بسم الله الرحمن الرحيم
BismiLLaah
walhamduliLLaah Rabbil 'Aalamiyn. Was-Swalaatu was-Salaamu
‘alaa Nabbiyihi asw-Swaadiq Al-Amiyn, wa ‘alaa aalihi wa Swahaabatihi
al-Ghurr Al-Mayaamiyn, wa man Tabi'ahum bi Ihsaani ilaa Yawmid Diyn.
Amma ba’ad:
ASILI YA APRIL FOOL
Asili ya April Fool haikujulikana kwa uhakika na kuna rai mbali mbali zinazohusiana nayo.
Wengine wamesema imeanza kutokana na sherehe za majira ya kuchipua (Spring) katika ikwinoksi (siku ya mlingano) tarehe 21 Machi.
Wengine
wamesema kuwa huu ni uzushi uliochomoza France mwaka 1564 M, baada
ya utangulizi wa kalenda mpya. Wakati mtu alipogoma kukubali kalenda
mpya akaishia kuwa ni mwathirika wa baadhi ya watu ambao wamemsababisha
aathirike kufedheheka na wakamfanyia istihzai na kumtania, akawa ni
kichekesho kwa watu.
Wengine
wanasema kuwa uzushi huu umeanza asili yake katika nyakati za kale na
sherehe za mapagani zilikuwa na uhusiano na siku hasa mwanzo wa majira
ya kuchipua. Kwa hiyo hii ni kasumba ya ibada za mapagani. Inasemekana
kuwa nchi nyingine, kuwinda hakukufaulu siku za mwanzo za uwindaji.
Le poisson d'avril (Samaki wa Aprili)
Wazungu
wameiita April Fool kwa jina la 'le poisson d'avril' (Samaki wa
Aprili). Na sababu hii ni kutokana na jua linavyosogea kutoka nyumba ya
zodiaki (nyota za unajimu) ya Pisces (Nyota ya samaki) ikielekea nyumba
nyingine. Au kwa sababu ya neno la poisson ambalo maana yake ni samaki,
hivyo ni ugeuzaji wa neno la 'passion' ambayo ina maana ya 'kuteseka'.
Kwa hiyo ni alama ya kuteseka aliyovumulia Nabii 'Iysa (Alayhis Salaam)
kama walivyodai Wakristo. Na madai yao haya yalitokea wiki ya kwanza
katika mwezi wa April.
Baadhi
ya makafiri wameiita siku hii 'Siku nzima ya wajinga' kama
inavyojulikana Kingereza. Hii ni kwa sababu uongo wanaousema ili wale
wanaousikia waamini kwa hiyo wanakuwa ni waathirika wa wale
wanaowafanyia dhihaka.
Utajo
wa mwanzo kabisa kwa Lugha ya Kingereza ilikuwa ni katika gazeti la
Dreck. Siku ya pili ya Aprili 1698 M, gazeti hili lilitaja kwamba idadi
kadha ya watu walialikwa kuhudhuria uoshaji wa watu weusi katika mnara
wa London asubuhi ya siku ya mwanzo ya Aprili.
Tukio
maarufu kabisa lililotokea Ulaya tarehe 1 Aprili lilikuwa wakati gazeti
la Kingereza 'Evening star' lilipotangaza mwezi wa Machi 1746 M kwamba
siku ya pili tarehe 1 Aprili, kutakuwa na gwaride la punda mji wa
Islington Uingereza. Watu wakakimbilia kuwatazama wanyama hao na
kulikuwa na zahma kubwa. Wakaendelea kusubiri na walipochoka kusubiri,
waliuliza kutaka kujua hili gwaride litakuweko baada ya muda gani.
Hawakupata jibu, hivyo wakatambua kuwa wamekuja kufanya maonyesho yao
wenyewe kama kwamba wao ndio mapunda.
Mmoja
wao ameandika kuhusu asili ya uzushi huu kwa kusema: Wengi wetu
tunasherehekea siku inayojulikana kuwa ni April Fool, au ikiwa
itafasiriwa kihalisi 'Siku ya Ujanja'. Lakini je, tunajua siri chungu
inayohusikana na siku hii?
