera muhimu za serikali yake. Katika hotuba yake
mbele ya kikao cha pamoja cha Bunge na Senate mjini Nairobi, Rais
Kenyatta amesema ataunda baraza dogo la mawaziri na kuimarisha utendaji
wa mashirika ya kiserikali. Amesema atachukua hatua za haraka kumaliza
ufisadi uliokita mizizi serikalini. Aidha Rais Kenyatta amebainisha
ajenda ya kitaifa yenye nguzo tisa kama vile uwazi katika huduma kwa
umma, kubuni nafasi za ajira, elimu, usalama, miundombinu bora na
serikali ya ugatuzi. Aidha amesema, serikali yake itahimiza ustawi wa
viwanda na kilimo. Kwingineko Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon amesema, uchaguzi uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa,
Kenya ni mfano mzuri wa kuigwa hasa kuhusu namna ambavyo mzozo wa baada
ya uchaguzi unaweza kutatuliwa kwa njia za amani. Ban ameyasema hayo
alipohutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana Jumatatu kuhusu
namna ya kutabiri, kuzuia na kukabiliana na mizozo Afrika. Akizungumza
katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Louise Mushikiwabo
ameikosoa vikali Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC na kusema inatumiwa
kisiasa. ICC inalaumiwa na viongozi wa Afrika kuwa ina malengo ya
kisiasa na kibeberu katika kufuatilia madai yake dhidi ya Rais Uhuru
Kenyatta wa Kenya na naibu wake, William Ruto.
Sikiliza Live
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment