TAMKO LA WANACHUO, WAFANYABIASHARA NA WAKAZI WA
IRINGA WANAOTOKA MIKOA YA LINDI NA MTWARA KUPINGA USAFIRISHAJI WA GESI ASILIA TOKA MNAZI
BAY- MTWARA KWENDA DAR ES SALAAM.
Ndugu,
Waandishi wa Habari na Wananchi wote mliohudhuria hapa kufuatia maandamano ya
wakazi wa Mkoa wa Mtwara yaliyofanyika mnamo tarehe 13 Januari 2013 sisi kama
Wanavyuo,Wafanyabiashara na Wakazi wa Iringa tunaotoka mikoa ya Lindi na Mtwara
na wadau wengine tunaungana na wenzetu wa Lindi na Mtwara KUPINGA VIKALI USAFIRISHAJI WA GESI
ASILIA toka Mnazi Bay - Mtwara kwenda Dar es Salaam. Tumeamua
kufanya hivi kutokana na sababu za msingi zenye maslahi kwa maendeleo ya Taifa
zima la Tanzania sio tu Mikoa ya Lindi na Mtwara kama inavyodaiwa na baadhi ya
viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa. Zifuatazo ni sababu
zinazotufanya tupinge usafirishaji wa gesi asilia toka Mtwara kwenda Dar es Salaam;
1. Sisi kama wazawa,wakazi wa mikoa ya Kusini mwa
Tanzania tuna haki ya kupigania haki kutokana na dhulma yeyote itakayofanyika kwa Watanzania wowote
wale na popote pale ndani na nje ya nchi hii.
2.
Kisheria na katika hali ya
kawaida rasilimali yoyote ile inayopatikana katika eneo fulani ni lazima
iwanufaishe wananchi waiishio katika eneo husika, hivyo rasilimali iliyopo
mikoa ya Lindi na Mtwara ni lazima wananchi wanufaike, kwani waswahili husema “Jungu kuu halikosi ukoko” na
“Mgeni aje mwenyeji apone” hivyo kusafirishwa kwa gesi kutawadhoofisha
wakazi wa Lindi na Mtwara na kujihisi kuwa pengine wao si wazawa wa Taifa hili.
3. Pia kumekuwa na dhulma nyingi za rasilimali na
kuzorotesha miradi mbalimbali ya maendeleo katika mikoani Lindi na Mtwara. Kwa
mfano;
a)
Kuondolewa kwa Mashine ya kuvuta maji katika vijiji vya Namitema
na Chihanga wilayani Newala kwa madai kuwa ni mbovu
hatimaye kupelekwa kutumika mkoani Dodoma.
b) Pia kuondolewa kwa taa zenye mwanga mkali katika uwanja wa ndege wa Mtwara na
kupelekwa katika viwanja vingine mkoani Arusha.
c)
Ubabaishaji uliofanywa na
serikali juu ya ahadi ya kukarabati Bandari ya Mtwara, bandari yenye
kina kirefu Afrika Mashariki na Kusini
mwa Afrika na hatimaye kujenga bandari mpya kwa kuchimba chini ya bahari
ili kupata kina kirefu huko Bagamoyo.
d) Kuahirisha ujenzi wa kiwanda cha Samaki
Mkoani Mtwara na hatimaye kwenda kujengwa Dar es Salaam.
e)
Ubabaishaji wa bei za korosho kupitia utaratibu mbovu wa stakabadhi
ghalani bila kuwashirikisha wakulima wa korosho. Utaratibu ambao kwa asilimia kubwa unawanyonya wakulima
wa zao la korosho ambalo ndio zao kuu la biashara mkoani humo. Kwa mfano;kulipwa
kwa mkopo 70% awamu ya kwanza na 30% ni awamu ya pili na wakulima wengine
hawalipwi kabisa.
f)
Kuwazuia wakulima kulima baadhi ya mazao mengine ya biashara mfano; Pamba kwa madai kwamba mazao
hayo yataharibiwa na wadudu toka nchi jirani ya Msumbuji, madai ambayo
hayana ukweli wowote ule kwani hakuna
utafiti wa kisayansi uliofanyika.
g)
Kutokamilika kwa barabara km. 60 toka Muhoro mpaka
Somanga ikiwa sasa yapata miaka takribani 10, barabara muhimu sana ambayo inaunganisha mikoa ya ukanda wa
kusini mwa Tanzania yaani Lindi na Mtwara wakati maeneo mengine katka nchi hii km.
300 hukamilika kwa muda mfupi tu.
h) Kuzorota kwa elimu katika mikoa ya Lindi na Mtwara
takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa matokeo ya Kidato cha pili 2012 Mikoa
ya Lindi na Mtwara imeshika mkia Kitaifa
haina maana kwamba ndugu zetu hawana akili ndio maana sisi wengi wetu tuko Vyuo
Vikuu, isipokuwa serikali ina
usimamamizi mbovu kama vile Upungufu wa waalimu nk.
4. Kusafirisha gesi kupeleka Dar es Salaam ni
kuendeleza tatizo la ongezeko la idadi ya watu jijini Dar es Saalam kama vile
wamachinga ambao asilimia kubwa wanatoka mikoa ya kusini yaani Lindi na Mtwara
kuja kufanya biashara ndogondogo jijini Dar es Salaam.