Habari nyingine ambazo usahihi wake umetiliwa shaka na wanahistoria ni kuwa:
Waislamu
walipotawala Hispania (Spain) takriban miaka elfu iliyopita, kulikuwa
na nguvu kubwa ya utawala wa Kiislam ambayo haikuwezekana kuivunja.
Wakristo wa Kimagharibi walitamani kuufuta Uislamu katika mgongo wa
ardhi na walifaulu kwa kiwango fulani.
Walijaribu
kuzuia Uislamu kusambaa Hispania na walitaka kuuzima na wautoweshe
kabisa lakini hawakufaulu, ingawa walijaribu mara nyingi bila ya
kufaulu.
Baada
ya hapo, makafiri walituma majasusi Hispania kufanya utafiti ili kujua
siri ya nguvu za Waislamu ambayo haikuwezekana kuishinda. Wakatambua
kuwa kushikamana na Taqwa (Ucha Mungu) ndio sababu.
Wakristo
walipotambua siri ya nguvu za Waislamu, wakaanza kufikiria mikakati za
kuvunja nguvu hiyo. Na kwa ajili hii wakaanza kupeleka ulevi na sigara
bure huko Hispania.
Mbinu
hizi kwa upande wa Magharibi zilifaulu kuleta taathira na imani za
Waislamu zikaanza kulegea, hasa miongoni mwa vizazi vipya Hispania.
Matokeo yake ni kwamba Wakristo Wakatholiki waliikandamiza Hispania
nzima na wakauangamiza utawala wa Kiislamu katika ardhi hiyo,
utawala ambao ulidumu zaidi ya miaka mia. Ngome ya mwisho ya Waislamu
Grenada ilianguka tarehe 1 Aprili, hivyo wakaichukulia kuwa ni 'Siku ya
Ujanja ya Aprili' au 'Siku ya Wajinga ya April'. Ujanja kwa wale
walioufanya, na Ujinga kwa wale waliofanyiwa na kutumbikia ndani yake.
Tokea
mwaka huo hadi sasa, wanasherehekea siku hii na wanachukulia kuwa
Waislamu ndio wajinga. Hawakuuhusisha ujinga huu na jeshi la Granada
pekee kuwa ni wajinga, bali wamekusudia kuwa ni Umma wa Kiislamu mzima
kuwa ni wajinga.
Hata
hivyo, habari hizi tumezinukuu hapa kwa kuwa zimeenea sana miongoni wa
Waislam, lakini kama tulivyotangulia kueleza, ni kuwa, uhakika na ukweli
wake una mashaka kwa sababu kuna wanaosema kuwa wakati huo sigara na
uvutaji tumbaku ulikuwa haujaanza hadi baada ya kushindwa Waislamu huko
Hispania. Wahahistoria wanasema sababu za kushindwa Waislamu zilikuwa ni
wenyewe kujiingiza zaidi kwenye mapenzi ya kidunia na starehe, pamoja
na kuacha mafundisho sahihi ya Uislam na badala yake kuchanganya zaidi
na falsafa ya Kigiriki na kutegemea zaidi fikra za kirumi katika
kuendesha mambo yao badala ya mwongozo imara wa Kiislam. Kadhalika kuna
Waislamu waliokuwa wakishirikiana na makafiri katika kupambana na
makundi mengine ya Kiislam waliyokuwa hawaelewani nayo kama tunavyoona
leo hii.
BAADHI YA UDANGANYIFU WANAODANGANYANA WATU KATIKA
SIKU HII YA APRIL FOOL
Wengine
wanapewa habari ya mmoja wa kipenzi chake katika familia kama mtoto,
mke au mume kwamba amefariki na kwa wengine taarifa hizo husababisha
hata kifo chao kutokana na kutokustahamili kupata mshtuko huo. Wengine
wanapewa habari ya kufukuzwa kazi, au kuwashtua kwa habari mbaya kama
kuunguliwa moto nyumba yake, au familia yake kupata ajali, na
husababisha aathirike mtu kwa mshtuko huo hadi apate maradhi ya moyo, au
maradhi ya kupooza au hata kifo cha ghafla.
