Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Monday 10 June 2013

SIKU YA WACHANGIA DAMU DUNIANI TAREHE 14 JUNI 2013.

                               

                              01 Shaaban,1434 Hijiriyah/ June10 ,2013 Miyladiyah
 
Mh. Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr. Seif S. Rashid.(Kulia) akiongea na waandishi wa Habari hawapo pichani mapema leo katika mkutano wa kutoa taarifa juu ya madhimisho ya siku ya Wachangia Damu Duniani inayotarajiwa


Tarehe 14 Juni 2013, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama inaadhimisha siku ya wachangia damu duniani. Kidunia maadhimisho haya yatafanyika Paris nchini Ufaransa. Kitaifa Maadhimisho haya mwaka huu yatafanyika Musoma Mkoani Mara katika kiwanja cha Mkendo siku ya Ijumaa tarehe 14,Juni 2013 kuanzia saa 3 asubuhi na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dr Hussein Mwinyi (MB)
Madhumuni ya maadhimisho haya ni kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ,kuwatambua, kuwaenzi na kuwashukuru walewote ambao wamekuwa wakichangia damu kwa hiari mara kwa mara bila malipo yoyote.
Ndugu Wananchi,
Duniani kote, maelfu ya watu huokolewa maisha na damu ya watu ambao hawajawahi kukutana nao, watu ambao huchangia damu yao ili kuwasaidia wengine. Lakini mamilioni bado hawawezi kupata huduma ya damu salama pindi wanapohitaji. Siku ya leo inatoa fursa ya kipekee kuwashukuru wale watu maalumu ambao huchangia damu ili kuokoa maisha ya wahitaji. Tunaweza pia kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari ili Watanzania wajenge utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara
Ndugu Wananchi
Kauli mbiu ya siku ya wachangia damu mwaka huu ni UCHANGIAJI DAMU NI ZAWADI YA MAISHA. Maadhimisho haya yanaenda sambamba na madhimisho ya miaka 10 ya siku ya wachangia damu duniani.
Zawadi kubwa ya thamani ambayo sisi binadamu tunaweza kupeana ni kuchangiana damu, zawadi ambayo inaweza kuokoa maisha na kutoa nguvu mpya ya maisha kwa watu wengi wanaohitaji tiba hii.
Kila mmoja wetu anaweza kutoa zawadi ya maisha kwa kuchangia damu, ndiyo maana dunia inaadhimisha siku hii ili kuwatambua watu ambao wamekuwa wakitoa zawadi ya maisha kwa kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine
Ndugu Wananchi,
Kwanini uchangiaji damu ni zawadi ya maisha?
Damu ni uhai na ina thamani kubwa, damu haipatikani viwandani wala kuzalishwa sehemu yeyote ila kwa kuchangiwa na binadamu wenzetu.
Hivyo zoezi la kuchangia damu ni endelevu na la kudumu, chupa moja ya damu inaweza kuokoa maisha ya watu zaidi ya mmoja kama ikigawanywa kwenye mazao ya damu kama vileplasma, chembe sahani na chembe nyekundu. Damu inaweza kuhifadhiwa kwa muda wa siku 35 kabla ya muda wake wa kutumika kwisha kulingana na virutubisho vilivyopo. Kutokana na uhifadhi wa damu kwa muda mfupi ndiyo maana tunasisitiza umuhimu wa watu kuchangia mara kwa mara. Kitaalamu mwanamume anaweza kuchangia mara nne kwa mwaka na mwanamke mara tatu kwa mwaka.


Ndugu Wananchi,
Upatikanaji wa damu kwa wakati huongeza nafasi ya kuishi kwa wahitaji wa damu, huduma ya damu huokoa maisha ya mamilioni ya wagonjwa kila mwaka duniani, Yafuatayo ni makundi makuu ya watu ambao huitaji damu:

Watoto wadogo hasa walio chini ya umri wa miaka mitano kutokana na upungufu wa damu unaosababishwa na malaria kali na magonjwa mengine (50%)

Wajawazito na wanawake wenye matatizo ya uzazi (30%)

Majeruhi wa ajali mbalimbali hasa ajali za barabarani na watu wanaofanyiwa tiba ya upasuaji (15%)

Wale wote wenye magonjwa mbalimbali yanayosababisha upungufu wa damu kamawagonjwa wa saratani, watu wanaosumbuliwa na seli mundu na hemophilia (5%)

