بسم الله الرحمن الرحيم
BismiLLaah
 walhamduliLLaah Rabbil 'Aalamiyn. Was-Swalaatu was-Salaamu 
‘alaa Nabbiyihi asw-Swaadiq Al-Amiyn, wa ‘alaa aalihi wa Swahaabatihi 
al-Ghurr Al-Mayaamiyn, wa man Tabi'ahum bi Ihsaani ilaa Yawmid Diyn. 
Amma ba’ad:
ASILI YA APRIL FOOL
Asili ya April Fool haikujulikana kwa uhakika na kuna rai mbali mbali zinazohusiana nayo.
Wengine wamesema imeanza kutokana na sherehe za majira ya kuchipua (Spring) katika ikwinoksi (siku ya mlingano) tarehe 21 Machi.
Wengine
 wamesema kuwa huu ni uzushi uliochomoza France mwaka 1564 M, baada 
ya utangulizi wa kalenda mpya. Wakati mtu alipogoma kukubali kalenda 
mpya akaishia kuwa ni mwathirika wa baadhi ya watu ambao wamemsababisha 
aathirike kufedheheka na wakamfanyia istihzai na kumtania, akawa ni 
kichekesho kwa watu. 
Wengine
 wanasema kuwa uzushi huu umeanza asili yake katika nyakati za kale na 
sherehe za mapagani zilikuwa na uhusiano na siku hasa mwanzo wa majira 
ya kuchipua. Kwa hiyo hii ni kasumba ya ibada za mapagani. Inasemekana 
kuwa nchi nyingine, kuwinda hakukufaulu siku za mwanzo za uwindaji. 
Le poisson d'avril (Samaki wa Aprili)
Wazungu
 wameiita April Fool kwa jina la 'le poisson d'avril' (Samaki wa 
Aprili). Na sababu hii ni kutokana na jua linavyosogea kutoka nyumba ya 
zodiaki (nyota za unajimu) ya Pisces (Nyota ya samaki) ikielekea nyumba 
nyingine. Au kwa sababu ya neno la poisson ambalo maana yake ni samaki, 
hivyo ni ugeuzaji wa neno la 'passion' ambayo ina maana ya 'kuteseka'. 
Kwa hiyo ni alama ya kuteseka aliyovumulia Nabii 'Iysa (Alayhis Salaam) 
kama walivyodai Wakristo. Na madai yao haya yalitokea wiki ya kwanza 
katika mwezi wa April.
Baadhi
 ya makafiri wameiita siku hii 'Siku nzima ya wajinga' kama 
inavyojulikana Kingereza. Hii ni kwa sababu uongo wanaousema ili wale 
wanaousikia waamini kwa hiyo wanakuwa ni waathirika wa wale 
wanaowafanyia dhihaka. 
Utajo
 wa mwanzo kabisa kwa Lugha ya Kingereza ilikuwa ni katika gazeti la 
Dreck. Siku ya pili ya Aprili 1698 M, gazeti hili lilitaja kwamba idadi 
kadha ya watu walialikwa kuhudhuria uoshaji wa watu weusi katika mnara 
wa London asubuhi ya siku ya mwanzo ya Aprili.
Tukio
 maarufu kabisa lililotokea Ulaya tarehe 1 Aprili lilikuwa wakati gazeti
 la Kingereza 'Evening star' lilipotangaza mwezi wa Machi 1746 M kwamba 
siku ya pili tarehe 1 Aprili, kutakuwa na gwaride la punda mji wa 
Islington Uingereza. Watu wakakimbilia kuwatazama wanyama hao na 
kulikuwa na zahma kubwa. Wakaendelea kusubiri na walipochoka kusubiri, 
waliuliza kutaka kujua hili gwaride litakuweko baada ya muda gani. 
Hawakupata jibu, hivyo wakatambua kuwa wamekuja kufanya maonyesho yao 
wenyewe kama kwamba wao ndio mapunda. 
Mmoja
 wao ameandika kuhusu asili ya uzushi huu kwa kusema: Wengi wetu 
tunasherehekea siku inayojulikana kuwa ni April Fool, au ikiwa 
itafasiriwa kihalisi 'Siku ya Ujanja'. Lakini je, tunajua siri chungu 
inayohusikana na siku hii?
Habari nyingine ambazo usahihi wake umetiliwa shaka na wanahistoria ni kuwa:
Waislamu
 walipotawala Hispania (Spain) takriban miaka elfu iliyopita, kulikuwa 
na nguvu kubwa ya utawala wa Kiislam ambayo haikuwezekana kuivunja. 