Wengine wadanganywe kuwa wake zao wameonana na wanaume wengine, jambo ambalo husababisha mauaji au talaka ya wake.
Kuna
visa visivyokuwa na mwisho na matukio yanayotokea kutokana na uongo
huu. Uongo ambao umeharamishwa katika Uislamu na ambao haukubaliwi
katika tabia za kiungwana.
HUKUMU YA UONGO KATIKA UISLAMU
Uongo
ni tabia ovu kabisa ambao dini zote na mfumo wa elimu za maadili
zimeonya dhidi yake, na pia asili ya kimaumbile ya binaadamu (fitrah)
inakubaliana kuwa ni uovu.
Ukweli
ni moja wa nguzo ambayo maadili ya maisha ya kiduniya yanategemea ili
yahifadhike. Ni asasi ya tabia za kustahili kusifiwa, ni msingi wa Utume
na matokeo ya Taqwa. Isingelikuwa ni ukweli, hukumu za shari'ah za
kufunuliwa kutoka mbinguni zingeliporomoka. Kuwa na tabia ya uongo ni
ujamaa wa kupukusa tabia pekee ya ubinaadamu, kwani kuzungumza uongo ni
uangamizaji wa hali ya kibinaadam.
(Bariyqah Mahmuudiyah, Muhammad al-Khaadimi, 3/183)
Shari'ah
ya Kiislamu; Qur-aan na Sunnah inatuonya kusema uongo na kwa
makubaliano ya wanachuoni kwamba ni haramu. Mtu muongo atachuma malipo
mabaya duniani na Akhera.
Katika
shari'ah, kuongopa hakuruhusiwi ila katika hali fulani ambazo
hazipotezi haki za mtu, au kumwaga damu au kufedhehesha, au kumvunjia
mtu heshima yake. Bali katika mas-ala ya kuokoa maisha, kusuluhisha
baina ya watu au kujenga mapenzi baina ya mume na mke umeruhusiwa uongo.
Wala Shari'ah haikumruhusu mtu aseme uongo wa utani usio na maana kama
huu wa April Fool.
MAKATAZO YA KUSEMA UONGO
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:
((إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللّهِ وَأُوْلئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ))
((Wanaozua uongo ni wale tu wasioziamini Ishara za Allaah. Na hao ndio waongo)) [An-Nahl: 105]
Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah hiyo:
"Allaah
Anatuambia kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
sio mzushi au muongo, kwa sababu ni watu waovu tu ambao hawaamini alama
za Allaah, makafiri na wanafiki wanaojulikana baina ya watu kwa uongo
wao, uongo kuhusu Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
wa sallam).
Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mkweli
kabisa miongoni mwa watu, mcha Mungu, mwenye elimu bora kabisa, mwenye
matendo mema, tabia njema. Hakuna aliyekuwa na shaka naye hadi kwamba
aliitwa 'Al-Amiyn' (Mkweli). Hivyo Hercules, mfalme wa Rome alipomuuliza
Abu Sufyaan kuhusu tabia za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam), jambo moja alilouliza lilikuwa ni: "Je, mmepata
kumtuhumu kwa uongo kabla ya kusema aliyoyasema?". Alijibu: "Hapana".
Hercules akasema: "Ikiwa alijiepusha kusema uongo kwa watu basi hawezi
kusema uongo kuhusu Allaah". [Tafsiyr Ibn Kathiyr, 2/588].
Imetoka
kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Alama za munaafiq ni tatu;
akizungumza husema uongo, akitoa ahadi huivunja, akiaminishwa kwa kitu
hufanya khiyana" [Al-Bukhaariy na Muslim]
UONGO ULIO MUOVU KABISA
1. Uongo Kuhusu Allaah Na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa aalihi Wa Sallam)
Huu
ni uongo wa hatari kabisa na anayezua hivyo basi hupewa onyo kali.
Baadhi wa Maulamaa wamesema kwamba anayezua uongo kama huu basi
ashutumiwe kuwa kafiri.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
((قُلْ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللّهِ الْكَذِبَ لاَ يُفْلِحُونَ))
((Sema: Hao wanaomzulia uongo Allaah hawatofanikiwa)) [Yuunus: 69]
Imetoka
kwa 'Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msinizulie uongo. Yeyote
atakayezua uongo kuhusu mimi basi ataingia motoni)) [Al-Bukhaariy]
Imetoka
kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayenizulia uongo basi
ajitayarishie makazi yake motoni)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ibnu
Al-Qayyim amesema kuhusu maana ya Hadiyth hii kwamba: "Yeyote
atakayezua uongo kuhusu mimi basi ajitayarishie makazi yake motoni
ambako ataishi milele, na sio kama kambi ambayo mtu huishi kwa muda
kisha akahamia kwengine" [Twariyqul-Hijratayn ukurasa 169]
2. Uongo Katika Kununua Na Kuuza
Uongo mwengine ni wakati mtu anapofanya biashara na katika kununua huzua na kuuza pia hudanganya.
Imetoka
kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu watatu ambao Allaah
Hatosema nao siku ya Qiyaamah na wala Hatowatazama wala kuwatukuza, na
watapata adhabu iumizayo)) Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) alisema mara tatu. Abu Dharr akasema: "Waangamizwe na wapotezwe,
ni nani hao ewe Mjumbe wa Allaah?" Akasema: (([mwanaume] Mwenye kuachia
nguo yake ivuke kiwiko cha mguu, mwenye kujisifu, na mwenye kufanya
biashara yake kwa kuapa uongo)). [Muslim]
Imesimuliwa
na Hakiym bin Hizaam (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba "Mtume (Swalla
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wawili wanaohusika
na makubaliano ya biashara wanayo khiyari (ya kuvunja makubaliano) hadi
watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano yao yatabarikiwa na
wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa katika makubaliano yao))
[Al-Bukhaariy na Muslim]
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:
Allaah
Ameusia ukweli na uaminifu, na Ameharamisha uongo na khiana katika
mambo yapasayo kujulikana na kufunuliwa kwa watu kama alivyosema Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
((Watu wawili wanaohusika na makubaliano ya biashara wanayo khiari (ya
kuvunja makubaliano) hadi watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano
yao yatabarikiwa na wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa
katika makubaliano yao)) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ لِلّهِ شُهَدَاء بِالْقِسْطِ وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى))
((Enyi
mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa
ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya
uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchaji
Allaah)) [Al-Maaidah: 8] [Minhaajus-Sunnah 1/16]
3. Kuharamishwa Uongo Kuhusu Njozi Na Ndoto
Hii ni kuhusu baadhi ya watu wanaodai kuwa wameona ndoto kadhaa kisha asubuhi wanawasimulia watu mambo ambayo wala hawakuyaona.
Imetoka
kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayesimulia ndoto
ambayo hakuiona, ataamrishwa (Siku ya Qiyaamah) aunganishe pamoja chembe
mbili za shayiri, lakini hatoweza. Yeyote atakayetega masikio (kwa
umbea) kusikiliza mazungumzo ya watu ambao wasingelipenda (yeye
asikilize), au ambao wanamuepuka atamiminiwa shaba ya moto iliyoyeyushwa
katika masikio yake siku ya Qiyaamah. Na Yeyote atakayetengeneza
(kuchora au kuchonga) picha ataadhibiwa na ataambiwa aitie uhai (roho)
na wala hatoweza)) [Al-Bukhaariy]
Al-Manaawiy
amesema: "Kuunganisha shayiri mbili, lakini hatoweza kufanya hivyo" kwa
sababu kuiunga moja kwa mwenziwe haiwezekani kikawaida. Ataadhibiwa
mpaka aweze kuziunga, na wala hataweza kuziunga. Kama kwamba anasema,
ameshurutishwa kufanya jambo asiloliweza na anaadhibiwa kwa hilo. Hii ni
sitiari ya adhabu inayoendelea. Sababu ya kutajwa shayiri hasa, ni
kwamba ndoto zina uhusiano na hisia (Kwa Kiarabu hisia ni shu'uur),
maneno ya shayiri na shu'uur yanatokana na mzizi (asili ya neno) mmoja
katika Kiarabu.
