Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 4 June 2013

Rasimu ya Katiba Mpya yapendekeza rais apunguziwe uwezo
 Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa jana, imependekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais wa Tanzania maeneo tofauti ya utendaji wake, ukiwamo uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu wa Serikali.

Tume hiyo inapendekeza kwamba Rais ashirikiane na mihimili mingine ya dola katika uteuzi huo, huku ikiwataja Mawaziri na Naibu Mawaziri, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi kuwa uteuzi wao utakapofanywa na Rais lazima uthibitishwe na Bunge.
Mapendekezo hayo ni tofauti na hali ilivyo sasa wakati uteuzi unaofanywa na Rais hauthibitishwi na Bunge, isipokuwa nafasi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais itapotokea ikawa wazi kwa sababu zozote zile.
Pia, tume inapendekeza Rais ashauriane na chombo kipya kitakachoundwa cha Baraza la Ulinzi la Taifa kuwateua viongozi wote wa taasisi za ulinzi nchini.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema mfumo wa utawala utaendelea kuwa kama ulivyo hivi sasa na kwamba, Rais ndiye mtendaji wa Jamhuri ya Muungano na atachaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Jaji Warioba alisema Tume imependekeza mgombea urais lazima apate zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na kwamba, kinga ya kutokuhoji matokeo ya uchaguzi mahakamani iondolewe.
“Mgombea urais anaweza kupendekezwa na chama cha siasa au kuwa mgombea huru, mgombea wa nafasi hiyo atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa,” alisema Jaji Warioba na kuongeza: “Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kulalamikiwa mahakamani, lakini siyo kila mtu anaweza kufungua kesi, wanaoweza kufungua kesi ni wagombea urais na Mahakama ya Juu pekee ndiyo itakuwa na mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya mwezi mmoja, yaani siku 30.”
Alisema Tume inapendekeza Rais achaguliwe moja kwa moja na wananchi na kwamba, suala la umri pia lilijadiliwa kwa upana.
“Wengine walisema umri wa mtu kuruhusiwa kugombea urais uwe miaka 35 au 50 na kuendelea, Tume imeyachambua maoni yote na ikafanya utafiti kwa kupitia Katiba za nchi zingine ,” alisema Jaji Warioba na kuongeza:
“Wengi walioomba kugombea nafasi hiyo walikuwa na umri wa miaka 40 au zaidi, kwa kuzingatia maoni ya wananchi, utafiti na hali halisi, Tume imependekeza Rais aendelee kuchaguliwa na wananchi pamoja na sifa nyingine mtu atakayegombea Urais asiwe chini ya miaka 40.”
Kutokupunguzwa kwa umri wa urais kutakuwa ni pigo kwa wansiasa vijana nchini waliopendekeza ushushwe na kuwa miaka 35, akiwamo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.

Akizungumzia suala hilo jana, Zitto alisema uamuzi huo wa umri hana la kusema, kwa sababu yaliyotolewa ni mapendekezo ya Tume na kwamba, Chadema watatoa kauli baada ya viongozi kuwasiliana.
Kwa upande wake, Makamba iwapo amebadili msimamo wake, alisema: “Suala la umri siyo kigezo pekee cha kupata uongozi mzuri.”
Makamba alisema ujana wala uzee siyo kigezo cha kumnyima mtu uongozi.
Siku za nyuma Makamba, ambaye ni Mbunge wa Bumbuli, aliwahi kunukuliwa akitaka umri wa kugombea urais uwe miaka 35 badala ya 40 ya sasa.
Alisema suala la umri lisingemwathiri binafsi, kwani mwaka 2015 atakuwa na umri wa miaka 41.
“Ninapongeza Watanzania kwa kutoa maoni yao na kutaka vijana kupewa nafasi za uongozi,” aliongeza Makamba.    

0 comments:

Post a Comment