Wakristo wa Kimagharibi walitamani kuufuta Uislamu katika mgongo wa 
ardhi na walifaulu kwa kiwango fulani. 
Walijaribu
 kuzuia Uislamu kusambaa Hispania na walitaka kuuzima na wautoweshe 
kabisa lakini hawakufaulu, ingawa walijaribu mara nyingi bila ya 
kufaulu. 
Baada
 ya hapo, makafiri walituma majasusi Hispania kufanya utafiti ili kujua 
siri ya nguvu za Waislamu ambayo haikuwezekana kuishinda. Wakatambua 
kuwa kushikamana na Taqwa (Ucha Mungu) ndio sababu.
Wakristo
 walipotambua siri ya nguvu za Waislamu, wakaanza kufikiria mikakati za 
kuvunja nguvu hiyo. Na kwa ajili hii wakaanza kupeleka ulevi na sigara 
bure huko Hispania. 
Mbinu
 hizi kwa upande wa Magharibi zilifaulu kuleta taathira na imani za 
Waislamu zikaanza kulegea, hasa miongoni mwa vizazi vipya Hispania. 
Matokeo yake ni kwamba Wakristo Wakatholiki waliikandamiza Hispania 
nzima na wakauangamiza utawala wa Kiislamu katika ardhi hiyo, 
utawala ambao ulidumu zaidi ya miaka mia. Ngome ya mwisho ya Waislamu 
Grenada ilianguka tarehe 1 Aprili, hivyo wakaichukulia kuwa ni 'Siku ya 
Ujanja ya Aprili' au 'Siku ya Wajinga ya April'.  Ujanja kwa wale 
walioufanya, na Ujinga kwa wale waliofanyiwa na kutumbikia ndani yake.
Tokea
 mwaka huo hadi sasa, wanasherehekea siku hii na wanachukulia kuwa 
Waislamu ndio wajinga. Hawakuuhusisha ujinga huu na jeshi la Granada 
pekee kuwa ni wajinga, bali wamekusudia kuwa ni Umma wa Kiislamu mzima 
kuwa ni wajinga.
Hata
 hivyo, habari hizi tumezinukuu hapa kwa kuwa zimeenea sana miongoni wa 
Waislam, lakini kama tulivyotangulia kueleza, ni kuwa, uhakika na ukweli
 wake una mashaka kwa sababu kuna wanaosema kuwa wakati huo sigara na 
uvutaji tumbaku ulikuwa haujaanza hadi baada ya kushindwa Waislamu huko 
Hispania. Wahahistoria wanasema sababu za kushindwa Waislamu zilikuwa ni
 wenyewe kujiingiza zaidi kwenye mapenzi ya kidunia na starehe, pamoja 
na kuacha mafundisho sahihi ya Uislam na badala yake kuchanganya zaidi 
na falsafa ya Kigiriki na kutegemea zaidi fikra za kirumi katika 
kuendesha mambo yao badala ya mwongozo imara wa Kiislam. Kadhalika kuna 
Waislamu waliokuwa wakishirikiana na makafiri katika kupambana na 
makundi mengine ya Kiislam waliyokuwa hawaelewani nayo kama tunavyoona 
leo hii.
 BAADHI YA UDANGANYIFU WANAODANGANYANA WATU KATIKA
SIKU HII YA APRIL FOOL
Wengine
 wanapewa habari ya mmoja wa kipenzi chake katika familia kama mtoto, 
mke au mume kwamba amefariki na kwa wengine taarifa hizo husababisha 
hata kifo chao kutokana na kutokustahamili kupata mshtuko huo. Wengine 
wanapewa habari ya kufukuzwa kazi, au kuwashtua kwa habari mbaya kama 
kuunguliwa moto nyumba yake, au familia yake kupata ajali, na 
husababisha aathirike mtu kwa mshtuko huo hadi apate maradhi ya moyo, au
 maradhi ya kupooza au hata kifo cha ghafla.  
Wengine wadanganywe kuwa wake zao wameonana na wanaume wengine, jambo ambalo husababisha mauaji au talaka ya wake.  
Kuna
 visa visivyokuwa na mwisho na matukio yanayotokea kutokana na uongo 
huu. Uongo ambao umeharamishwa katika Uislamu na ambao haukubaliwi 
katika tabia za kiungwana.
HUKUMU YA UONGO KATIKA UISLAMU
Uongo
 ni tabia ovu kabisa ambao dini zote na mfumo wa elimu za maadili 
zimeonya dhidi yake, na pia asili ya kimaumbile ya binaadamu (fitrah) 
inakubaliana kuwa ni uovu.