Adhabu
ya aina hii ya uongo ni kali sana ingawa anapokuwa macho huenda
akasababisha madhara zaidi, kwa sababu huenda yakahusiana na kutoa
ushahidi na huenda yakampelekea kuuliwa au kupewa adhabu ya hadd. Hii ni
kwa sababu kusema uongo kuhusu ndoto ni kumzulia Allaah (Subhaanahu wa
Ta'aala) kwani ndoto ni sehemu ya Utume, hivyo zinatoka Kwake. Na
kumzulia Muumba ni hatari zaidi kuliko kuwazulia viumbe.
[Faydhul-Kabiyr 6/99]
4. Kuharamishwa Kusema Kila Anachokisikia Mtu
Imesimuliwa
kwamba Hafsw bin 'Aaswim amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema: ((Inatosheleza kuwa ni uongo kwa mtu
anayesema kila anachokisikia)) [Muslim]
"Kutokana
na maana ya Hadiyth kuhusu maudhui hii, tunaona kwamba inakatazwa
kutaja au kuhadithia kila jambo analolisikia mtu, kwa sababu kawaida mtu
anasikia yote ya kweli na uongo. Kwa hiyo ikiwa atasema kila
anachokisikia atakuwa anasema uongo kwa kusema jambo lisilotokea.
Tumetaja juu rai za watu wakweli, kwamba uongo una maana kwamba kusema
au kuelezea jambo katika hali dhidi ya lilivyotokea. Sio sharti juu yake
ikiwa limefanyika makusudi lakini kufanyika kwake makusudi
kunashurutisha kuwa ni dhambi. Na Allaah Anajua zaidi" [Sharh Muslim
1/75]
5. Uongo Wa Utani
Watu
wengine wanadhania kwamba inaruhusiwa kusema uongo wakati wa utani. Na
huu ndio udhuru wanaoutoa katika kuongopa siku ya terehe 1 Aprili au
siku nyinginezo. Hayo ni makosa. Hakuna msingi wa jambo hili katika
sharia safi. Kuongopa ni haraam ikiwa ni kwa kutania au kwa dhati.
Kuongopa kwa kutania ni haramu sawa sawa na kuongopa kwa aina yoyote
nyingine.
Imesimuliwa
kwamba 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mimi hutania lakini sisemi ila
ni ya kweli)) [At-Twabaraaniy
katika 'Al-Mu'jam Al-Kabiyr 12/391 – Hadiyth hii imepewa daraja ya
hasan na Al-Haythamiy katika Majma' Az-Zawaaiyd 8/89 na Shaykh
Al-Albaaniy ameipa daraja ya sahihi katika Swahiyh Al-Jaami' 2394]]
Imesimuliwa
kwamba amesema: "Walisema, ee Mjumbe wa Allaah, unafanya utani na
sisi". Akasema: ((Lakini nnayoyasema ni ukweli tu)) [At-Tirmidhiy]
'Abdur-Rahmaan
bin Abi Layla amesema: "Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) wametuambia kuwa walikuwa safarini pamoja na Mjumbe wa
Allaah. Mtu mmoja miongoni mwao alilala na baadhi yao walikwenda
kuchukua mishale yake. Alipoamka alishtuka (alipoona mishale yake
haipo). Watu wakacheka. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) akasema: ((Mnacheka nini?)) Wakasema: "Hakuna kitu isipokuwa
tumechukua mishale yake na ameshtuka". Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) akasema: ((Haimpasi Muislamu kumtisha Muislamu
mwingine)) [Abu Daawuud, Ahmad na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']
Imesimuliwa
kutoka kwa 'Abdullaah bin As-Saa'ib bin Yaziyd kutoka kwa baba yake,
kutoka kwa babu yake kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) akisema: ((Haimpasi yeyote katika nyinyi kuchukua kitu
cha ndugu yake, ikiwa ni kwa utani au kwa vyovyote. Yeyote aliyechukua
kijiti cha ndugu yake basi akirudishe)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami']
6. Kuongopa Wakati Wa Kucheza Na Watoto
Lazima
tutahadhari na kusema uongo tunapocheza na watoto kwa sababu itaandikwa
katika kitabu cha hesabu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) ameonya jambo hili.
