Utafiti huo umebaini kwamba, baadhi ya wakulima wanaponyunyuzia
dawa za kuulia wadudu waharibifu wa mazao katika bustani za mboga,
vyombo wanavyowekea dawa hizo huvisafisha katika vyanzo hivyo vya maji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Mazingira ya Pamoja, Stuart
Hedi, wakulima wamekuwa wakitumia maji hayo kusafishia zana zao za
kilimo kutokana na uelewa mdogo juu ya kanuni za afya na matumizi sahihi
ya dawa hizo na athari zake kwa binadamu.
“Kila dawa ina kanuni za matumizi kama hutazifuata lazima kuna
athari zitakazojitokeza na hii inatokana na kiwango cha uelewa kwa
watumiaji sasa hawa wanahitaji kufuatiliwa kwa karibu na kuelimishwa kwa
sababu jambo hili likiachwa athari zake ni kubwa kwani hata mboga
wanazonyunyizia zina muda zinazotakiwa kukaa kabla ya kuvunwa” alisema
Hedi.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mwandamizi wa NEMC, Dk.Carlos Mbuta,
alisema uchunguzi uliofanywa katika vijiji vya Lukozi na Mnadani
vilivyopo katika kata ya Malindi, umeonyesha kuwa baadhi wakulima
hawazingatii maelekezo ya maafisa ugani wakati wa kunyunyiza dawa hizo
katika mazao yao, hivyo pia wanahatarisha maisha ya watumiaji wa mboga
maeneo ya mjini ambao ndio wateja wao wakubwa.
“Athari hizi kwa hali hii inaweza zisitokee kwa watumiaji wa maji
tu kwenye vyanzo hivi, lakini hata kwa walaji wa mboga zinazozalishwa
hivyo ni vema wakulima wakaelimishwa ipasavyo namna ya kutumia dawa hizi
bila kuleta athari kwa walaji” alisisitiza Dk. Mbuta.
Mmoja wa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha nyanya, kabichi na
vitunguu, Jumaa Mngazija, alisema hatua hiyo inatokana na baadhi ya
wakulima kukataa kuheshimu sheria ndogo ndogo zilizotungwa na serikali
za vijiji, ambapo baadhi yao huendelea kumwaga kwa makusudi kemikali
hizo.
Naye Afisa Ugani wa Kata ya Malindi, Kimomwe Halifa, alisema
wakulima wamekuwa wakaidi licha ya kupewa elimu ya matumizi ya dawa hizo
na kuwataka kuacha vitendo hivyo kwa sababu athari zake sio tu
zitawakumba walaji wa mboga bali hata wao wenyewe na familia zao
kutokana na matumizi ya maji hayo yanayomwagiwa kemikali zenye sumu.
0 comments:
Post a Comment