Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 16 April 2013

KIBAMBA , KIDILA KUHOJIWA NA POLISI LEO

JESHI la Polisi Kanda ya Kinondoni, leo linatarajia kuwahoji Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba na mratibu wake, Diana Kidila, kuhusiana na madai ya kutishiwa maisha.
Mbali na mahojiano hayo, jeshi hilo pia limefungua jalada la uchunguzi kutokana na taarifa za kutishiwa maisha viongozi hao.
Akizungumza na Tanzania Daima ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyela, alisema suala hilo lina mkanganyiko kutokana na viongozi hao kutotoa taarifa yoyote katika kituo cha polisi.
“Jana (juzi) nilipokea barua ya kutishiwa kwa viongozi wa Jukata; ilikuwa ni saa 8:00 mchana. Barua hiyo ilionyesha imeandikwa Aprili 13, mwaka huu yenye namba JKT/TPF/APRIL/2013, lakini pia ilionyesha kuwa wametoa taarifa kituo cha polisi Kijitonyama na kupewa RB namba KJN/RB/2898/2013.
“Lakini nilipofuatilia taarifa hiyo baada ya kusikia katika vyombo vya habari nikamuuliza OCS wa kituo hicho na kunieleza kuwa hakukuwa na taarifa ya viongozi hao kutishiwa bali ripoti ya kutishiwa iliyotolewa Aprili 15, mwaka huu saa 4:35 ni ya Lazaro Katembo(43), ambaye ni mlinzi katika ofisi ya Jukata,” alisema.
Kenyela aliendelea kueleza kuwa Katembo alitoa maelezo ya awali kuwa Aprili 12, mwaka huu, majira ya saa 6:15 mchana gari T126 CCG Land Cruiser ikiwa na takriban watu nane ilifika zilizoko ofisi hizo na kutaka namba ya Kibamba.
Kenyela alieleza kuwa taarifa iliyotolewa na Lazaro haikuonyesha kama ilikuwa na vitisho pia viongozi hao hawakuripoti, kufungua kesi wala kuandika maelezo katika kituo chochote cha polisi.
“Napata mashaka kutokana na barua ya viongozi hao iliyoandikwa Aprili 13, 2013 wakati RB imetolewa Aprili 15, 2013 saa 4:35 na wakawa na mkutano na waandishi wa habari siku hiyohiyo; sasa namba ya RB walitoa wapi wakati barua ni ya Aprili 13,” alihoji Kenyela.
Alisema japo viongozi hao walikaa na taarifa hiyo bila kuripoti, wao wameamua kufanya uchunguzi kutokana na kukimbilia kwenye vyombo vya habari.
“Tunachunguza kujua mbivu na mbichi, kulitafuta gari, liko wapi, dereva aliyehusika na watu waliokuwemo na pia walienda kufanya nini na baadaye nini kilitokea,” alisema Kenyela.
Alisema kutokana nafasi za viongozi hao katika jamii wataimarisha ulinzi katika ofisi zao na maeneo wanayoishi.
Pia alitoa wito kwa viongozi wowote kutoa taarifa mapema pindi wanapoona matukio kama hayo na si kukimbilia katika vyombo vya habari kwa kufanya hivyo husababisha kuharibu upelelezi.
 

0 comments:

Post a Comment