Sikiliza Live
Monday, 22 October 2012
Mwendesha Mashtaka wa ICC awasili Kenya
Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) amewasili
nchini Kenya mapema leo na kupokelewa na viongozi wa masuala ya sheria
akiwemo Waziri wa Sheria, Eugene Wamalwa.
Bi. Fatou Bensouda atakuwa nchini Kenya kwa siku 5 ambapo anatarajiwa
kutembelea maeneo yaliyokumbwa na machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2007. Pia atatembelea kambi kadhaa za wakimbizi wa ndani pamoja
na kukutana na waathiriwa wa ghasia hizo za baada ya uchaguzi.
Taarifa kutoka ofisi ya mwanasheria huyo zinasema kuwa lengo la safari
yake nchini Kenya ni kujionea kwa karibu athari zilizosababishwa na fujo
za kisiasa pamoja na kuandaa mazingira ya kuanza kesi za washukiwa
wanne wa ghasia hizo mjini The Hague, Uholanzi mwaka ujao.
Ghasia za baada ya uchaguzi mkuu uliopita nchini Kenya zilisababisha
vifo vya zaidi ya watu 1400 huku mamia ya maelfu wakilazimika kuyakimbia
makazi yao. Wakenya wanne wakiwemo wanasiasa mashuhuri wanatuhumiwa
kuhusika na ghasia hizo na kesi zao zinatarajiwa kuanza mwezi Aprili
mwakani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment