Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 25 June 2013

Muafaka wazidi kutikiswa

  MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, amesema siasa za chuki na uhasama zimeanza kurudi tena Zanzibar na kutishia Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kuwa katika hatari ya kumeguka.
Tamko hilo amelitoa wakati akifunga mjadala wa bajeti ya ofisi yake katika kikao cha Baraza la Wawakilishi (BLW) kinachofanyika huko Chukwani, nje kidogo ya Manispaa ya mji wa Zanzibar jana.
Alisema kuwa malengo makubwa ya kuazishwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa kuondoa siasa za chuki, uhasama na kujenga misingi ya amani na mshikamano kwa wananchi wa Zanzibar.
Balozi Seif alisema dalili za Serikali ya Umoja wa Kitaifa kumeguka zimeanza kujitokeza kutokana na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kutumia vibaya majukwaa ya kisiasa na kuwashambulia kwa matusi ya viongozi.
Alisema kama viongozi wataendelea kutumia vibaya majukwaa ya kisiasa kueneza chuki, matusi na kashifa dhidi ya viongozi wengine wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itameguka na Zanzibar kuingia katika mpasuko mkubwa wa kisiasa.
Alisema kuwa viongozi wanaounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa lazima wajiepushe na kauli za matusi na uchochezi ambazo wamekuwa wakitoa bila ya kuzingatia madhara yake na kuwa chanzo cha kubomoa Umoja wa Kitaifa Zanzibar.
Alisema kwamba wakati viongozi wa kitaifa wamekuwa wakifanya kazi kwa mashirikiano makubwa tofauti na viongozi wa CUF wanapokuwa katika majukwa ya kisiasa wamekuwa wakitumia muda mwingi kueneza chuki na kutukana viongozi wezao.
Alisema kwamba viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitoa kauli za chuki ikiwemo kumtukana yeye binafsi, kupachika majina ya kejeli na kusababisha hali ya wasiwasi kuanza kujitokeza kuhusu mustakabali wa mwelekeo wa Serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar.
“Mheshimiwa Spika, mahusiano ya viongozi wakuu wa serikali ni mazuri lakini majukwaa ya kisiasa yanatumiwa vibaya kutukana viongozi wengine .....tukiendelea kama hivyo tutarudi kule kule Zanzibar,” alisema Balozi Seif.

0 comments:

Post a Comment