Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 4 July 2013

Muhongo: Tusipofikia malengo tufukuzeni kazi




Serikali iko katika hatua za mwisho za kulifumua na kuliunda upya Shirika la Umeme nchini (Tanesco) na lile la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kwa lengo la kuhakikisha kwamba Watanzania wapatao milioni tano (asilimia 30), wanafikiwa na umeme ifikapo mwaka 2015, toka asilimia 21 ya hivi sasa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akitoa ahadi na ombi kwa wananchi la kumchukulia hatua yeye na watendaji walio chini ya wizara yake, endapo watashindwa kulifikia lengo hilo.

Mradi huo ujulikanao kama ‘Matokeo Makubwa Sasa’ ulizinduliwa jana na kumshuhudia Profesa Muhongo na katibu mkuu wake Eliakim Maswi pamoja na wakuu wa mashirika ya Tanesco, TPDC na Wakala wa Umeme Vijijini, wakitoa ahadi mbele ya wananchi waliohudhuria kongamano hilo la kuitekeleza miradi iliyoainishwa na wizara ya kulifikia lengo hilo.

Waziri Muhongo alisema wanayafumua mashirika hao ili yaweze kuchangia lengo la kuwa na nishati ya uhakika nchini.

“Tunalenga kuondoa matatizo yaliyopo pale Tanesco ili iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Tayari tumeshapokea mapendekezo ya bodi ya wakurugenzi wa shirika tokea Mei 30 na sasa tunaandaa mapendekezo ya kwetu kama wizara na kisha tutatafuta na maoni ya mtaalamu mshauri, kwa lengo la kupata muundo mzuri unaolifaa shirika,” alisema.

Kwa upande wa TPDC, Profesa Muhongo alisema wanalisuka upya shirika hilo, ili lifanye shughuli za utafiti na uvunaji wa gesi na mafuta.

Ili kuhakikisha lengo la kuwafikishia umeme wananchi kwa asilimia 30 mwaka 2015, Waziri Muhongo alisema wametoa kipaumbele kwenye malengo makuu matatu, yakiwamo yale ya kupata umeme zaidi kutokana na mitambo iliyopo na kuondoa mitambo ya dharura.

Malengo mengine ni pamoja na kutekeleza miradi ya ufuaji, usafirishaji na usambazaji umeme na kuifanya sekta ya nishati kujiendesha kwa faida na kuandaa mwelekeo wa sekta ndogondogo ya umeme.

Wakati huo huo, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa, Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), imesema mageuzi ndiyo nyenzo ya kufanikisha mpango wa nishati Afrika uliotangazwa na Rais wa Marekani, Barack Obama; na kwamba inakusudia kutenga dola za Marekani bilioni tatu kwa ajili ya kuleta mageuzi ya sekta ya nishati.

Taarifa ya benki hiyo iliyotolewa Dar es Salaam jana ilieleza kwamba AfDB itaongeza fedha kwa ajili ya uzalishaji wa nishati, usambazaji na miundombinu, pamoja na maboresho ya sera na kanuni mbalimbali za serikali.

“Tunatarajia kutenga kama dola bilioni tatu katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Hii itaongeza uwekezaji mara nne zaidi katika sekta ya nishati.

Mkakati wetu unalenga mikopo ya uwekezaji, mageuzi, ushauri na dhamana," alisema Rais wa AfDB, Donald Kaberuka.

Nchi za kipaumbele katika mpango wa Obama unaojulikana kama 'Power Afrca' ni Tanzania, Kenya, Ethiopia, Ghana, Liberia na Nigeria.

Alisema fedha hizo za uwekezaji kwenye sekta ya nishati zinalenga kutafsiri maisha ya watu wa kawaida kwa kuhakikisha upatikanaji wa umeme ili kukuza biashara ndogondogo na mageuzi ya sera ili kuwezesha na kuimarisha masoko ya nishati ya kuvuka mpaka.

Mapema wiki hii, akizungumza na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali, Rais Obama alisema Afrika inaelekea kwenye mafanikio makubwa na kwamba kupitia mpango wa Power Africa, anataka Marekani iwe sehemu ya mafanikio hayo.

0 comments:

Post a Comment