Fadhila Za Mwezi Wa Muharram, Siku Ya 'Aashuraa Na
Bid'ah Zake
AlhamduliLLaah,
Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha tena katika mwaka
mwengine mpya wa Kiislamu. Katika mwezi wa Muharram, kuna fadhila zake
maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi mja
anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho ili aweze kujichumia thawabu
nyingi. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana kama Taasu'aa na
'Aashuraa. Hivyo ndugu Waislamu tusiache kufunga siku hizi mbili kwani
thawabu zake ni kama ilivyotajwa katika mapokezi yafuatayo:
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم
عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي
قبله)) رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga
ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya
mwaka uliotangulia)) [Muslim]
(soma
maelezo chini kujua kwanini tufunge pia na tarehe 9 Muharram)
Jumla ya miezi mitukufu ni minne na mwezi huu wa Muharram ndio
mwezi wa kwanza unaoanza kuhesabika kama ni mwaka mpya.
((إِنَّ
عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَق السَّمَاوَات وَالأَرْضَ
مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ
تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ))
((Idadi
ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Allaah ni miezi kumi na mbili katika ilimu
ya Allaah (Mwenyewe tangu) siku Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo
minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajab, Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na
Muharram) (kufanya) hivi ndiyo dini iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu
(kwa kufanya maasi) katika (miezi) hiyo)) [At-Tawbah
9:36]
Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth
iliyotoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu):
(السنة اثنا عشر شهرا، منها أربعة حرم: ثلاث
متواليات، ذو القعدة، وذو الحجة، والمحرم، ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان)) رواه البخاري، ومسلم
((Mwaka
una miezi kumi na mbili, minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana
pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab ambao uko baina ya
(mwezi wa) Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Ni neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Kutujuaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au masiku bora au
masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu za mema yanayotendeka humo huwa ni
zaidi ya nyakati nyingine.
Kuhesabika
Kwa Mwaka Mpya Wa Hijriyah
Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya kuhama (Hijrah)
kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba kutoka
Makkah kuhamia Madiynah. Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu
'anhu) akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji
ambao wataanza kutumia Sharia'h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu
miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana kama
Muharram. Na pia inasemekana kuwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipata
barua kutoka kwa mabalozi wake wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislam,
na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe. Akawashauri Maswahaba
wenzake kuwa kuwe na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata
miaka ya kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe
wakakubaliana ianze pale alipohamia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) Madiynah.
Na
mwaka huu wa Kiislam
ambao unafupishwa
kama A.H au H kwa kirefu yenye maana 'After Hijrah' au
Hijriyah, tarehe 1 Muharram A.H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622M. Na
ndivyo hivi inavyohesabika mpaka mwezi wa Dhul-Hijjah unapomalizika na mwezi wa
Muharram utakapoingia hivi karibuni
Fadhila
Za Mwezi Huu Khaswa
Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika Aayah ya juu ni mitukufu
lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine kama ilivyo
katika Hadiyth zifuatazo:
عَنْ
أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى
اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ((أَفْضَلُ
الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم
Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada
ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]
عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ
عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا
هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ
يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان "
رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye
amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa
sallam) akisubiri kufunga siku yoyote kama siku hii ya siku ya 'Aashuraa na
mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhaan" [Al-Bukhaariy]
Swawm ya 'Ashuraa imependezeshwa hata kwa watoto kuifunga kama walivyokuwa wakifanya
Maswahaba katika siku hiyo.