Ukweli
 ni moja wa nguzo ambayo maadili ya maisha ya kiduniya yanategemea ili 
yahifadhike. Ni asasi ya tabia za kustahili kusifiwa, ni msingi wa Utume
 na matokeo ya Taqwa. Isingelikuwa ni ukweli, hukumu za shari'ah za 
kufunuliwa kutoka mbinguni zingeliporomoka. Kuwa na tabia ya uongo ni 
ujamaa wa kupukusa tabia pekee ya ubinaadamu, kwani kuzungumza uongo ni 
uangamizaji wa hali ya kibinaadam. 
(Bariyqah Mahmuudiyah, Muhammad al-Khaadimi, 3/183) 
Shari'ah
 ya Kiislamu; Qur-aan na Sunnah inatuonya kusema uongo na kwa 
makubaliano ya wanachuoni kwamba ni haramu. Mtu muongo atachuma malipo 
mabaya duniani na Akhera. 
Katika
 shari'ah, kuongopa hakuruhusiwi ila katika hali fulani ambazo 
hazipotezi haki za mtu, au kumwaga damu au kufedhehesha, au kumvunjia 
mtu heshima yake. Bali katika mas-ala ya kuokoa maisha, kusuluhisha 
baina ya watu au kujenga mapenzi baina ya mume na mke umeruhusiwa uongo.
 Wala Shari'ah haikumruhusu mtu aseme uongo wa utani usio na maana kama 
huu wa April Fool.
MAKATAZO YA KUSEMA UONGO
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema:
((إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لاَ يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللّهِ وَأُوْلئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ))
((Wanaozua uongo ni wale tu wasioziamini Ishara za Allaah. Na hao ndio waongo)) [An-Nahl: 105]
Ibn Kathiyr amesema kuhusu Aayah hiyo:
"Allaah
 Anatuambia kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 
sio mzushi au muongo, kwa sababu ni watu waovu tu ambao hawaamini alama 
za Allaah, makafiri na wanafiki wanaojulikana baina ya watu kwa uongo 
wao, uongo kuhusu Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi
 wa sallam). 
Mtume
 Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni mkweli
 kabisa miongoni mwa watu, mcha Mungu, mwenye elimu bora kabisa, mwenye 
matendo mema, tabia njema. Hakuna aliyekuwa na shaka naye hadi kwamba 
aliitwa 'Al-Amiyn' (Mkweli). Hivyo Hercules, mfalme wa Rome alipomuuliza
 Abu Sufyaan kuhusu tabia za Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa
 aalihi wa sallam), jambo moja alilouliza lilikuwa ni: "Je, mmepata 
kumtuhumu kwa uongo kabla ya kusema aliyoyasema?". Alijibu: "Hapana". 
Hercules akasema: "Ikiwa alijiepusha kusema uongo kwa watu basi hawezi 
kusema uongo kuhusu Allaah". [Tafsiyr Ibn Kathiyr, 2/588].
Imetoka
 kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Alama za munaafiq ni tatu; 
akizungumza husema uongo, akitoa ahadi huivunja, akiaminishwa kwa kitu 
hufanya khiyana" [Al-Bukhaariy na Muslim]
UONGO ULIO MUOVU KABISA
1.    Uongo Kuhusu Allaah Na Mtume Wake (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa aalihi Wa Sallam)
Huu
 ni uongo wa hatari kabisa na anayezua hivyo basi hupewa onyo kali. 
Baadhi wa Maulamaa wamesema kwamba anayezua uongo kama huu basi 
ashutumiwe kuwa kafiri. 
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: 
((قُلْ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللّهِ الْكَذِبَ لاَ يُفْلِحُونَ)) 
((Sema: Hao wanaomzulia uongo Allaah hawatofanikiwa)) [Yuunus: 69]
Imetoka
 kwa 'Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba   Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Msinizulie uongo. Yeyote 
atakayezua uongo kuhusu mimi basi ataingia motoni)) [Al-Bukhaariy] 
Imetoka
 kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayenizulia uongo basi
 ajitayarishie makazi yake motoni)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 
Ibnu
 Al-Qayyim amesema kuhusu maana ya Hadiyth hii kwamba:  "Yeyote 
atakayezua uongo kuhusu mimi basi ajitayarishie makazi yake motoni 
ambako ataishi milele, na sio kama kambi ambayo mtu huishi kwa muda 
kisha akahamia kwengine" [Twariyqul-Hijratayn ukurasa 169] 
2.    Uongo Katika Kununua Na Kuuza 
Uongo mwengine ni wakati mtu anapofanya biashara na katika kununua huzua na kuuza pia hudanganya.