Imesimuliwa kwamba 'Abdullaah bin 'Aamir (Radhiya Allaahu 'anhu) alisema: "Siku moja mama yangu aliniita wakati alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameketi
nyumbani kwetu. Akasema: Njoo hapa nikupe (kitu). Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Je, unataka kumpa nini?))
Akasema: 'Nitampa tende'. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) akasema: ((Kama usingelimpa basi ungelikuwa unasema uongo)).
Na
imesimuliwa kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote
atakayemuambia mtoto 'njoo hapa uchukue hii' kisha asimpe kitu basi
itahesabiwa ni uongo)) [Abu Daawuud na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami']
7. Uongo Ili Kuchekesha Watu
Imesimuliwa
kwamba Mu'aawiyah bin Hadah amesema: "Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ole wake mtu anayezungumza kwa
ajili ya kuwachekesha watu na akasema uongo, ole wake, ole wake)) [At-Trimidhiy akisema ni hadiyth hasan na Abu Daawuud]
ADHABU KWA AJILI YA KUSEMA UONGO
Mwenye kusema uongo amepewa onyo kali la adhabu ya hizaya duniani na adhabu kali Akhera nazo ni kama zifuatazo:
Unafiki Katika Moyo
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:
((فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ يَكْذِبُونَ))
((Basi
Akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapokutana Naye, kwa
sababu ya kuwa walimkhalifu Allaah katika yale waliyomuahidi, na kwa
sababu ya kusema kwao uongo)) [At-Tawbah: 77]
'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Unaweza kumjua mtu mnafiki kwa mambo matatu; anaposema anaongopa, anapotoa ahadi anaivunja, anapoaminiwa na amana hufanya khiyana". Akasema: "Someni aya hizi:
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللّهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ))
((فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُواْ بِهِ وَتَوَلَّواْ وَّهُم مُّعْرِضُونَ))
((فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ يَكْذِبُونَ))
((Na
miongoni mwao wapo waliomuahidi Allaah kwa kusema: Akitupa katika
fadhila Yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao
mema))
((Alipowapa katika fadhila Yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza))
((Basi
Akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapokutana Naye, kwa
sababu ya kuwa walimkhalifu Allaah katika yale waliyomuahidi, na kwa
sababu ya kusema kwao uongo)) [At-Tawbah: 75-77]
[Muswanaf Ibn Abi Shaybah, 6/125]
Uongo Humpeleka Mtu Motoni
Imesimuliwa
kwamba 'Abdullaah bin Mas'uud amesema: " Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi
wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukweli ni utiifu, na utiifu
huelekeza Peponi. Mtu ataendelea kusema ukweli hadi Ataandikiwa na
Allaah kuwa ni mkweli. Uongo ni uovu, na uovu huelekeza motoni. Mtu
ataendelea kusema uongo hadi Ataandikiwa kuwa ni muongo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
As-Swan'aaniy amesema:
"Hadiyth
hii inaonyesha kwamba yeyote anayeendelea kusema ukweli, itakuwa ni
wasifu wake, na yeyote anayesema uongo makusudi na kuendelea, itakuwa ni
wasifu wake. Hii ni sawa kama kitendo chochote kingine chema au kiovu.
Mtu akiendelea nacho kinakuwa ndio sifa yake.
Vile
vile Hadiyth hii inaonyesha jinsi gani ilivyo muhimu kusema ukweli hadi
kwamba unampeleka mtu Peponi na imeonyesha vipi ubaya wa kusema uongo
hadi unampeleka mtu motoni. Juu ya hivyo, bado kuna matokeo ya adhabu za
duniya kwani anayesema ukweli atakuwa anakubaliwa usemi wake na watu na
ushahidi wake utakubaliwa na jaji na atapendwa kwa yale anayoyasema.
