Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 16 April 2013

Wakulima wahimizwa kujiunga katika vikundi

 
WAKULIMA wa nyanya na alizeti katika vijiji vya Kising’a na Ikokoto, wilayani Kilolo, Iringa wameshauriwa kujiunga na vikundi kwa lengo la kupata mikopo.

Ushauri huo ulitolewa jana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Adam Swai, katika ofisi za Muungano wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) na kuongeza kuwa wakulima wanapokuwa wameungana inakuwa rahisi  kupata mikopo.

Alisema mikopo inajenga uwezo katika shughuli za kilimo na ikitumiwa ipasavyo inaweza kuwainua kiuchumi wakulima na  kuongeza pato la taifa.

“Hakikisheni vikundi vinakuwa imara zaidi kwa manufaa ya kilimo, hivyo ndivyo ambavyo hata mikopo inakuwa rahisi zaidi kupata kutoka katika benki zozote na kuweni na wanachama wengi kadiri muwezavyo,” alisema Swai.
Aidha, aliwashauri wakulima wa nyanya kupunguza matumizi ya dawa katika kilimo hicho hasa muda wa kuvuna, kwani ni hatari kwa matumizi ya binadamu.

Alisema matumizi ya simu katika kupeana elimu ya kilimo ni muhimu hata kama wako mbalimbali kimaeneo.
Swai aliwataka wakulima hao kuwa na tabia ya kuandaa mashamba mapema na kupanda kwa wakati  ili kuepukana na mabadiliko ya tabia nchi.

Naye mwakilishi wa ushirikiano wa wakulima wa nyanya, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ikokoto, Kestor Luhwago, alisema changamoto wanazokumbana nazo katika biashara hiyo ni soko dogo na wakati wa msimu wa mavuno wafanyabiashara wengine hupanga nyanya zao nje na ukosefu wa sehemu ya kuegeshea magari wakati wa kupakia mizigo.
'T.daima'

0 comments:

Post a Comment