Imetoka
 kwa Abu Dharr (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu watatu ambao Allaah 
Hatosema nao siku ya Qiyaamah na wala Hatowatazama wala kuwatukuza, na 
watapata adhabu iumizayo)) Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa 
sallam) alisema mara tatu. Abu Dharr akasema: "Waangamizwe na wapotezwe,
 ni nani hao ewe Mjumbe wa Allaah?" Akasema: (([mwanaume] Mwenye kuachia
 nguo yake ivuke kiwiko cha mguu, mwenye kujisifu, na mwenye kufanya 
biashara yake kwa kuapa uongo)). [Muslim]  
Imesimuliwa
 na Hakiym bin Hizaam (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba "Mtume (Swalla 
Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Watu wawili wanaohusika 
na makubaliano ya biashara wanayo khiyari (ya kuvunja makubaliano) hadi 
watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano yao yatabarikiwa na 
wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa katika makubaliano yao))
 [Al-Bukhaariy na Muslim] 
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:
Allaah
 Ameusia ukweli na uaminifu, na Ameharamisha uongo na khiana katika 
mambo yapasayo kujulikana na kufunuliwa kwa watu kama alivyosema Mtume 
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) 
((Watu wawili wanaohusika na makubaliano ya biashara wanayo khiari (ya 
kuvunja makubaliano) hadi watakapofarikiana. Ikiwa waaminifu makubaliano
 yao yatabarikiwa na wakikhini kitu na kusema uongo, baraka itafutwa 
katika makubaliano yao)) na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema: 
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ لِلّهِ شُهَدَاء بِالْقِسْطِ وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَى أَلاَّ تَعْدِلُواْ اعْدِلُواْ هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَى))  
((Enyi
 mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa 
ushahidi kwa haki. Wala kuchukiana na watu kusikupelekeeni kutofanya 
uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchaji 
Allaah)) [Al-Maaidah: 8] [Minhaajus-Sunnah 1/16]
3.    Kuharamishwa Uongo Kuhusu Njozi Na Ndoto
Hii ni kuhusu baadhi ya watu wanaodai kuwa wameona ndoto kadhaa kisha asubuhi wanawasimulia watu mambo ambayo wala hawakuyaona.
Imetoka
 kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayesimulia ndoto 
ambayo hakuiona, ataamrishwa (Siku ya Qiyaamah) aunganishe pamoja chembe
 mbili za shayiri, lakini hatoweza. Yeyote atakayetega masikio (kwa 
umbea) kusikiliza mazungumzo ya watu ambao wasingelipenda (yeye 
asikilize), au ambao wanamuepuka atamiminiwa shaba ya moto iliyoyeyushwa
 katika masikio yake siku ya Qiyaamah. Na Yeyote atakayetengeneza 
(kuchora au kuchonga) picha ataadhibiwa na ataambiwa aitie uhai (roho) 
na wala hatoweza)) [Al-Bukhaariy]  
Al-Manaawiy
 amesema: "Kuunganisha shayiri mbili, lakini hatoweza kufanya hivyo" kwa
 sababu kuiunga moja kwa mwenziwe haiwezekani kikawaida. Ataadhibiwa 
mpaka aweze kuziunga, na wala hataweza kuziunga. Kama kwamba anasema, 
ameshurutishwa kufanya jambo asiloliweza na anaadhibiwa kwa hilo. Hii ni
 sitiari ya adhabu inayoendelea. Sababu ya kutajwa shayiri hasa, ni 
kwamba ndoto zina uhusiano na hisia (Kwa Kiarabu hisia ni shu'uur), 
maneno ya shayiri na shu'uur yanatokana na mzizi (asili ya neno) mmoja 
katika Kiarabu. 
Adhabu
 ya aina hii ya uongo ni kali sana ingawa anapokuwa macho huenda 
akasababisha madhara zaidi, kwa sababu huenda yakahusiana na kutoa 
ushahidi na huenda yakampelekea kuuliwa au kupewa adhabu ya hadd. Hii ni
 kwa sababu kusema uongo kuhusu ndoto ni kumzulia Allaah (Subhaanahu wa 
Ta'aala) kwani ndoto ni sehemu ya Utume, hivyo zinatoka Kwake. Na 
kumzulia Muumba ni hatari zaidi kuliko kuwazulia viumbe.  
