Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Saturday, 4 May 2013

Maliasili wakiri uwapo wa ujangili,ujambazi

                         24Jumaadal Aakhir,1434 Hijiriyah/ May 04,2013 Miyladiyah
 Wizara ya Maliasili na Utalii, imekiri kuwapo kwa changamoto kubwa ya ujangili,ujambazi na wahamiaji haramu wanaojificha na kutumia vibaya Pori la Akiba la Kigosi.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), Naibu waziri wa wizara hiyo Lazaro Nyalandu, alisema tayari hatua madhubuti zimeanza kuchukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Katika swali lake Lembeli,alihoji ni lini pori hilo litapandishwa hadhi na kuwa hifadhi ya taifa kwani linapakana na makazi ya watu lakini kutokana na kutelekezwa limekuwa kichaka cha majambazi na majangili na hivyo kuwa kero.

Akijibu swali hilo, Nyalandu alikiri pori hilo kutumiwa vibaya na wahalifu hao ambapo pamoja na hatua za kudhibiti hali hiyo kuendelea kuchukuliwa, lakini alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kulipima kisayansi pori hilo ili kuona kama linakidhi vigezo vya kuwa hifadhi ya taifa.
“Suala la kupandisha hadhi mapori ya akiba kuwa hifadhi za kitaifa unahitaji utafiti wa kisayansi na katika suala hili, utafiti wa kina ufanyike ili kuona kama linakidhi vigezo vya kitaifa vya kuwa hifadhi ya taifa,” alisisitiza.

Awali, katika swali lake la msingi la Mbunge wa Mbogwe, Augustino Maselle (CCM), alitaka kujua Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza Kitalu cha Kigosi kilichopo katika Pori la Akiba la Kigosi ambacho hakina mwekezaji hali inayotoa mwanya kwa ujangili na uharibifu wa mazingira.
Akijibu swali hilo, Nyalandu, alisema wizara hiyo inatambua kuwa kitalu hicho hakijapata mwekezaji na kwamba katika kuimarisha ulinzi wa wanyapori waliopo ndani ya pori hilo, Serikali ilianzisha Kituo cha Lwahika chenye askari wasiopungua watano wanaofanya doria katika eneo hilo.

Alisema wizara hiyo pia imeendelea kuimarisha ulinzi wa eneo hilo ikiwa ni pamoja na kuidadi wanyamapori ili kutambua mwenendo, aina na idadi yao katika eneo hilo

0 comments:

Post a Comment