Ama mtu muongo ni dhidi ya hayo." [Subul-As-Salaam 2/687]
Ushahidi Wake Utakanushwa
Ibnul-Qayyim amesema kuhusu sababu ya ushahidi wa mtu muongo kukanushwa:
"Sababu
ya nguvu kabisa kwa nini katika kutoa ushahidi, fatwa na ripoti
zikanushwe ni kusema uongo, kwa sababu inafisidi asili ya ushahidi,
fatwa au taarifa. Ni kama ushahidi wa kipofu kuona mwezi mpya, au
ushahidi wa kiziwi kuhusu kusikia kuruhusiwa kuingia mtu mahali. Ulimi
unaoongopa ni kama baadhi ya uelekevu ambao haufanyi kazi tena. Hakika
ni mbaya zaidi kuliko hivyo, kwani kitendo kiovu kabisa mtu kumiliki ni
ulimi muongo." [I’ilaam Al-Muwaqqi'iyn 1/95]
Nyuso Kuwa Nyeusi Duniani Na Akhera
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:
((وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُواْ عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ))
((Na
Siku ya Qiyaamah utawaona waliomsingizia uongo Allaah nyuso zao
zimesawijika (zimekuwa nyeusi). Je! Si katika Jahannamu makaazi ya
wanaotakabari?)) [Az-Zumar: 60]
Ibnul-Qayyim
amesema: "Hivyo siku ya Qiyaamah Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aala)
Atazifanya nyuso ziwe alama za waliosema uongo kuhusu Allaah na Mjumbe
Wake. Kusema uongo kunaleta taathira kubwa ya kufanya nyuso ziwe nyeusi
na kuzifunika na kitambaa cha hizaya na kila mtu mkweli ataziona nyuso
hizo. Wasifu wa mtu muongo utatambulikana dhahiri kabisa usoni na kila
mtu aliye na macho ataweza kumuona. Lakini Allaah (Subhaanahu wa
Ta'aala) Anambariki mtu mkweli kwa hadhi na heshima ili yeyote
atakayemuona atamuheshimu na kumpenda. Na Atampa muongo fedheha na aibu
ili yeyote atakayemuona atamchukia na kumdharau. Na Allaah Ni Mwenye
Chanzo cha Nguvu" [A'alaam Al-Muwaqqi'iyn 1/95]
Mtu Muongo Atachanwa Mashavu Yake Kutoka Kisogoni
Imesimuliwa kwamba Samurah ibn Jundub (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:"Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaambia mara
kwa mara Maswahaba zake: ((Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliyeona
ndoto?)). Kisha yeyote aliyejaaliwa na Allaah ataelezea ndoto yake. Siku
moja alituambia: (([Malaika] Wawili walinijia jana usiku na kuniamsha,
kisha wakaniambia: 'Twende…' Tukatoka na kwenda hadi tukafika kwa mtu
aliyelala chali na mwengine amesimama juu ya kichwa chake akiwa na
ndoana ya chuma. (Akashtuka aliyoyaona na kusema) Na kitu gani cha
kutazama! Alikuwa akitia ndoana katika upande mmoja mdomoni mwa mwenzake
(aliyelala) akimchana kutoka upande mmoja wa uso hadi nyuma (ya shingo)
na hivyo hivyo akiichana pua kutoka mbele hadi nyuma ya macho yake
kisha akiendelea kufanya hivyo hivyo kama alivyofanya kwa upande
mwingine. Hawahi kumaliza kumchana upande mmoja ila upande mwingine
unarudishwa hali yake (ya mwanzo). Kisha hurudia kufanya hivyo hivyo
upya tena. Nikasema kwa Maswahaba zangu (Malaika) wawili, 'Subhaanahu
Allaah! Ni watu gani hawa wawili?' Wakaniambia: 'Endelea kwenda, endelea
kwenda!' (kisha akasema akielezea vipi Malaika wawili wakielezea mambo
aliyokuwa akiyaona): 'Ama yule mtu uliyemuona kuwa anachanwa mdomo, pua
na macho yake, ni alama ya mtu anayetoka nyumbani kwake asubuhi na
kusema uongo mwingi hadi unasambaa duniani kote')) [Al-Bukhaariy]
KAULI ZA MASWAHABA KUHUSU UONGO
Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'anhu):
"Tahadharini na uongo kwani hauna uhusiano na Iymaan".