[Faydhul-Kabiyr 6/99] 
4. Kuharamishwa Kusema Kila Anachokisikia Mtu
Imesimuliwa
 kwamba Hafsw bin 'Aaswim amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 
aalihi wa sallam) amesema: ((Inatosheleza kuwa ni uongo kwa mtu 
anayesema kila anachokisikia)) [Muslim] 
"Kutokana
 na maana ya Hadiyth kuhusu maudhui hii, tunaona kwamba inakatazwa 
kutaja au kuhadithia kila jambo analolisikia mtu, kwa sababu kawaida mtu
 anasikia yote ya kweli na uongo. Kwa hiyo ikiwa atasema kila 
anachokisikia atakuwa anasema uongo kwa kusema jambo lisilotokea. 
Tumetaja juu rai za watu wakweli, kwamba uongo una maana kwamba kusema 
au kuelezea jambo katika hali dhidi ya lilivyotokea. Sio sharti juu yake
 ikiwa limefanyika makusudi lakini kufanyika kwake makusudi 
kunashurutisha kuwa ni dhambi. Na Allaah Anajua zaidi" [Sharh Muslim 
1/75] 
5. Uongo Wa Utani
Watu
 wengine wanadhania kwamba inaruhusiwa kusema uongo wakati wa utani. Na 
huu ndio udhuru wanaoutoa katika kuongopa siku ya terehe 1 Aprili au 
siku nyinginezo. Hayo ni makosa. Hakuna msingi wa jambo hili katika 
sharia safi. Kuongopa ni haraam ikiwa ni kwa kutania au kwa dhati. 
Kuongopa kwa kutania ni haramu sawa sawa na kuongopa kwa aina yoyote 
nyingine. 
Imesimuliwa
 kwamba 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mimi hutania lakini sisemi ila 
ni ya kweli)) [At-Twabaraaniy
 katika 'Al-Mu'jam Al-Kabiyr 12/391 – Hadiyth hii imepewa daraja ya 
hasan na Al-Haythamiy katika Majma' Az-Zawaaiyd 8/89 na Shaykh 
Al-Albaaniy ameipa daraja ya sahihi katika Swahiyh Al-Jaami' 2394]] 
Imesimuliwa
 kwamba amesema: "Walisema, ee Mjumbe wa Allaah, unafanya utani na 
sisi". Akasema: ((Lakini nnayoyasema ni ukweli tu)) [At-Tirmidhiy] 
'Abdur-Rahmaan
 bin Abi Layla amesema: "Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 
aalihi wa sallam) wametuambia kuwa walikuwa safarini pamoja na Mjumbe wa
 Allaah. Mtu mmoja miongoni mwao alilala na baadhi yao walikwenda 
kuchukua mishale yake. Alipoamka alishtuka (alipoona mishale yake 
haipo). Watu wakacheka. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa 
sallam) akasema: ((Mnacheka nini?)) Wakasema: "Hakuna kitu isipokuwa 
tumechukua mishale yake na ameshtuka". Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 
aalihi wa sallam) akasema: ((Haimpasi Muislamu kumtisha Muislamu 
mwingine)) [Abu Daawuud, Ahmad na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']
Imesimuliwa
 kutoka kwa 'Abdullaah bin As-Saa'ib bin Yaziyd kutoka kwa baba yake, 
kutoka kwa babu yake kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 
aalihi wa sallam) akisema: ((Haimpasi yeyote katika nyinyi kuchukua kitu
 cha ndugu yake, ikiwa ni kwa utani au kwa vyovyote. Yeyote aliyechukua 
kijiti cha ndugu yake basi akirudishe)) [Abu Daawuud, At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami'] 
6.    Kuongopa Wakati Wa Kucheza Na Watoto
          Lazima
 tutahadhari na kusema uongo tunapocheza na watoto kwa sababu itaandikwa
 katika kitabu cha hesabu. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa 
sallam) ameonya jambo hili. 
         Imesimuliwa kwamba 'Abdullaah bin 'Aamir (Radhiya Allaahu 'anhu) alisema: "Siku moja mama yangu aliniita wakati alipokuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameketi
 nyumbani kwetu. Akasema: Njoo hapa nikupe (kitu). Mtume (Swalla Allaahu
 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Je, unataka kumpa nini?)) 
Akasema: 'Nitampa tende'. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa 
sallam) akasema: ((Kama usingelimpa basi ungelikuwa unasema uongo)). 
