Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini
(MOAT), wamesema kuwa bado wanaamini kwamba ni makosa kufunga mitambo ya
analojia katika kipindi cha mpito cha kutoka utangazaji wa analojia kwenda
dijitali, na kwamba ni jambo la busara kwa serikali kubadilisha mtazamo juu ya
suala hilo.
Kadhalika, wameeleza kuwa kwa
kutekeleza hayo itawaletea manufaa wananchi ambao wanaendelea kunyimwa haki yao
ya kupata habari katika kipindi cha mpito.
Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya
habari jana, Katibu Mtendaji wa MOAT, Henry Muhanika alisema ni jambo la busara
kwa serikali kubadilisha mtazamo wake juu ya suala hilo.
Alisema mpaka sasa kuna wananchi
ambao wanaendelea kunyimwa haki yao ya kupata habari katika kipindi cha mpito,
na kueleza kuwa kutofanya hivyo itakuwa ni ubabe kwa upande wa waziri na
serikali.
Uamuzi wa utoaji wa taarifa
huo, umefuatia baada ya kauli ya Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mbarawa kueleza bungeni kuwa serikali haiwezi kurudi kwenye
mfumo wa analojia.
Katika maelezo hayo, Profesa Mbawara
alisema kurudi katika mfumo wa analojia kutaongeza gharama hasa zile za
kuendesha mitambo ya analojia.
Profesa Mbawara alisema mfumo wa
dijitali unakwenda vizuri katika mikoa iliyofungwa hususan Dar es Salaam na
kusema kwamba hadi Aprili, mwaka huu, ving’amuzi 250,000 vilishauzwa kati ya
watu wenye runinga 600,000.
Kuhusu takwimu hizo, MOAT ilieleza
kuwa zaidi ya wananchi wapatao 350,000 sawa na asilimia 60 wa Jiji la Dar es
Salaam, wananyimwa haki yao ya msingi ya kupata habari.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Kasulu
Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alitoa hoja bungeni ya kuitaka serikali
iangalie uwezekano wa kutoizima mitambo ya utangazaji ya analojia katika
kipindi cha mpito cha kutoka utangazaji wa analojia kwenda dijitali unaoendelea
nchini.
0 comments:
Post a Comment