Ndugu Wananchi,
Tangu kuanzishwa kwa Mpango wa Damu Salama Tanzania kumekuwepo na ongezeko la wachangia damu wa hiari kutoka kiasi cha chupa 5,000 mwaka 2005 hadi kiasi cha chupa 120,000 mwaka 2012. Hata hivyo kiasi hiki hakikidhi mahitaji halisi nchini ambapo wastani wa chupa 400,000-450,000 zinahitajika kwa mwaka. Hii inaonyesha nakisi kubwa iliyoko ya upatikanaji damu kwenye hospitali zetu. Nakisi hii mara nyingi imekuwa inafidiwa na ndugu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa. Lengo la Mpango ni kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji damu wa hiari.
Hata hivyo, katika nchi nyingi Tanzania ikwemo, hakuna ugavi wa damu salama unaotosheleza, na huduma za damu hukabiliwa na changamoto ya kupatikana kwa damu ya kutosha, na wakati huo huo kuhakikisha ubora na usalama wa damu hiyo
Usambazaji wa damu ya kutosha unaweza kuwa wa uhakika kupitia uchangiaji damu wa mara kwa mara na wa hiari usiohitaji malipo. Lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kwa nchi zote kupata mahitaji yao yote ya damu inayohitajika kutoka kwa wachangiaji wa hiari wasiolipwa ifikapo mwaka 2020. Leo hii, ni nchi 62 tu, ambazo usambazaji wa damu kitaifa unatokana na uchangiaji wa hiari usio na malipo takribani kwa asilimia 100, huku kukiwa na nchi 40 ambazo bado zinategemea wachangiaji wa familia Tanzania ikiwemo.
Ndugu wananchi;
Katika hatua ya kuboresha kazi za ukusanyaji, upimaji na usambazaji wa damu hospitalini, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeanzisha mfumo wa kisasa wa tekinolojia ya habari na Mawasiliano-ICT (Blood Establishment computer System) ambapo mpaka sasa mfumo huu umeshafungwa katika kanda tano ambazo niKanda ya Ziwa(Mwanza),Kanda ya Kaskazini(Moshi), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini(Mbeya), Kanda ya Mashariki (Dar-es-salaam) na Zanzibar
Katika mfumo huu taarifa muhimu kuanzia kwa mchangiaji hadi damu inapomfikia mgonjwa zitapatikana kwa urahisi. Vilevile mfumo huu utasaidia kutambua wachangiaji wa mara kwa mara na hivyo kuweza kuongeza idadi ya wachangiaji wa kudumu wa mara kwa mara(regular blood donors). Aidha mfumo huu unasaidia kutambua viashiria mbalimbali ikiwemo kiasi cha maambukizi ya magonjwa mbalimbali yanayosababishwa kwa kuongezewa damu na hivyo kuhakikisha usalama wa mgonwa anayepewa damu. Pia mfumo umerahisisha upatikanaji wa takwimu mbalimbali ikiwemo usambazaji wa damu salama kwenye hosipitali zetu.
Pia katika hatua za kuhakikisha Mpango unatoa huduma bora zinazoendana na viwango vya kimataifa, Mpango umeanza mchakato wa kupata kibali (accreditation) kwa ajili ya kanda za Mpango wa Damu Salama. Mchakato huu umeanza kwa hatua ya kupitia miongozo na sera katika mtiririko mzima wa upatikanaji wa damu salama na ukaguzi wa ndani. Katika hatua ya mwanzo inakadiriwa ifikapo mwaka 2014 vituo viwili vya Damu Salama vitakuwa vimepata Cheti kutambulisha kuwa vinatoa huduma kulingana na viwango vya kimataifa
Ndugu Wananchi,
Mpango umeanzisha matumizi ya mitandao ya kijamii, hizi ni tovuti zilizoundwa ili kuwezesha na kuongeza ufanisi wa mawasiliano baina ya mpango na wadau wake. Lengo likiwa kuwafikia zaidi wananchi wote wa Tanzania waliopo katika mitandao hii. Tovuti hizi ni kama "Facebook, Tweeter na YouTube". Uanzishaji wa mitandao hiiinaiwezesha Damu salama kujulikana, kukuza na kuimarisha mahusiano mazuri kati ya damu salama na wachangia damu, wafadhili na wadau wengine kupitia kubadilishana habari kwa njia ya haraka na kwa wakati. Mpango unawasihi na kuwaomba wananchi kujiunga kufuatilia na kutumia vyombo hivi ili kuongeza ufanisi waMpango wa Taifa wa Damu Salama na hivyo kuongeza makusanyo ya damu toka kwa wachangiaji wa hiari.