         Na
 imesimuliwa kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume 
(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote 
atakayemuambia mtoto 'njoo hapa uchukue hii' kisha asimpe kitu basi 
itahesabiwa ni uongo)) [Abu Daawuud na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya hasan katika Swahiyh Al-Jaami']
7.    Uongo Ili Kuchekesha Watu
Imesimuliwa
 kwamba Mu'aawiyah bin Hadah amesema: "Nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 
'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Ole wake mtu anayezungumza kwa 
ajili ya kuwachekesha watu na akasema uongo, ole wake, ole wake)) [At-Trimidhiy akisema ni hadiyth hasan na Abu Daawuud] 
ADHABU KWA AJILI YA KUSEMA UONGO
Mwenye kusema uongo amepewa onyo kali la adhabu ya hizaya duniani na adhabu kali Akhera nazo ni kama zifuatazo:
Unafiki Katika Moyo
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema: 
((فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ يَكْذِبُونَ))
((Basi
 Akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapokutana Naye, kwa
 sababu ya kuwa walimkhalifu Allaah katika yale waliyomuahidi, na kwa 
sababu ya kusema kwao uongo)) [At-Tawbah: 77] 
'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: "Unaweza kumjua mtu mnafiki kwa mambo matatu; anaposema anaongopa, anapotoa ahadi anaivunja, anapoaminiwa na amana hufanya khiyana". Akasema: "Someni aya hizi: 
وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللّهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ))
 ((فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُواْ بِهِ وَتَوَلَّواْ وَّهُم مُّعْرِضُونَ))
((فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَى يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُواْ اللّهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُواْ  يَكْذِبُونَ))  
((Na
 miongoni mwao wapo waliomuahidi Allaah kwa kusema: Akitupa katika 
fadhila Yake hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika watendao 
mema))  
((Alipowapa katika fadhila Yake wakaifanyia ubakhili na wakageuka, na huku wakipuuza)) 
((Basi
 Akawalipa unafiki kuutia nyoyoni mwao mpaka Siku watapokutana Naye, kwa
 sababu ya kuwa walimkhalifu Allaah katika yale waliyomuahidi, na kwa 
sababu ya kusema kwao uongo)) [At-Tawbah: 75-77]
[Muswanaf Ibn Abi Shaybah, 6/125] 
Uongo Humpeleka Mtu Motoni 
Imesimuliwa
 kwamba 'Abdullaah bin Mas'uud amesema: " Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi 
wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ukweli ni utiifu, na utiifu 
huelekeza Peponi. Mtu ataendelea kusema ukweli hadi Ataandikiwa na 
Allaah kuwa ni mkweli. Uongo ni uovu, na uovu huelekeza motoni. Mtu 
ataendelea kusema uongo hadi Ataandikiwa kuwa ni muongo)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 
As-Swan'aaniy amesema:
"Hadiyth
 hii inaonyesha kwamba yeyote anayeendelea kusema ukweli, itakuwa ni 
wasifu wake, na yeyote anayesema uongo makusudi na kuendelea, itakuwa ni
 wasifu wake. Hii ni sawa kama kitendo chochote kingine chema au kiovu. 
Mtu akiendelea nacho kinakuwa ndio sifa yake. 
Vile
 vile Hadiyth hii inaonyesha jinsi gani ilivyo muhimu kusema ukweli hadi
 kwamba unampeleka mtu Peponi na imeonyesha vipi ubaya wa kusema uongo 
hadi unampeleka mtu motoni. Juu ya hivyo, bado kuna matokeo ya adhabu za
 duniya kwani anayesema ukweli atakuwa anakubaliwa usemi wake na watu na
 ushahidi wake utakubaliwa na jaji na atapendwa kwa yale anayoyasema. 
