Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 18 October 2012

Kutusi matukufu ya Kiislamu, ujahili wa kisasa


Hamjambo wapenzi wasomaji wa Blog hii na karibuni kujiunga nami katika makala hii ya wiki ambapo leo tutachungua kitendo cha kijahili cha kutengeneza filamu inayomvunjia heshima Mtume SAW. Karibuni kujiunga nami hadi mwisho.
Baada ya kusambaratika Shrikisho la Sovieti, nchi za Magharibi ziliutaja Uislamu kuwa tishio kubwa zaidi kwao.
Kwa msingi huo nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kukabiliana na wimbi la kuenea Uislamu zimeanzisha mradi wa chuki dhidi ya Uislamu ambao ulishika kasi baada ya matukio ya Septemba 11 mwaka 2001.
Katika upande mwingine Ulimwengu wa Kiislamu unashuhudia Mwamko wa Kiislamu jambo linaloashiria mwanzo wa mabadiliko makubwa duniani.
Historia ya mwanaadamu imejaa milima na mabonde na hivi sasa katika kurasa zake tunashuhudia kuanguka tawala za kidikteta katika nchi za Kiarabu na hivyo kutoa bishara njema na mafanikio makubwa kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Uislamu unazidi kuenea kwa kasi kote duniani jambo ambalo limezidisha hasira na ghadhabu za maadui. Katika kujaribu kuzuia wimbi la kunawiri na kuenea Uislamu, maadui wanachukua hatua za kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu. Mfano wa hivi karibuni kabisa wa njama hizi zilizojaa taasubi ni kutengenezwa filamu inayomvunjia heshima Mtume wa Rehma na Amani, Mohammad al Mustafa SAW.
Filamu hii imesambazwa kwenye intaneti na Terry Jones mhubiri Mkristo mwenye chuki dhidi ya Uislamu. Katika filamu hii ya masaa mawili, shakhsia yenye thamani ya Mtume Mtukufu SAW imevunjiwa heshima.
Sam Bacile mwandishi na mtengeneza filamu hii iliyopachikwa jina la ‘’Innocence of Muslims’ ni Yahudi Mmarekani mkaazi wa California ambaye anafanya biashara ya uuzaji na ununuzi wa nyumba.
Sam Bacile ameliambia gazeti la Wall Street Journal kuwa: “Zaidi ya Mayahudi 100 walitoa msaada wa dola milioni tano kuchangia utengenezaji wa filamu hii.”
Utengenezaji filamu hiyo chafu ulijumuisha wacheza filamu 60 na watu 45 nyuma ya pazia katika muda wa miezi mitatu.
Filamu hii imeonyeshwa mara moja tu katika ukumbi usio na watu wengi huko Hollywood na pia katika kumbukumbu ya matukio ya Septemba 11 ilikuwa ionyeshwe katika kanisa la mhubiri Mkristo mwenye chuki dhidi ya Uislamu Terry Jones. Hata hivyo mpango wa kuionyesha filamu hiyo hapo ulibatilishwa. Lakini pamoja na hayo filamu hii inayomvunjia heshima Mtume SAW ilisambazwa katika mtandao wa intaneti. Kutokana na kuwa watu wa kwanza kueneza filamu hii katika intaneti walikuwa ni Wakristo wa dhehebu la Kopti kutoka Misri, maandamano ya kwanza ya kuipinga filamu hii chafu yalianzia Misri. Baada ya hapo maandamano hayo yalienea Libya, Yemen na hatimaye katika nchi zingine duniani.
Serikali ya Marekani sasa inajaribu kujinusuru kufuatia kuongozeka hasira za Waislamu wanaolalamikia utengenezwaji filamu hii chafu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton amesema hivi kuhusu filamu hii iliyo dhidi ya Uislamu: "Marekani kamwe haitawanyima raia wake haki ya kubainisha maoni yao." Kwa maneno mengine ni kuwa serikali ya Marekani imeunga mkono utengenezwaji na usambazwaji wa filamu hii inayoyavunjia heshima matukufu ya Waislamu zaidi ya bilioni moja na nusu duniani.  Hakuna shaka kuwa utengenezaji wa filamu kama hii na vitendo vingine vya chuki dhidi ya Uislamu vinafanyika kwa ridhaa kamili ya watawala wa Ikulu ya White House.
Historia inatuoneysha chanzo cha ujahili wa mushrikina katika zama za Mtume wa Uislamu SAW kilikuwa ni hofu kuhusu Uislamu. Kwa hivyo kutokana na hofu yao majahili walitekeleza vitendo vya kijinga ili kwa dhana yao potofu waweze kuzuia kuenea duniani dini ya Mwenyezi Mungu. Hivi sasa pia katika zama zetu hizi kimeanza kipindi kingine cha ujahiliya ambapo maadui wa Uislamu kwa kutoa nara potofu kama vile 'uhuru', 'haki za binaadamu' n.k wanatusi na kuuvunjia heshima Uislamu na Mtume wake Mtukufu.
Leo nara ya 'uhuru wa maoni' ambayo ni kati ya nara za Uislamu ni jambo linatotumiwa vibaya na Wamagharibi kuvunjia heshima Uislamu.
Sasa swali ambalo tunapaswa kuuliza ni hili, Je, uhuru wa maoni ni uhuru wa kutusi na kuvunjia heshima matukufu?
