Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday, 13 June 2013

Kesi ya ghorofa lililoanguka na kuua yaahirishwa
 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imehairisha kesi ya mfanyabiashara Razah Hussein Ladha na wenzake 10 wanaokabiliwa na jumla ya makosa 24 ya kuua bila kukusudia kufuatia jengo la ghorofa 16 kubomoka jijini Dar es Salaam na kuua watu 36.

Washitakiwa wengine ni Godluck Mbaga, Wilbroad Mugabisyo, Ibrahim Kisoki, Mohamed Abdubakari, Charles Salu, Zonazea Anage,Vedasto Ferand, Michael Hemed  Hemed, Albert  Jones na Joseph  Ringo.

Kesi hiyo ilihairishwa jana na Hakimu Devotha Kisoka, kutokana na upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, na itakuja tena Julai 15, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Awali walisomewa  mashitaka 24 yanayowakabili ambayo yanafanana ya kuua bila kukusudia kinyume na kifungu cha 195 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa  Machi 29 mwaka huu katika eneo la Mtaa wa Indira Gandhi waliwaua watu bila kukusudia.

Hata hivyo washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ni Mahakama Kuu.

Machi 29 mwaka huu, ghorofa mmoja lililokuwa linajengwa katika mtaa wa Indira Gandhi lilianguka na kusababisha watu  36 kupoteza maisha.

0 comments:

Post a Comment