Ama mtu muongo ni dhidi ya hayo." [Subul-As-Salaam 2/687]
Ushahidi Wake Utakanushwa 
Ibnul-Qayyim amesema kuhusu sababu ya ushahidi wa mtu muongo kukanushwa:
"Sababu
 ya nguvu kabisa kwa nini katika kutoa ushahidi, fatwa na ripoti 
zikanushwe ni kusema uongo, kwa sababu inafisidi asili ya ushahidi, 
fatwa au taarifa. Ni kama ushahidi wa kipofu kuona mwezi mpya, au 
ushahidi wa kiziwi kuhusu kusikia kuruhusiwa kuingia mtu mahali. Ulimi 
unaoongopa ni kama baadhi ya uelekevu ambao haufanyi kazi tena. Hakika 
ni mbaya zaidi kuliko hivyo, kwani kitendo kiovu kabisa mtu kumiliki ni 
ulimi muongo." [I’ilaam Al-Muwaqqi'iyn 1/95]
Nyuso Kuwa Nyeusi Duniani Na Akhera            
    Allaah (Subhaanahu wa Ta'aala) Anasema: 
((وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ تَرَى الَّذِينَ كَذَبُواْ عَلَى اللَّهِ وُجُوهُهُم مُّسْوَدَّةٌ أَلَيْسَ فِي جَهَنَّمَ مَثْوًى لِّلْمُتَكَبِّرِينَ))
((Na
 Siku ya Qiyaamah utawaona waliomsingizia uongo Allaah nyuso zao 
zimesawijika (zimekuwa nyeusi). Je! Si katika Jahannamu makaazi ya 
wanaotakabari?)) [Az-Zumar: 60]
Ibnul-Qayyim
 amesema: "Hivyo siku ya Qiyaamah Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aala) 
Atazifanya nyuso ziwe alama za waliosema uongo kuhusu Allaah na Mjumbe 
Wake. Kusema uongo kunaleta taathira kubwa ya kufanya nyuso ziwe nyeusi 
na kuzifunika na kitambaa cha hizaya na kila mtu mkweli ataziona nyuso 
hizo. Wasifu wa mtu muongo utatambulikana dhahiri kabisa usoni na kila 
mtu aliye na macho ataweza kumuona. Lakini Allaah (Subhaanahu wa 
Ta'aala) Anambariki mtu mkweli kwa hadhi na heshima ili yeyote 
atakayemuona atamuheshimu na kumpenda. Na Atampa muongo fedheha na aibu 
ili yeyote atakayemuona atamchukia na kumdharau. Na Allaah Ni Mwenye 
Chanzo cha Nguvu" [A'alaam Al-Muwaqqi'iyn 1/95]
Mtu Muongo Atachanwa Mashavu Yake Kutoka Kisogoni
Imesimuliwa kwamba Samurah ibn Jundub (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema:"Mtume
 (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaambia mara 
kwa mara Maswahaba zake: ((Je, kuna yeyote miongoni mwenu aliyeona 
ndoto?)). Kisha yeyote aliyejaaliwa na Allaah ataelezea ndoto yake. Siku
 moja alituambia: (([Malaika] Wawili walinijia jana usiku na kuniamsha, 
kisha wakaniambia: 'Twende…' Tukatoka na kwenda hadi tukafika kwa mtu 
aliyelala chali na mwengine amesimama juu ya kichwa chake akiwa na 
ndoana ya chuma. (Akashtuka aliyoyaona na kusema) Na kitu gani cha 
kutazama! Alikuwa akitia ndoana katika upande mmoja mdomoni mwa mwenzake
 (aliyelala) akimchana kutoka upande mmoja wa uso hadi nyuma (ya shingo)
 na hivyo hivyo akiichana pua kutoka mbele hadi nyuma ya macho yake 
kisha akiendelea kufanya hivyo hivyo kama alivyofanya kwa upande 
mwingine. Hawahi kumaliza kumchana upande mmoja ila upande mwingine 
unarudishwa hali yake (ya mwanzo). Kisha hurudia kufanya hivyo hivyo 
upya tena. Nikasema kwa Maswahaba zangu (Malaika) wawili, 'Subhaanahu 
Allaah! Ni watu gani hawa wawili?' Wakaniambia: 'Endelea kwenda, endelea
 kwenda!' (kisha akasema akielezea vipi Malaika wawili wakielezea mambo 
aliyokuwa akiyaona): 'Ama yule mtu uliyemuona kuwa anachanwa mdomo, pua 
na macho yake, ni alama ya mtu anayetoka nyumbani kwake asubuhi na 
kusema uongo mwingi hadi unasambaa duniani kote')) [Al-Bukhaariy]         
KAULI ZA MASWAHABA KUHUSU UONGO
Abu Bakr As-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'anhu):   
"Tahadharini na uongo kwani hauna uhusiano na Iymaan".
'Umar Ibnul-Khatwtwaab (Radhiya Allaahu 'anhu):  
"Iymaan ya dhaati haiwezi kupatikana hadi mtu aache uongo wa utani"
'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu):  
"Mtu
 atasema ukweli na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya 
uovu katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano. Au mtu atasema 
uongo na kuendelea kufanya hivyo hadi hakutakuwa na nafasi ya ukweli 
katika moyo wake japo kama ni wa kiasi cha sindano". 
