Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 18 October 2012

Polisi yakataa kumpa dhamana Sheikh Ponda

Jeshi la Polisi la Tanzania limekataa kutoa dhamana kwa Sheikh Ponda Issa Ponda Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini Tanzania ambaye jana alitiwa mbaroni na jeshi la polisi jijini Dar es salaam kwa tuhuma kadhaa za kutenda jinai. Taarifa za awali zilieleza kuwa, Sheikh Ponda anatuhumiwa kuwa amehamasisha maandamano kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani, uvamizi wa kiwanja cha Chang'ombe, maandamano kidongo chekundu na hali kadhalika vurugu zilizotokea hivi karibuni Mbagala. Duru za karibu na jumuiya za Kiislamu Tanzania zimeeleza kuwa, jeshi la polisi lilimuhoji Sheikh Ponda kwa masaa kadhaa, na hatimaye kukataa kumpa dhamana mtuhumiwa huyo. Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam Afande Suleiman Kova amesema kuwa, mtuhumiwa huyo hawezi kupewa dhamana hadi pale yatakapofanyika mashauriano ya kina na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DPP. Afande Kova amesema kuwa, uchunguzi wa vurugu za Mbagala bado unaendelea, kwani kuna uwezekano wa kuunganishwa Sheikh Ponda na watuhumiwa wengine waliofanya uhalifu na uporaji Mbagala. Hata hivyo ripoti tulizopokea hivi karibuni zinaeleza kuwa, Sheikh Ponda na wenzake waliokamatwa leo wamesomewa shitaka moja tu ambalo ni la kuvamia kiwanja kilichopo Chang'ombe. Baada ya kukataliwa dhamana, washtakiwa hao wamerejeshwa rumande na kesi yao imepangwa kusikilizwa tarehe Mosi Novemba mwaka huu.

0 comments:

Post a Comment