'Umar Ibnul-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu):
"Iymaan ya dhaati haiwezi kupatikana hadi mtu aache uongo wa utani"
'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu):
"Mtu
atasema ukweli na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya
uovu katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano. Au mtu atasema
uongo na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya ukweli
katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano".
Vile vile amesema: "Haimpasi mtu kusema uongo ikiwa ni kwa kutania au kikweli". Kisha Ibn Mas'uud akasoma Ayah:
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ))
((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli)) [At-Tawbah: 119]
Sa'ad bin Abi Waqqaasw (Radhiya Allaahu 'anhu)
"Muumini anaweza kuwa na sifa zote isipokuwa usaliti na uongo"
[Muswannaf Ibn Abi Shaybah, 5/235, 236]
AINA YA UONGO UNAORUHUSIWA
Uongo
unaruhusiwa katika hali tatu; kwenye vita, kusuluhisha baina ya watu
wawili waliogombana, mume kumuongopea mkewe au kinyume chake kwa ajili
ya mapenzi na maelewano.
Imesimuliwa
kutoka kwa Ummu Kulthuum bint 'Uqbah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba
amemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Sio muongo mwenye kupatanisha baina ya watu na akasimulia jambo zuri
au akasema maneno mazuri)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Imesimuliwa
kwamba Asmaa bin Yaziyd amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) amesema: ((Hairuhusiwi kusema uongo isipokuwa katika
hali tatu; mtu anapozungumza na mkewe katika njia ya kumfurahisha,
kusema uongo katika vita, na uongo kwa ajili ya kusuluhisha baina ya
watu)) [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']
KHITIMISHO
Baada
ya kutambua chanzo cha siku hiyo ya April Fool, uongo na madhara yake,
basi tujitahidi nafsi zetu kutosherehekea siku hiyo kabisa, ili tubakie
katika tabia ya ukweli daima. Hata kama si muhimu kujua chanzo cha siku
hii, bali lililo muhimu ni kujua hukumu ya kusema uongo na khofu ya
adhabu zake kama tulivyopata mafundisho katika Aayah na Hadiyth
zilizotangulia.
Hiyo
ni shari'ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ambayo ina Hikma
inayorekebisha nafsi za binaadamu kubakia katika hali ya fitrah (asili
ya maumbile) ili abakie binaadamu daima ni mwenye kuishi salama na amani
katika jamii, na vile vile ajiepushe na adhabu kali Alizoziandaa Mola
Mtukufu kwa maovu kama hayo.
Mafundisho
muhimu na yatakayoonekana mapya kwa wengi wetu tunayoyapata katika
makala haya ni kujihadhari na matani yaliyojaa uongo; tukitazama matani
mengi hadi yawe matani basi kutakuwepo na uongo ndani yake, na utani
haufurahishi kwa wengi hadi uwe na udanganyifu na hila ndani yake, hivyo
tujihadhari sana Waislam na uongo kwenye matani. Vilevile tujiepushe na
tabia mbaya ambayo baadhi yetu wanaipenda, nayo ni kuleta matani watu
wacheke, au kuwafurahisha watu kwa matani. Kuna watu kazi yao kukaa
vijiweni na kumwaga matani hadi wakawa wanajulikana kwa sifa hiyo na
wasipoonekana siku moja ni pengo kwenye kijiwe! Hadi inafika mtu jina
lake kubadilishwa na kuitwa Fulani Matani! Na kuna wengine ambao tabia
yao ni kupenda kuwa katika mwangaza daima (kuonekana) na kuwa na tabia
ya kujipendekeza na haswa kwa watu wa jinsia tofauti ili akusanye sifa
au kupendeka, mwisho akawa anajulikana kwa kufanya sifa hizo na vituko
ambavyo vimejaa uongo, matusi, kuigiza wenzake, kebehi n.k.
Kadhaalika, tuifuate Hadiyth isemayo: ((Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho, aseme kheri (maneno mazuri/ukweli) au anyamaze...)) [Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Tunamuomba
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aturuzuku ukweli daima na Ajaalie ndimi
zetu ziseme yanayopasa tu kusema na Atujaalie miongoni mwa walioamini na
wasemao kweli (Swiddiyqiyn). Aamiyn.
0 comments:
Post a Comment