Vile vile amesema:  "Haimpasi mtu kusema uongo ikiwa ni kwa kutania au kikweli". Kisha Ibn Mas'uud akasoma Ayah: 
((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ اتَّقُواْ اللّهَ وَكُونُواْ مَعَ الصَّادِقِينَ))
((Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli)) [At-Tawbah: 119]
 Sa'ad bin Abi Waqqaasw (Radhiya Allaahu 'anhu)    
"Muumini anaweza kuwa na sifa zote isipokuwa usaliti na uongo"
[Muswannaf Ibn Abi Shaybah, 5/235, 236] 
AINA YA UONGO UNAORUHUSIWA
Uongo
 unaruhusiwa katika hali tatu; kwenye vita, kusuluhisha baina ya watu 
wawili waliogombana, mume kumuongopea mkewe au kinyume chake kwa ajili 
ya mapenzi na maelewano.
Imesimuliwa
 kutoka kwa Ummu Kulthuum bint 'Uqbah (Radhiya Allaahu 'anhaa) kwamba 
amemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: 
((Sio muongo mwenye kupatanisha baina ya watu na akasimulia jambo zuri 
au akasema maneno mazuri)) [Al-Bukhaariy, Muslim]   
Imesimuliwa
 kwamba Asmaa bin Yaziyd amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa 
aalihi wa sallam) amesema: ((Hairuhusiwi kusema uongo isipokuwa katika 
hali tatu; mtu anapozungumza na mkewe katika njia ya kumfurahisha, 
kusema uongo katika vita, na uongo kwa ajili ya kusuluhisha baina ya 
watu)) [At-Tirmidhiy na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh katika Swahiyh Al-Jaami']
KHITIMISHO
Baada
 ya kutambua chanzo cha siku hiyo ya April Fool, uongo na madhara yake, 
basi tujitahidi nafsi zetu kutosherehekea siku hiyo kabisa, ili tubakie 
katika tabia ya ukweli daima. Hata kama si muhimu kujua chanzo cha siku 
hii, bali lililo muhimu ni kujua hukumu ya kusema uongo na khofu ya 
adhabu zake kama tulivyopata mafundisho katika Aayah na Hadiyth 
zilizotangulia.
Hiyo
 ni shari'ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) ambayo ina Hikma 
inayorekebisha nafsi za binaadamu kubakia katika hali ya fitrah (asili 
ya maumbile) ili abakie binaadamu daima ni mwenye kuishi salama na amani
 katika jamii, na vile vile ajiepushe na adhabu kali Alizoziandaa Mola 
Mtukufu kwa maovu kama hayo. 
Mafundisho
 muhimu na yatakayoonekana mapya kwa wengi wetu tunayoyapata katika 
makala haya ni kujihadhari na matani yaliyojaa uongo; tukitazama matani 
mengi hadi yawe matani basi kutakuwepo na uongo ndani yake, na utani 
haufurahishi kwa wengi hadi uwe na udanganyifu na hila ndani yake, hivyo
 tujihadhari sana Waislam na uongo kwenye matani. Vilevile tujiepushe na
 tabia mbaya ambayo baadhi yetu wanaipenda, nayo ni kuleta matani watu 
wacheke, au kuwafurahisha watu kwa matani. Kuna watu kazi yao kukaa 
vijiweni na kumwaga matani hadi wakawa wanajulikana kwa sifa hiyo na 
wasipoonekana siku moja ni pengo kwenye kijiwe! Hadi inafika mtu jina 
lake kubadilishwa na kuitwa Fulani Matani! Na kuna wengine ambao tabia 
yao ni kupenda kuwa katika mwangaza daima (kuonekana) na kuwa na tabia 
ya kujipendekeza na haswa kwa watu wa jinsia tofauti ili akusanye sifa 
au kupendeka, mwisho akawa anajulikana kwa kufanya sifa hizo na vituko 
ambavyo vimejaa uongo, matusi, kuigiza wenzake, kebehi n.k.
Kadhaalika, tuifuate Hadiyth isemayo: ((Mwenye kumuamini Allaah na siku ya mwisho, aseme kheri (maneno mazuri/ukweli) au anyamaze...)) [Hadiyth kutoka kwa Abu Hurayrah iliyosimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]
Tunamuomba
 Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aturuzuku ukweli daima na Ajaalie ndimi 
zetu ziseme yanayopasa tu kusema na Atujaalie miongoni mwa walioamini na
 wasemao kweli (Swiddiyqiyn). Aamiyn.


0 comments:
Post a Comment