Askari wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI), tayari wapo
Arusha kushirikiana na polisi ili kuchunguza tukio la mlipuko wa bomu la
kutupa kwa mkono kwenye mkutano wa kampeni za Chadema.
Katika tukio hilo lililotokea Juni 15, mwaka huu
Viwanja vya Soweto, eneo la Kaloleni, Arusha, watu wanne walipoteza
maisha huku zaidi ya 60 wakijeruhiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas, alithibitisha ushiriki wa FBI katika upelelezi huo.
Licha ya FBI, polisi wanashirikiana na wenzao
kutoka nchi jirani ya Kenya, ambao wana uzoefu na matukio ya milipuko ya
mabomu yanayotokea nchini mwao mara kwa mara, hasa baada ya nchi hiyo
kupeleka wanajeshi nchini Somalia kukabiliana na Kundi la Al-Shabaab.
“Tunaendelea na uchunguzi wa kina mlipuko wa bomu
Soweto, tayari wenzetu wa FBI na polisi wa Kenya wamefika kushirikiana
nasi, nachukua fursa hii kuwaomba wenye ushahidi utakaosaidia upelelezi
kujitokeza,” alisema Sabas.
Serikali imetangaza zawadi ya Sh100 milioni kwa
yeyote atakayetoa taarifa itakayosaidia kumpata aliyehusika, au
wanaohusika na mlipuko huo.
Sabas alisema watu watatu waliokuwa wakishikilia na polisi kwa mahojiano kuhusu bomu hilo, tayari wameachiwa kwa dhamana.
Hii ni mara ya pili maofisa wa FBI na polisi kutoka Kenya kushiriki uchunguzi wa mlipuko wa bomu Arusha.
Mara ya kwanza walishiriki kuchunguza mlipuko
uliotokea kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, eneo la Olasiti
iliyotokea Mei 5, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bomu lililolipuka Soweto ni la kijeshi na limetengenezwa nchini China.
Uchaguzi wa madiwani kata nne za Elerai,
Kimandolu, Themi na Kaloleni, uliahirishwa hadi Juni 30, mwaka huu kabla
ya kusogezwa mbele tena hadi Julai 14, kwa kile kilichoelezwa na
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva, kuwa sababu za usalama.
Wakati huohuo, Serikali imetangaza kugundua
mtandao wa milipuko ya mabomu yaliyotokea Kanisa la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi, eneo la Olasiti na Viwanja vya Soweto, Arusha.