skip to main |
skip to sidebar
MAUAJI YA PADRI: DPP, POLISI WAKOROGANA
23,Jumaadal ula,1434Hijiriyah/ April 04,2013Miyladiyah

Mkurugenzi
wa Mashtaka (DPP) Zanzibar, Ibrahim Mzee Ibrahim, ametupilia mbali
uchunguzi wa mauaji ya Padri Evarist Mushi uliofanywa na Jeshi la Polisi
kwa kushirikiana na Maafisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI)
na kusema mtuhumiwa hana kesi ya kujibu mahakamani.
Uchunguzi umebaini kuwa DPP baada ya kulipitia jalada la uchunguzi wa
mauaji hayo, juzi alitoa mwongozo kwa Jeshi la Polisi kuendelea
kumtafuta muuaji wa Padri Mushi.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo,
DPP aliliandikia barua Jeshi la Polisi na kukabidhiwa juzi ikieleza
sababu za ofisi yake kutofungua hati ya mashtaka hadi sasa dhidi ya
mtuhumiwa wa mauaji hayo.
Jeshi la Polisi limethibitisha
kuipokea barua ya DPP ambayo inaeleza kuwa ushahidi uliokusanywa katika
jalada la kesi hiyo hauna mashiko na kwamba mtuhumiwa hahusiki na mauaji
hayo.
Chanzo cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilieleza kuwa
DPP hajaridhishwa na uchunguzi wote uliokusanywa dhidi ya mtuhumiwa
pamoja na watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya askari polisi,
Said Abdulrahman aliyeuawa kwa kupigwa mapanga na watu wanaosadikiwa
kuwa wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar
Oktoba 17, mwaka jana.
Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar,
Mussa Ali Mussa, alithibitisha hatua ya DPP kutupa uchunguzi wote wa
jalada la mauaji ya Padri Mushi na kuwataka waandishi wa habari
kumtafuta DPP azungumzie sababu za uamuzi wake wa kutokubaliana na
uchunguzi wa Polisi.
Hata hivyo, alisema kwamba Jeshi la
Polisi bado linaamini uchunguzi walioufanya kwa kushirikiana na FBI
hauna shaka na kwamba mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu mahakamani na
wataendelea kumshikilia.
Alisema kwamba kwa mujibu wa sheria,
Jeshi la Polisi jukumu lake ni kuchunguza kesi na ofisi ya DPP jukumu
lake ni kufungua hati ya mashtaka na kutetea kesi mahakamani.
Hata hivyo, NIPASHE ilipofika katika ofisi ya DPP, Katibu muhtasi wake
alisema amepokea maagizo kutoka kwa bosi wake kuwa waandishi wote wa
habari wanaofuatilia suala hilo, wamuone Kamishna wa Polisi kwa vile
kazi aliyopewa ya kupitia jalada la uchunguzi kabla ya kufungua kesi
ameikamilisha.
“Kamishna ndiye aliyeitisha mkutano na
waandishi wa habari kuelezea hatua iliyofikiwa pamoja na kukamatwa kwa
mtuhumiwa, sasa awaite tena amalizie kazi yake ya kuwaeleza hatua
iliyofikiwa baada ya Mkurugenzi kurejesha jalada la mauaji,” alisema
Katibu muhtasi huyo.
Katika hatua nyingine, Naibu Mkurugenzi
wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Yusuph Ilembo, jana alifika katika
Mahakama Kuu ya Zanzibar, kufuatia ombi lililofunguliwa mahakamani na
wakili anayemtetea mtuhumiwa wa mauaji, Abdallah Juma Mohamed.
Abdallah Juma amefungua ombi katika Mahakama Kuu kwa kutumia kifungu
cha sheria 390 cha sheria namba 7 ya mwenendo wa makosa ya jinai ya
mwaka 2004, akitaka Jeshi la Polisi litoe maelezo kwa nini mteja wake
hajafikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu alipokamatwa Machi 17,
mwaka huu.
Wakili Abdallah Juma akisaidiwa na mawakili Shaban
Juma Bakari na Shaibu Ibrahim Shaibu waliitaka Mahakama Kuu itoe amri ya
kuachiwa kwa mteja wao kutoka mikononi mwa Jeshi la Polisi. Hata hivyo,
Ilembo alisema kuwa kutokana na uzito wa kesi hiyo, anaomba kupewa muda
wa kutayarisha majibu ya hati ya kiapo kwa maandishi na kuuwasilisha
kwa upande wa utetezi na mbele ya mahakama hiyo kabla ya ombi hilo
kuanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi.
“Tunaomba mtuhumiwa aendelee kushikiliwa na Polisi, wakati tukifanya matayarisho ya kujibu hati ya kiapo,” alisema Ilembo.
Kwa upande wake Jaji wa Mahakama Kuu, Mkusa Isaack Sepetu, alisema
baada ya kusikiliza pande zote mbili, alimtaka Ilembo awe amejibu kwa
maandishi hati ya kiapo ya maombi hayo kabla ya kuanza kusikilizwa kwa
shauri hilo Aprili 8, mwaka huu.
Aidha, Jaji alisema wakati wa
kusikilizwa kwa shauri hilo, ametaka mtuhumiwa huyo afikishwe
mahakamani, baada ya hoja za upande wa mawakili wanaomtetea kutaka
dhamana kwa mteja wao, kwa vile bado hajafikishwa mahakamani kwa tuhuma
za mauaji.
Kutupwa kwa uchunguzi wa jalada la mauaji hayo
pamoja na jalada la uchunguzi wa mauaji ya Polisi kunadhihirisha kuwapo
kwa mvutano mkubwa baina ya Jeshi la Polisi Zanzibar na ofisi ya DPP.
CHANZO: NIPASHE, 4th April 2013
0 comments:
Post a Comment