Swali lingine linaloibuka ni hili kuwa, je uhuru wa maoni hauna mipaka?, Je, kwa kisingizio cha uhuru wa maoni inawezekana kutusi na kuvunjia heshima matukufu ya kidini? Iwapo jibu ya mwaswali haya ni ndio, basi ni kwa nini serikali za nchi za Magharibi zinawaadhibu na kuwafunga jela wasomi ambao wanajadili na kutilia shaka madai ya Wazayuni kuhusu kuuawa kwa umati Mayahudi katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia katika tukio lililiopachikwa anwani ya Holocaust?
Uhuru wa kiitikadi unamaanisha kuwa kila mtu aweze kuchagua fikra aipendayo ya kisiasa, kidini na kijamii bila mashinikizo. Uhuru wa maoni pia ni sehemu ya uhuru wa kiitikadi kwa maana ya kubainisha itikadi kwa uhuru. Haki hii ni kati ya haki zilizo katika hati mbali mbali za haki za binaadamu. Katika mada ya 19 ya Azimio la Dunia la Haki za Binadamu imeandikwa hivi: "Kila mtu ana haki ya itikadi na maoni na haki hiyo inajumuisha uhuru wa kuwa na maoni pasina kuingiliwa na uhuru wa kutafuta na kupokea maelezo na fikra kupitia njia yoyote." Aidha azimio hilo linaongeza kuwa ‘mtu hapaswi kubughudhiwa kwa sababu ya akida yake.’
Vile vile katika mada ya 19 ya Mapatano ya Kimataifa ya Haki za Kiraia na Kisiasa imeandikwa kuwa: ‘Haki ya uhuru wa maoni inaandamana na wajibu na majukumu maalumu, awali ni kuheshimu hadhi na haki za wengine na pili ni kuhifadhi usalama wa taifa au nidhamu ya ummah au afya ya jamii na maadili.'
Aidha katika mada ya 13 ya Mkataba wa Amerika wa Haki za Binaadamu uliopitishwa mwaka 1969 suala la uhuru wa fikra na maoni si mutlaki kwani kuna vizingiti kama kutashuhudiwa hujuma dhidi ya nidhamu, maadili ya umma na heshima ya watu.
Kwa hivyo tunaona kuwa sheria za kimataifa mbali na kukubali uhuru wa maoni kama haki ya kimsingi ya wanaadamu lakini pia haki hiyo ina mipaka yake.
Tukizingatia hilo tunafikia natija kuwa haiwezekani kutumia kisingizio cha kuwepo uhuru wa maoni katika kuhalalisha kutusi matukufu ya dini ya mbinguni. Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya dini ya Kiislamu vinaweza kutajwa kuwa ni ‘Uhuru wa Kutusi.’
Katika upande mwingine, kushiriki Wazayuni katika utengenezaji wa filamu kwa uwekezaji wa dola milioni tano ni ishara ya chuki ya kina walionayo dhidi ya Waislamu. Kitendo hicho cha wendawazimu na chuki ni ishara ya namna walivyokasirishwa na kuimarika na kuenea Uislamu duniani.
Leo Wamagharibi wamelemewa na kukata tamaa katika mapambano ya kimantiki dhidi ya Uislamu na ndio sababu wakaishia kutengeneza filamu zilizojaa matusi. Uislamu ni dini ya mantiki na fikra na inawaita watu wote waje katika meza ya mdahalo na mazungumzo ya kutegemea dalili za kiakili. Lakini Wamagharibi hawajatoa jibu la kimantiki kwa wito huu bali kinyume chake wanatoa matusi. Kumvunjia heshima Mtume SAW na kuhujumu itikadi za Waislamu ni jambo linaloashiria kuporomoka hatua kwa hatua ustaarabu wa Magharibi na utawala katili wa Israel.
Lakini kile ambacho watawala wa Marekani na Israel wanasahau ni kuwa vitendo vyao vya kuyavunjia heshima mtukufu ya Kiislamu vimekuwa na natija kinyume na walivyotarajia. Vitendo hivyo vichafu sasa vimeimarisha zaidi umoja na mshikamano wa Waislamu. Tunashuhudia umoja wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni katika kuitetea Qur’ani Tukufu na Mtume Muhammad SAW. Aidha idadi ya watu wanaovutiwa na dini ya Kiislamu na kusilimu inazidi kuongezeka kote duniani hasa huko Marekani kwenyewe. Katika upande wa pili, walimwengu wakiwemo Waislamu na wasio kuwa Waislamu wanazidi kuyachukia madola ya Magharibi hasa Marekani na Israel. Walimwengu na hasa Waislamu wanataka jamii ya kimataifa ichukue hatua za kuzuia vitendo vya kuvunjiwa heshima matukufu ya kidini. Hakuna shaka kuwa wanaadmau wote huru na wasomi kutoka kila dini na itikadi wanapinga kuvunjiwa heshima matukufu ya Kiislamu. Wapenzi wasikilizaji haiwezekani kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu wala kuangamiza fitra ya mwanaadamu. Kama alivyosema Ayatullah Sayyed Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu: “Uislamu umetufunza kuwa, wanaadamu, pamoja na kuwa na tafuati za rangi, lugha na utamaduni wote wana chimbuko moja la fitra ambayo inawavutia kuelekea katika utakasifu, uadilifu, amali njema na mshikamano; kwa hivyo iwapo wanaadamu wataweza kusalimika na upotofu, basi watafika katika tauhidi na maarifa ya dhati ya Mwenyezi Mungu."

0 comments:

Post a Comment