Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 27 June 2013

Wananchi wakimbilia mahakamani kupinga utandazaji bomba la Dawasa




Baadhi ya wananchi wanaotakiwa kuhama kupisha utandazaji wa bomba kubwa la kusukuma maji kutoka Ruvu Chini wilayani  Bagamoyo mkoani Pwani kwenda Dar es Salaam, wamekimbilia mahakamani kupinga kubomolewa kwa madai kuwa wanazo hati halali za kumiliki ardhi yao.

Diwani wa Kata ya Wazo jijini Dar es Salaam, John Moro, alisema wananchi waliokimbilia mahakamni ni wanaishi eneo la Salasala.

Alithibitisha kupokea malalamiko kadhaa wenye hati wakidai kwamba hawapo tayari kubomolewa kwa kuwa walipata maeneo hayo kwa njia za halali na kwamba wanazo hati zilizotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Wananchi wenye hati ambao bomba linawapitia hawawezi kuondolewa kimabavu, ni lazima mazungumzo yafanyike ili kuhakikisha kila upande unapata hai yake,” alisema Moro.

Alisema wanaendelea kuwaelimisha wananchi hao waliokwenda mahakamani na wale wanaokaidi kuhama kupisha zoezi la kulaza bomba umuhimu wa wao kukubali kuvunjiwa nyumba zao ama ukuta uliozidi ili mradi huo uweze kukamilika.

“Kwa kushirikiana na Dawasa tunawaita wananchi hao ambao kwa sasa hawazidi 15 waliobaki ili kuwaomba wengine sita waondoe kesi mahakamani na wengine wakubali kupokea fidia za mali zao ili wakubali kuachia ardhi kupisha kupisha ulazaji wa bomba,” alisema.

Mthamnini wa ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Benada Komba, alithibitisha kuwa hati walizonazo wananchi hao ni halali.

Alisema wananchi sita wanazo hati halali zilizotolewa na ofisi ya Kamishina wa Ardhi na barua halali kutoka Dawasa zinazowaruhusu kujenga na kuishi katika maeneo wanayotakiwa kuhama.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Boniface Kasiga, alisema mazungumzo ya kumaliza suala hilo yanaendelea.

Kasiga alisema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam na kuwataka wananchi wanaokaidi kuhama wakubali kuondoka kupitia mazungumzo.

Bomba hilo litawekwa urefu wa kilomita 56 kutoka chanzo cha maji cha Ruvu Chini hadi matangi yaliyopo Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), litakuwa na uwezo wa kusukuma lita za ujazo milioni 270  kwa siku na litafanya kazi sambamba na hili lililopo sasa ambalo linasukuma lita za ujazo milioni 180 kwa siku.

Wakazi hao wanatakiwa kuhama kupisha mradi huo ambao utakuwa ukombozi mkubwa kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ambao wanaokabiliwa na tatizo sugu la uhaba wa maji.
Maeneo ambayo wakazi wake wataathirika kutokana na mradi huo ni vijiji vya Buma, Kerege, Majingu, Kiromo katika Wilaya ya Bagamoyo na maeneo ya Bunju, Boko na Wazo jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya maeneo ni mashamba ambayo hawaishi watu na mujibu wa Dawasa njia ya bomba hilo inatakiwa kuwa nyeupe bila kuingiliwa na mtu yeyote kwa kujenga ama kufanya shughuli yoyote.

Kwa upande wake, Mhandishi Mkazi wa mradi huo kutoka kampuni ya JBG ya nchini Ujerumani, Chrispina Mwashala, alisema mradi huo uliaonza mwaka jana mwishoni, utakamilika mwaka 2014.
 

 
 

0 comments:

Post a Comment