RAIS Jakaya Kikwete juzi aliwaonya wanachama wa CCM akiwataka waache
kubweteka kwa kuwategemea askari polisi katika masuala ya kisiasa, kwani
kufanya hivyo watakuwa wanajidanganya.
Kikwete alitoa kauli hiyo
wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM uliofanyika kwa siku tatu
mfululizo katika Ukumbi wa Kizota mjini Dodoma.
Kikwete ambaye
pia ni Mwenyekiti wa CCM, alisema kitendo cha wanaCCM kuishi katika
siasa kwa kutegemea Jeshi la Polisi hakipaswi kukubaliwa kwani kimepitwa
na wakati.
“Mnaishia kulalamika tu kila siku, eti wanatukana
halafu mnaishia kusema ndiyo kawaida yao…au utasikia mtu anasema eti
Serikali haipo! Kazi ya Serikali siyo hiyo, hiyo ni kazi ya kisiasa
maana hao ndio wenzenu,”alisema Kikwete na kuongeza:
“Sasa
mnataka wakisema Serikali ya CCM haijafanya kitu polisi wawafuate, au
wakisema Kikwete nchi imemshinda, polisi wakawakamate? Kama wakisema
hatujafanya kitu ni kazi yenu kusema kwamba tumefanya kitu, waonyesheni
barabara, shule na mambo mengine.”
Licha ya kwamba hakuwataja
moja kwa moja, kauli za Rais Kikwete zilikuwa zikielekezwa kwa uogozi wa
Chadema ambao kimsingi kinaonekana kuwaumiza vichwa CCM.
Huku
akirudia mara kadhaa maneno hayo alisema, “Nataka mfahamu ndugu zangu
kuwa tukiishi kwa kutegemea Jeshi la Polisi kufanikisha mambo yetu,
tutakwisha na tutakwisha kweli.”
Kikwete aliwatuhumu viongozi wa
upinzani kwamba ni waongo na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakizusha
mambo ambayo hayapo, huku wakijifanya kuwa na ushahidi wa kimaandishi.
Alimtaja
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwamba kuna wakati aliwahi
kuzusha kwamba yeye (Kikwete), na makada kadhaa wa chama hicho wakiwamo
Rostam Aziz walikuwa jijini Mwanza usiku, wakati si kweli kwani siku
waliyodai alikuwa Nachingwea mkoani Lindi kwenye mikutano ya kampeni za
urais.
Katika mazingira hayo, aliwataka wanaCCM kila mahali
kujibu hoja za wapinzani kwa kauli na vitendo na wasikubali kuburutwa
kwani uongo ukiachwa kwa muda mrefu unageuka kuwa ni ukweli.
Aliwaeleza
kuwa ukimya wao katika kujibu hoja za wapinzani ni sumu kwao na kwamba
wenzao wameanza kuaminika zaidi yao licha ya kuwa CCM ndio wenye majibu
yote.
“Mkijibu kwa hoja wanatulia, sio Polisi. Nakumbuka Mwigulu
aliwajibu pale bungeni kuhusu bajeti yao mbadala. Walipoitoa kijana wetu
akasimama na kupiga msumari kweli wakachanganyikiwa sasa hizo ndio kazi
zinazotakiwa jamani,” alisisitiza Kikwete.
Mbali na hilo aliwaonya kuacha malumbano ya mara kwa mara akieleza kuwa hali hiyo inakibomoa chama.
Alisema baadhi ya wanaCCM wamekuwa wakitumia muda mwingi kukosoana wao kwa wao, huku wakitoa nafasi kwa adui zao.
Mwenyekiti
huyo alisema hakuna mtu kutoka nje ya chama anayeweza kukidhoofisha CCM
kwa hoja isipokuwa chama hicho kinaumizwa na wanachama wake ambao
wamekuwa wakilumbana bila sababu.
Akizungumzia suala la wagombea
urais aliwataka wanachama wenye nia kufuata taratibu zote za chama
pamoja na kuvumiliana ili ifikapo Mei 2015, mkutano utafanya uamuzi wa
nani anasimama kupeperusha bendera ya chama hicho.
“Kwa wale
mnaotaka kugombea, andikeni hiyo tarehe tutakuja hapa kuteua, lakini
msituvuruge lazima mfuate utaratibu. Utaratibu huo utatangazwa, maana
mkianza kupita huko na huko ndiko tunakopata matatizo,” alisema Kikwete.
Kikwete
juzi alichaguliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa CCM baada ya
kupata asilimia 99.92 ya kura zilizopigwa, huku kura mbili zikimkataa.
Kadhalika mkutano huo uliwachagua Dk Ali Mohamed Shein kuwa Makamu
Mwenyekiti (Tanzania – Zanzibar) na Phillip Mangula kuwa Makamu
Mwenyekiti (Tanzania Bara).
Sikiliza Live
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


0 comments:
Post a Comment