. Serikali imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi
mwa polisi ikieleza kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia
nguvu za kadiri hata kiasi cha kusababisha madhara au kifo.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia
kwa kuwapiga watu wote wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.
Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa
Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha 18(B) na
18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa kutumia
nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au kifo
katika mazingira ya kisheria.
Aliyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa
uhai wa mtu mwingine, kuzuia madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au
kwa mtu mwingine na kumzuia mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au
kunajisi mtoto au kufanya vitendo kinyume na maumbile.
Pia kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au
unyang’anyi wa kutumia silaha au kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo
chochote kinachohatarisha uhai wa mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu cha 18 na 18(A) cha Sheria
ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002, kinampa haki mtu
yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda mtu mwingine, kulinda mali
yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya Serikali na taasisi zake, ambayo
iko chini ya uangalizi wake kisheria.
Kauli hiyo ya Serikali kuhusu mauaji ya raia
mikononi mwa polisi, ilitolewa ikiwa ni ufafanuzi wa jibu la swali la
nyongeza lililoulizwa bungeni Mei 28,2013 na Rashir Ally Abdalah
(Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji yanayofanywa na askari polisi
ni mauaji ya kisheria. Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad
Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo,
na jana Silima kutoa kauli ya Serikali kujibu mwongozo huo.
“Ikumbukwe pia kuwa, kifungu cha 29 cha Sheria ya
Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura322, pamoja na Kanuni za Kudumu
za Utendaji za Jeshi la Polisi Na274, vinampa haki ya kisheria askari
polisi kubeba na kutumia silaha za moto ikiwamo bunduki na mabomu katika
utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku..,”alisema Silima.
Alifafanua kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni
na taratibu mbalimbali ikiwamo alizozitaja, mahakama katika nyakati
tofauti imetoa msimamo wa kisheria juu ya suala hilo.
Akitoa mfano alisema: “Mathalan katika kesi ya
Seif Mohamed Senzagala dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1994 kama
ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report ukurasa wa 122, ambapo mshitakiwa
(mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga mlalamikaji ambaye alimfuata
nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”
Alisema katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja
na kuridhia uamuzi wa mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia
nguvu kupita kiasi, ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani
alitenda kosa lile wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa
mlalamikaji.
0 comments:
Post a Comment