Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 25 June 2013

Chakula cha sumu chaua mtoto, nduguze wanne hoi





Mtoto Kaneza Nicodem anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka saba, amefariki dunia na wengine wanne wa familia moja kunusurika baada ya kula chakula kinachodhaniwa kuwa na suku.
Marehemu huyo na ndugu zake waliokutwa na mkasa huo ni wakazi wa kijiji cha Rulenge wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera.

Mganga wa zamu wa hospitali ya Rulenge wilayani Ngara inayomilikiwa na Kanisa Katoliki, Dk. Therezia Kaluhanga, alisema kuwa mtoto huyo alipoteza maisha wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Dk. Kaluhanga aliwataja walionusurika kifo ambao bado wamelazwa katika hospitali hiyo kuwa ni Korona Nicodem (12), Matusi Nicodem (3), Cornery Nicodem (10) na mama yao mzazi, Genogeva Nicodem.

 Alisema kuwa watu hao walifikishwa hospitalini hapo juzi saa kumi alasiri wakiwa wanatapika na kuharisha baada ya kula chakula cha mchana kinachohofiwa kuwa kilikuwa na sumu na kuwa hali za walionusurika zinaendelea vizuri.

Hata hivyo,  Dk. Kaluhanga hakueleza aina ya chakula ambacho watu hao walikula kabla ya kukumbwa na athari hizo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa uchunguzi unafanyika ili kubaini chanzo chake.


0 comments:

Post a Comment