5. Kadhalika tunawalaani viongozi wa serikali ambao wanahujumu maendeleo
ya kusini wengine ni wakazi wa Mikoa ya Kusini wameonyesha usaliti wa wazi kabisa
kwa wananchi wao wanaowawakilisha, hivyo basi tunawapa taarifa kuwa hatuna
imani nao tena ya kutuwakilisha wananchi wa Lindi na Mtwara.
6. Tumekerwa na
baadhi ya kauli za viongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa juu ya wakazi wa
Mtwara kuhusu gesi.Mfano.Ndugu,Mwigulu Nchemba ambaye ni
Naibu Katibu wa CCM Taifa alitoa kauli chafu
katika mkutano wa CCM Taifa
Kibaha tarehe 30 Desemba 2012.
7.
Mikoa ya kusini haina vitega uchumi vikubwa vya kuliingizia pato taifa
pamoja na wananchi wa kusini, hivyo hii ni fursa pekee kwa serikali kuleta
chachu ya maendeleo kwa wakazi hawa wa kusini na sio kuwatelekeza kwa
kusafirisha gesi kwenda Dar es Salaam.
8.
Tunalaani jeshi la polisi kwa kuwachukulia hatua wale wanaofanya
mikutano ya kuhamasisha wananchi kupinga kauli ya serikali ya kusafirisha gesi
kwenda Dar es Salaam.
9.
Katika mikoa ya Lindi na Mtwara toka uhuru kuna
kero kubwa ya umeme, sasa hii ni fursa pekee kwa wakazi hawa wa kusini
kuondokana na kero hii ya giza totoro. Kwa mfano; Wilaya ya Nanyumbu
hakuna umeme kabisa na wilaya zingine
umeme usio na uhakika kama vile Masasi,Nachingwea,Liwale, Tandahimba, Newala
na Ruangwa.
Kufauatana na
hali hiyo sisi tunaitaka serikali izingatie yafuatayo kuhusu gesi asilia
iliyogundulika Mkoani Lindi na Mtwara;
1.
Kwa kuipunguzia serikali gharama katika mchakato wa ujenzi wa mabomba ya
kusafirisha gesi umbali wa km.560
toka Mtwara hadi Dar es Salaam kutumia Tsh.trilioni 1.9 iliyokopwa, badala yake ijenge kiwanda cha gesi hiyo
katika mikoa ambako rasilimali hiyo inapatikana.
2.
Kutakana na umuhimu mkubwa wa
gesi hii kwa uchumi wa taifa basi kuwe na muda wa kutosha kwa wananchi kufanya
mjadala juu ya gesi kwani hadi sasa kuna
mvutano kati ya serikali na wananchi na hii ndio demokrasia ya kweli.
3.
Kulipa nafasi Bunge tukufu kuangalia upya sera na sharia za gesi pamoja
na madini mengine kama vile Uranium.
4.
Serikali iheshimu na kuthamini mawazo na matakwa ya wananchi na sio
kufanya maamuzi kibabe kwani kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za
utawala bora na demokrasia ya kweli.
5.
Tunamkumbusha Mh. Rais Jakaya Mrisho Kikwete ahadi
yake ya mwaka 2009-2010 iliyopo
katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliahidi kwamba mikoa ya Kusini
(Lindi na Mtwara) itakuwa ni Ukanda wa Viwanda na akawahimiza wakazi wa Mtwara
kujenga hoteli za kisasa za kutosha, zimejengwa lakini wanalala wenyewe tu,
sasa ikiwa gesi asilia itasafirishwa kupelekwa Dar es Salaam ni viwanda gani
tena ambavyo vitajengwa? Hii inaonyesha dhahiri kuwa serikali inataka
kuitelekeza mikoa ya kusini katika taswira ya maendeleo ya taifa la Tanzania.
6.
Rais asiwaone viongozi wa siasa kama wachochezi kwa serikali na
wanajitafutia umaarufu bali wanaungana na wananchi wa Lindi na Mtwara kupinga
usafirishaji wa gesi kwenda Dar es Salaam kwa hoja za msingi kwa manufaa na maendeleo ya
Taifa
7.
Tunaikumbusha serikali juu ya ahadi walizoahidi kuwafanyia wakazi wa
kusini ambazo hazijatekelezwa na hazina muendelezo wowote ule kama ifuatavyo;
a) Serikali iliahidi kujenga Tawi la Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Mtwara.
b) Serikali pia iliahidi kujenga Hospitali ya Rufaa
katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
c)
Kuzorota kwa utekelezaji wa mpango wa Mtwara Corridor hadi hivi
leo.
Tunaomba Rais na wananchi wote kwa ujumla
watuelewe kwamba, hatuna maana kwamba gesi yote ya Lindi na Mtwara itumike kwa
wananchi wa Lindi na Mtwara tu, bali Kiwanda au Mitambo ya kufua umeme wa Gesi
ijengwe Lindi na Mtwara na sio Dar es Salaam.
ENDAPO
SERIKALI ITASHIKILIA MSIMAMO WAKE WA KUSAFIRISHA GESI ASILIA TOKA MNAZI
BAY-MTWARA KWENDA DAR ES SALAAM BASI HATUA ZAIDI YA HII ITACHUKULIWA.
Ahsanteni.
0 comments:
Post a Comment