عن الرُّبيّع بنت معوذ رضي الله عنها قالت:
"أرسل رسول الله صلى الله عليه وسلم غداة عاشوراء إلى قرى الأنصار "من أصبح مفطرا فليتم بقية يومه ومن أصبح صائما
فليصم" ، قالت : فكنا نصومه بعد ونصوّمه صبياننا ... رواه البخاري ومسلم
Kutoka kwa Ar-Rubay'i bint Mu'awwadh (Radhiya
Allaahu 'anhaa) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituma
ujumbe Alfajiri ya siku ya 'Ashuraa katika vijiji vya Answaar "Aliyeamka akiwa amefuturu
amalize siku yake (kwa kutokula) na aliyeamka amefunga afunge" Akasema
(Ar-Rubay'i: 'Tulikuwa tukifunga baada yake na tukiwafungisha watoto wetu...' [Al-Bukhaariy na Muslim]
Sababu Ya
Kufunga Siku Ya 'Aashuraa
عَنْ
ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ
تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا
هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ
عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ))
فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ"
رواه البخاري
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema
"Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah
akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Aashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani
kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa
Wana wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema
(Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu
ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy]
Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)
ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa
kuongeza siku moja kabla.
روى عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قال : "حِينَ صَامَ رَسُولُ اللَّهِ
صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَأَمَرَ
بِصِيَامِهِ قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ يَوْمٌ تُعَظِّمُهُ
الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ
وَسَلَّمَ: ((فَإِذَا كَانَ الْعَامُ الْمُقْبِلُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ صُمْنَا
الْيَوْمَ التَّاسِعَ)) قَالَ فَلَمْ يَأْتِ الْعَامُ
الْمُقْبِلُ حَتَّى تُوُفِّيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ
وَسَلَّمَ ". رواه مسلم
Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema
"Alipofunga Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya
'Aashuraa na akaamrisha ifungwe wakasema: Ewe Mtume wa Allaah, hii ni siku wanayoitukuza
Mayahudi na Manaswara. Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam): ((Ikifika mwakani In shaa Allaah tutafunga siku ya tisa
pia)). Akasema (Ibn 'Abbaas) haukufika mwaka uliofuata ila alifariki Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Muslim]
Kwa hiyo ni bora kufunga siku ya tisa na kumi Muharram, na
kama mtu hakujaaliwa kufunga siku ya tisa na kumi, basi afunge siku ya kumi na
kumi na moja. Na kama mtu hakujaaliwa kufunga hivyo basi afunge siku ya kumi
peke yake ili asikose kupata fadhila ya siku hiyo.
Kwa vile siku hii ni siku Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
Aliyomnusuru Muusa ('Alayhis-Salaam) na Wana wa Israaiyli, na sisi pia tutakaofunga tuwe na tegemeo kuwa nasi Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) Atatunusuru pia kutokana maadui wetu na mabaya kama
Alivyotuahidi In shaa Allaah
((إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا
فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ))
((Bila ya
shaka Sisi Tunawanasuru Mitume Yetu na wale walioamini katika maisha ya dunia
ya siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe)) [Ghaafir 40: 51]
Juu ya kwamba fadhila ya kufunga Swawm ni ibada Aipendayo
kabisa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama ilivyo katika Hadiyth mbali
mbali, vilevile funga hii itatusafisha na madhambi ya mwaka
mzima,
قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم
عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم
Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga
ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya
mwaka wa nyuma)) [Muslim]
Ndugu Waislam, hii ni fursa kubwa ya kujisafisha na dhambi na
kuzidisha taqwa (ucha Mungu) ili kujibebea zawadi nyingi twende nazo
Akhera kwa vile hatujui amali njema zipi zitakazokubaliwa na Allaah
(Subhaanahu wa Ta'ala) na hatujijui kama tutakuwa na umri wa kuchuma
zaidi.
Bid'ah
Katika Siku Ya 'Aashuraa
Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa,
tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni
nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu,
kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha
mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu). Matendo hayo ni mambo ambayo
hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani
anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam).
Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah
Amrehemu):
"Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu
wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya
Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa
aalihi wa sallam) aliharamisha kama ilivyo katika Hadiyth hii sahihi:
عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي
صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية)) البخاري .
Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu
atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy]
Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani
Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku
hiyo."
Ibn
Rajab amesema:
"Wanayoyafanya Ma-Rafidhah (Mashia) katika siku hii kuwa ni
siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali
ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema,
wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya
siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya
huzuni kwa wasio Mitume?"
Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale
ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema. Aamiyn.

0 comments:
Post a Comment