Duru za Pentagon zimeeleza kuwa, Waziri wa Ulinzi wa Marekani Chuck Hagel aliwasiliana na mwenzake wa Misri Jenerali Abdul-Fattah al Sissi mara mbili wiki iliyopita huku Misri ikiwa katika mgogoro.
Afisa wa habari wa Pentagon George Little amesema hayo na bila kutoa maelezo zaidi, ingawa wengi wanaamini kuwa, kuna mkono wa Marekani katika matukio yanayojiri nchini Misri. Hii ni katika hali ambayo baada ya kupinduliwa Mursi, Rais Barack Obama wa Marekani amesema kwamba, ana matumaini demokrasia itaimarishwa tena nchini Misri kwa kuchaguliwa serikali mpya.
Saudi Arabia na Imarati zimekaribisha kuteuliwa Adly Mansour kuwa kiongozi wa mpito wa Misri baada ya Mursi kung'olewa madarakani na jeshi. Jeshi la Misri lilichukua uamuzi wa kumuondoa madarakani Rais Muhammad Mursi baada ya maandamano makubwa ya kumpinga na baada ya kutoa muda wa masaa 48 ya kutatuliwa mgogoro huo yaliyomalizika hapo jana. Hata hivyo Musri amesema kupitia mtandao wake wa Facebook kuwa, anapinga uamuzi huo wa jeshi aliouita kuwa ni mapinduzi ya kijeshi na amewataka Wamisri kuheshimu katiba na sheria na kutoliunga mkono jeshi.
0 comments:
Post a Comment