CHAMA cha Wananchi (CUF) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wameingia katika mvutano mkali kuhusu mateso yanayodaiwa kufanywa na askari wa jeshi hilo dhidi ya viongozi wa chama hicho na raia mkoani Mtwara.
Wakati CUF wakizitaka asasi za kiraia zinazoshughulikia haki za binadamu na haki za wanawake kumsaidia kisaikolojia mwanamke anayedaiwa kubakwa na askari wa JWTZ mkoani humo, jeshi hilo limeonya kuwa tukio hilo ni la kupandikizwa.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, JWTZ imewataka wananchi wapuuze taarifa hizo zinazofanywa na watu wenye malengo ya kulichafua jeshi.
Wakati JWTZ ikitoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema askari wa jeshi hilo waliopo Mtwara wamekuwa wakifanya vitendo vya kihalifu ikiwemo kutesa, kubaka na kuwapiga watu.
Lipumba alisema kutekwa kwa Naibu Mkurugenzi wa CUF Taifa, Shaweji Mketo na viongozi wengine wa chama hicho Mkoa wa Mtwara, ni kinyume cha sheria na kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam jana, Lipumba alisema wanafanya mchakato wa kushughulikia uonevu huo wa JWTZ.
Profesa Lipumba alisema mbali ya Mketo, viongozi wengine waliotekwa na kuteswa ni Salum Hamis Mohamed (Mwenyekiti CUF Mtwara Mjini), Ismail Hamis Jamal (Mwenyekiti CUF Mtwara Vijijini), Ismail Bakari Njalu (Mwenyekiti wa Vijana -JUVICUF Mtwara Mjini), Said Issa Kulaga (Katibu CUF Mtwara Mjini) na Kashindye Kalungwana (Dereva wa CUF Ofisi Kuu)
Alisema katika hatua hizo, watahakikisha waliohusika na unyama dhidi ya mwanamke huyo wanafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Alieleza kuwa, viongozi hao baada ya kutekwa na askari wa JWTZ, walivuliwa nguo zote na kulazwa kifudifudi, kumwagiwa maji ya baridi na kupakwa chumvi kisha kuanza kupigwa usiku kucha kwa kutumia mikanda ya jeshi, ngumi, mateke, fimbo maalumu za ngozi za wanyama na miti maalumu.
Akielezea tukio hilo, Profesa Lipumba alisema viongozi hao wakiwa njiani kurejea Mtwara mjini wakitokea Msimbati, ghafla waliona magari mawili ya kijeshi ambayo baada ya kuona gari la CUF lenye namba T 886 BGW, waliziba barabara na askari wa JWTZ waliwashusha na kuanza kuwapiga na kisha kuwarusha kwenye karandinga la jeshi.
Alisema baadaye viongozi hao walipelekwa katika kambi ya jeshi ya Naliendele kabla ya kuachiwa majira ya saa 5:00 usiku kwa kukabidhiwa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ambaye hadi anakabidhiwa viongozi hao, alikataa kutoa ushirikiano kwa CUF.
Alisema Mketo alipozinduka Juni 28 alijikuta ana dripu na hakuelewa ni ya nini na baadaye wanajeshi waliitoa.
Profesa Lipumba alisema tukio la utesaji raia ndani ya kambi ya jeshi ukiliunganisha na matukio mengine kama ya uteasaji wa Dk. Stephen Ulimboka, kutekwa nyara kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda, kulipuliwa bomu katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kunadhihirisha hatua za awali za kusambaratika kwa dola.
Licha ya malalamiko hayo, taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Jeshi la Wananchi, ilieleza endapo taarifa hizo zitatangazwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari wananchi wazipuuze, kwani hazina ukweli wowote zaidi ya kuwa ni za upotoshaji.
Kauli ya jeshi ilisema: “Msichana huyo amepandikizwa ili kuharibu taswira nzuri ya JWTZ. Ifahamike kwamba maofisa na askari wa JWTZ waliopo Mtwara wanafanya kazi kwa uangalizi wa karibu, na vitendo hivyo vya aibu hawawezi kuvifanya. Jeshi letu linafanya kazi kwa nidhamu na si kama baadhi ya watu wenye maslahi binafsi wanavyolipaka matope.”
0 comments:
Post a Comment