Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Friday 11 January 2013

MATOKEO KIDATO CHA PILI YATANGAZWA

SERIKALI imetangaza matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2012, takwimu zikionesha kuwa nusu ya watahiniwa wameshindwa kupata alama 30, huku shule kumi za mikoa ya Lindi na Mtwara zikishika mkia.
Licha ya watahiniwa hao kushindwa kupata alama hizo, zile za ufaulu zimeongezeka kutoka asilimia 45.40 mwaka 2011 hadi kufikia 64.55 kwa mwaka 2012.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema kuwa watahiniwa 136,946 walioshindwa kupata alama 30 na wengine 23 walioonekana kudanganya watalazimika kukariri kidato cha pili mwaka huu.
Mulugo alisema kuwa watahiniwa 249,325 wataendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Ni vema ikaeleweka kuwa kukariri kidato sio adhabu bali ni kutoa fursa nyingine kwa wanafunzi hao kuweza kupata maarifa, stadi na ujuzi wa elimu ya sekondari kidato cha kwanza na pili kwa kiwango kizuri,” alisema.
Ufaulu wa watahiniwa
Kwa ipande wa ufaulu wa watahiniwa Mulugo alisema kuwa watahiniwa 249,325 sawa na asilimia 64.55 walifaulu huku wasichana wakiwa 113,213 na wavulana 136,112 kiwango kikipanda kwa asilimia 19.15.
“Watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha A, B na C walikuwa 127,981 sawa na asilimia 33.13 na waliofaulu kwa kiwango cha D ni 121,344 na alama ya juu ya ufaulu ilikuwa ni asilimia 92,” alisema.
Shule zilizofanya vizuri
Mulugo alizitaja shule za serikali kumi zilizoongoza ni Mzumbe, Tabora wavulana, Ilboru, Kibaha, Iyunga, Msalato, Malangali, Ifunda Ufundi, Samora Machel na Kilakala.
Kwa upande wa shule zisizo za serikali, Mulugo alizitaja kuwa ni Kaizerege, Marian wavulana, St Francis, Don Bosco, Bethel SABS, Marian wasichana, Don Bosco Moshi, Cannosa, St Joseph Iterambogo na Carmel.
Shule zilizofanya vibaya
Kwa upande wa shule za serikali zilizofanya vibaya ni Mihambwe, Dinduma, Kiromba, Marambo, Mbembaleo, Kinjumbi, Litipu, Luagala, Miguruwe na Napacho ambazo zote ni kutoka mikoa ya kusini – Mtwara na Lindi.
Kwa upande wa shule zisizo za serikali ni Mfuru, Pwani, Doreta, Kigurunyembe, Ruruma, At-taaun, Jabal hira, Mkono wa Mara, Kilepile na Kiuma.
Wanafunzi waliofanya vizuri
Mulugo aliwataja wanafunzi walioongoza katika mtihani huo na shule wanazotoka katika mabano kuwa ni Magreth Kakoko (St Francis) Queen Masiko (St Francis), Lukundo Manase (Kaizerege), Frank Nyamtarila (Kaizerege), Grace Msovella (St Francis), Harieth Makireye (St Francis) Robinnancy Mtitu (St Francis), Humrath Lusheke (St Francis), Mukhsin Hamza (Kaizerege) na Anastazia Kabelinde (Kaizerege).
Walimu shule za mijini
Katika hatua nyingine, Mulugo alisema kuwa kuanzia mwaka huu hakuna mwalimu atakayepangwa shule za mjini.
Hatua hiyo imetokana na ukosefu wa walimu ulioko vijijini na tabia ya walimu wengi kupenda kuishi mijini.
Akizungumza na viongozi wa kanda mbalimbali kutoka Jumuia ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Tahliso), Mulugo alisema kuwa mwalimu yeyote ambaye hataripoti katika kituo chake cha kazi ndani ya wiki mbili atakuwa amejipotezea ajira yake mwenyewe.
Akitoa nasaha kwa viongozi hao wa Tahliso, Mulugo aliwataka kuachana na tabia ya kuingiza siasa katika mambo ya elimu kwani husababisha migogoro.
Mulugo alisema kuwa zinapotokea changamoto zozote vyuoni, ni vyema wanafunzi kukubali kukaa meza moja ya mazungumzo badala ya kusisitiza migomo na maandamano ya yasiyoleta tija ambayo huaribu mfumo.
Naye mwenyekiti wa Tahliso, Amn Chakushemeire, aliwataka wanafunzi wa vyuo vyote kuacha kutumika na wanasiasa ikiwemo kuondoa chuki za itikadi za vyama vya siasa ndani ya vyuo vyao.

0 comments:

Post a Comment