Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 25 June 2013

MOAT bado walia na mfumo wa digitali





Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT), wamesema kuwa bado wanaamini kwamba ni makosa kufunga mitambo ya analojia katika kipindi cha mpito cha kutoka utangazaji wa analojia kwenda dijitali, na kwamba ni jambo la busara kwa serikali kubadilisha mtazamo juu ya suala hilo.
Kadhalika, wameeleza kuwa kwa kutekeleza hayo itawaletea manufaa wananchi ambao wanaendelea kunyimwa haki yao ya kupata habari katika kipindi cha mpito.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari jana, Katibu Mtendaji wa MOAT, Henry Muhanika alisema ni jambo la busara kwa serikali kubadilisha mtazamo wake juu ya suala hilo.
Alisema mpaka sasa kuna wananchi ambao wanaendelea kunyimwa haki yao ya kupata habari katika kipindi cha mpito, na kueleza kuwa kutofanya hivyo itakuwa ni ubabe kwa upande wa waziri na serikali.
 Uamuzi wa utoaji wa taarifa huo, umefuatia baada ya kauli ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa kueleza bungeni kuwa serikali haiwezi kurudi kwenye mfumo wa analojia.
Katika maelezo hayo, Profesa Mbawara alisema kurudi katika mfumo wa analojia kutaongeza gharama hasa zile za kuendesha mitambo ya analojia.
Profesa Mbawara alisema mfumo wa dijitali unakwenda vizuri katika mikoa iliyofungwa hususan Dar es Salaam na kusema kwamba hadi Aprili, mwaka huu, ving’amuzi 250,000 vilishauzwa kati ya watu wenye runinga 600,000.
Kuhusu takwimu hizo, MOAT ilieleza kuwa zaidi ya wananchi wapatao 350,000 sawa na asilimia 60 wa Jiji la Dar es Salaam, wananyimwa haki yao ya msingi ya kupata habari.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alitoa hoja bungeni ya kuitaka serikali iangalie uwezekano wa kutoizima mitambo ya utangazaji ya analojia katika kipindi cha mpito cha kutoka utangazaji wa analojia kwenda dijitali unaoendelea nchini.

0 comments:

Post a Comment