Ndugu Wananchi,
Nchini Tanzania mahitaji ya damu yanazidi upatikanaji. Mpango wa Taifa wa Damu Salama unakabiliwa na changamoto ya kuhakikishaupatikanaji wa damu salama na ya kutosha ili kuweza kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji damu hospitalini. Mahitaji ya damu kitaifa ni wastani wa chupa 400,000-450,000. Mpango wa Taifa wa Damu Salama kwa sasa unakusanya wastani wa chupa 120,000 kwa mwaka(26%). Hii inaonyesha nakisi kubwa iliyoko ya upatikanaji damu kwenye hospitali zetu. Nakisi hii mara nyingi imekuwa inafidiwa na ndugu kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mgonjwa. Lengo la Mpango ni kukusanya damu kwa 100% toka kwa wachangiaji damu wa hiari.Mikakati kadhaa imewekwa kukabiliana na changamoto hii kama tutakavyoona baadaye.
Changamoto nyingine ni kama ifuatavyo;
Uelewa mdogo katika jamii kuhusu suala zima la uchangiaji damu kwa hiari kwani mfumo uliozoeleka ni ndugu wa mgonjwa kuchangia damu
Uhamasishaji usiotosheleza toka kwa viongozi mbalimbali wa jamii,wanasiasa,viongozi wa dini nk.
Uuzwaji wa damu usio halali hospitalini jambo mbalo linawakatisha tamaa wachangia damu wa hiari
Matumizi yasiyo sahihi ya damu katika hospitali na
Miudombinu hafifu hususan barabara duni wakati wa kukusanya na kusambaza damu
Ndugu Wananchi
Mpango wa Taifa wa Damu Salama umeweka mikakati ili kukabiliana na changamoto na kufikia malengo kama ifuatavyo;
Kufanya kampeni ya kuhamasisha uchangiaji damu katika jamii (Community Campaign), Kampeni hii ina lengo la kuhakikisha upatikanaji wa damu ya kutosha wakati wanafunzi ambao ndio wadau wakubwa wapo likizo
Kuongeza vituo vidogo vya kuchangia damu- "Blood collection satellite sites" katika sehemu mbalimbali za nchi. Kwa sasa Mpango una vituo vidogo vinne Dar-es-salaam- Mnazi Mmoja , Dodoma, Lindi na Morogoro ambavyo vina uwezo wa kukusanya chupa za damu 18,000 kwa mwaka
Kushirikiana na uongozi wa mkoa kupitia mganga mkuu wa mkoa ili wilaya zitenge bajeti ya kukusanya damu kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa damu salamaKufanya mkakati wa kujua matumizi halisi ya damu (Blood need assessment) nchini na kuendelea kuhamasisha madaktari, wauguzi na watumishi wa maabara juu ya matumizi sahihi ya damu
Kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali Puplic Private Partnership(PPP) kuhakikisha Mpango unafikia malengo ya kukusanya chupa za kutosha za damu
Kuendelea kuelimisha jamii kuhusu damu haiuzwi kwa kutumia vyombo vya habari na vipeperushi pia kutumia vifungashio vya damu (Blood bag) vyenye ujumbe "DAMU HAIUZWI"
Kuendelea kuelimisha na kuhamasisha jamii (nje ya shule na vyuo) umuhimu wa kuchangia damu kwa hiari
Kutoa majibu, na ushauri nasaha ndani yawiki mbili mpaka nne baada ya mtu kuchangia damu lengo ni kufikia 75% ya wachangiaji damu wa hiari ifikapo mwishoni mwa 2014. Kwa sasa Mpango umeweza kutoa majibu na ushauri nasaha kwa 58% ya wachangiaji damu wa hiari.
Kuanzisha utaratibu wa kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa njia ya simu kwa wachangia damu. Ujumbe huo utakuwa wa kuhamasisha, kumkumbusha mchangiaji siku ya kuchangia tena damu n.k
Kuongeza utengenezaji wa mazao mbalimbali ya damu (Blood Products) toka30% ya sasa mpaka 50% mwaka 2014.
Kuongeza kiwango cha asilimia ya wachangia damu wa mara kwa mara kutoka 20% kwa sasa (Repeat donors), hadi 50%ifikapo mwaka 2015 . Mpango utahakikisha unatembelea taasisi kwa ajili ya kuchangia damu angalau mara mbili kwa mwaka.
Ndugu Wananchi;
Uchangiaji damu wa hiari wa bila malipo yoyote na wa mara kwa mara ni msingi wa upatikanaji wa damu salama na ya kutosha. Wachangiaji damu wa kujirudia ni salama kwani damu yao hainakiwango kikubwa cha maambukizo ya magonjwa yanayoweza kuenezwa kwa njia ya damu. Lengo la Shirika la Afya Duniani (WHO) ni kwa nchi zote kupata mahitaji yao yote ya damu inayohitajika kutoka kwa wachangiaji wa hiari wasiolipwa ifikapo mwaka 2020

Ndugu Wananchi;
Natoa rai/ujumbe kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kuchangia damu kwa hiari mara kwa mara ili nchi iwe na akiba ya damu ya kutosha , kwani asilimia moja ya Watanzania wakiamua kuwa wachangiaji damu wa kujirudiaMpango wa Taifa wa Damu Salama utaweza kukidhi mahitaji ya damu nchini.
NAMALIZIA KWA KUSEMA NAOMBA WANANCHI WAJITOKEZE KWA WINGI SIKU HIYO ILI TUONYESHE MSHIKAMANO NA KUTOA ZAWADI YA MAISHA KWA KUCHANGIA DAMU. PAMOJA INAWEZEKANA

0 comments:

Post a Comment