Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 4 June 2013

serikali yatangaza oparesheni kuzuia ujangili wa meno ya tembo

                            

 Naibu Waziri wa mali asili na utalii, Lazaro Nyalandu akifungua kikao cha wadau wa ulinzi wa mali asili juu ya janga la ujangili wa tembo mikoa ya Nyanda za juu kusini kinachofanyika kwenye ukumbi wa siasa ni kilimo Manispaa ya Iringa. Kikao hicho kimejumuisha viongozi waandamizi wa serikali katika mikoa mitano, Taasisi za kimataifa ikiwemo INTERPOL
 Godwell  ole  Maing’ataki Mratibu Mradi wakuboresha mtandao wa maeneo yaliohifadhiwa (SPANEST) akiwasilisha mada katika mkutano wa kujadili mbinu za kutokomeza ujangili wa Tembo katika hifadhizote Tanzania, mkutano unaofanyika siku mbili katika ukumbi wa siasa ni kilimo mkoani Iringa  ukishirikisha mikoa mitano kanda yakati na nyanda za juu kusini
 
Dkt. Christopher Timbuka  Mhifadhi  mkuu hifadhi ya Ruaha akiwasilisha mada katika mkutano wa wadau wa uhifadhi wanyama poli katika ukumbi wa siasa ni kilimo manispaa ya Iringa.

SERIKALI imetangaza oparesheni kubwa inayolenga kuusaka na kuufikisha katika vyombo vya dola mtandao wa majangili wa meno ya tembo bila kujali nafasi walizonazo katika jamii.
 Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu  alisema kuanzia sasa watakaokamatwa au kugundulika kuwepo katika mtandao huo watatangazwa majina yao, wanakoishi, nchi wanazotoka na watafunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria za nchi.
 Aliwataja baadhi ya watu waliopo katika mtandao huo wa ujangili kuwa ni pamoja na majangili, wahifadhi, maafisa wanyamapori, viongozi wa serikali, wasafirishaji, idara ya uhamiaji na baadhi ya watumishi wa vikosi vya usalama nchini.
 Oparesheni hiyo inayolenga kuwanusuru tembo wachache waliobaki nchini, itakwenda sambamba na kuwasaka na kuwatia nguvuni watu wanaomiliki silaha za kijeshi kinyume na sheria za nchi.
 Aliyasema hayo kwenye kwenye kikao cha siku mbili cha  wadau wa ulinzi wa maliasili juu ya jannga la ujangili wa tembo mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, kilichoanza jana mjini Iringa.
 Aliwataja baadhi ya wadau watakaohusishwa katika oparesheni hiyo itakayoendeshwa kwa siri na intelejensia ya hali ya juu kuwa ni pamoja na kamati za ulinzi na usalama za mikoa na wilaya, vyombo vya usalama, interpol na wahifadhi.
 Alisema oparesheni hiyo itazitumia taarifa mbalimbali zikiwemo za siri kutoka kwa wadau na akawataka wananchi kuwa sehemu ya mpango wa taifa wa kuumaliza mtandao wa ujangili unaohusisha pia watu wanaofadhili ujangili.
 Alisema serikali ipo katika mchakato wa mwisho wa kuzifanyia marekebisho sheria za hifadhi zitakazokuja na adhabu kali kwa watakaohusika.
 “Serikali inawatahadharisha watu wanaojihusisha na ujangili kuacha mara moja; tunaomba wajumbe ndani ya familia watusadie kutoa taarifa au kuwasihi ndugu zao kuacha ujangili na kusalimisha silaha kwa hiari yao ili wasifikishwe kwenye vyombo vya dola,” alisema.
 Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Ole Meinng’ataki alisema ujangili wa tembo katika karne ya 21 ni tishio jipya.
 Wakati ripoti za awali zinaonesha idadi ya tembo nchini kote imepungua kutoa 109,000 mwaka 2009 hadi 70,000 mwaka 2012, Meing’ataki alisema tembo 65 hadi 70 wanauawa kila siku na takribani 10,000 kila mwaka.
 Awali Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allein Kijazi alisema makadiro yanaonesha kwamba kuwa biashara ya meno ya tembo isipositishwa, tembo wa Afrika watapotea kote ifikapo mwaka 2020.
 Alisema mbali na kuongeza fedha na juhudi za kupambana na ujangili kwa kuboresha uwezo wa askari wa doria, alisema ushawishi wa kisiasa  na kidiplomasia ni muhimu ukafanyika.
 Mbali na wakuu wa mikoa ya Iringa, Mbeya na Njombe, wengine wanaoshiriki mkutano huo utakaojadili kwa kina mbinu shirikishi katika kukabiliana na ujangili wa tembo na wanyamapori wengine  ni pamoja na wakuu wa wilaya, wahifadhi, vikosi vya usalama na Interpol, na wadau wengine wa uhifadhi. Chanzo: mjengwablog

0 comments:

Post a Comment