Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 4 July 2013

mwanzo Habari Kitaifa Kitaifa Mzee Mandela kuzikwa Qunu

                           

Gari la kubeba maiti likiwasili katika eneo la Mvezo Resort kuchukua mabaki ya miili ya watoto watatu wa Nelson Mandela iliyokuwa imezikwa kinyemela katika eneo hilo na mjukuu wa kiongozi huyo, Mandla. Picha na AFP.

 Vita ya wapi atakapozikwa  Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela imefikia tamati na sasa ni rasmi kwamba atazikwa Qunu uamuzi ambao umeacha ufa na uhasama mkubwa katika familia ya kiongozi huyo.
Jana, mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela ambao ni marehemu ilitarajiwa kuzikwa upya katika eneo la Qunu, yakiwa ni mazishi ya mara ya tatu tangu walipofariki dunia katika vipindi tofauti, ukiwa ni utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya Eastern Cape.
Uamuzi huo ulimaanisha kushindwa kwa mjukuu wa Mandela, Mandla ambaye jana katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema: “Sikusudii kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama,” lakini akahusisha ugomvi katika familia ya babu yake kwamba ni vita ya fedha na mali za Mandela.
Mabaki hayo ni ya mtoto wa kwanza wa kiume wa kiongozi huyo, Makgato aliyefariki dunia 2005, binti yake wa kwanza Makaziwe (mkubwa) ambaye alifariki akiwa mchanga mwaka 1948 na mtoto wake wa pili wa kiume, Madiba Thembekile aliyefariki katika ajali ya gari 1969.
Mahakama Kuu ya Eastern Cape ilitoa uamuzi uliowapa ushindi wanafamilia 16 wa Mandela ambao walifungua madai wakiongozwa na shangazi yake Mandla, Makaziwe.
Jaji Lusindiso Pakade katika hukumu yake, mbali na kutoa amri hiyo alitaja vitendo vya Mandla kuwa ni vya aibu visivyo vya kibinadamu hivyo kutoa amri ya kufukuliwa miili hiyo na kisha kurejeshwa Qunu. Mabaki hayo yalihamishwa kutoka kijiji cha Mvezo ambako yalizikwa mara ya pili kwa kificho miaka miwili iliyopita na mjukuu mkubwa wa Mandela, Mandla ambaye pia ni kiongozi wa kimila katika kijiji hicho.
Kazi ya kufukua makaburi ya watoto wa Mandela katika eneo la Mvezo ilifanyika hadi juzi usiku chini ya ulinzi wa polisi baada ya madalali wa mahakama kutumia sururu kuvunja lango (geti) kuu la kuingia katika makazi ya Mandla.
Kwa mujibu wa msemaji wa polisi wa eneo hilo, Luteni Kanali Mzukisi Fatyela, uchimbuaji wa makaburi ulifanywa na wataalamu wa Kituo cha Afya cha Mthatha na baadaye kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho juzi usiku na jana asubuhi mabaki ya marehemu hao yalifanyiwa uchunguzi wa kimaabara kabla ya kupelekwa Qunu kwa maziko.

 
 

0 comments:

Post a Comment