Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 13 June 2013

Chenge: Fedha nyingi hazipelekwi kwenye vipaumbele

                                

Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge amesema fedha nyingi zinazotengwa kwa ajili ya vipaumbele, hazipelekwi kwenye maeneo husika na huelekezwa maeneo mengine.
Chenge alikuwa akiwasilisha Taarifa ya Kamati ya Bajeti ya Bunge mjini Dodoma jana kuhusu majumuisho ya uchambuzi wa hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Kamati za Kisekta kwa ajili ya Bajeti ya mwaka 2013/14.
Vipaumbele vinavyotajwa katiba bajeti hiyo ni pamoja na maji, kilimo, miundombinu hasa barabara, mifugo, uvuvi na nishati ya umeme. “Kamati imeiagiza Serikali kusimamia fedha zinazopelekwa kwenye vipaumbele, zitumike kama zilivyoombwa na pia imeitaka Serikali kuhakikisha miradi inayoanzishwa imalizike kwa wakati na zaidi kulinda fedha ili kufanikisha kilichopangwa,” alisema Chenge.
Alisema wamesikiliza hoja mbalimbali za mawaziri, naibu mawaziri, wataalamu wa Hazina, Mipango na makatibu na wengi walitoa hoja kutaka kuongezewa kasma kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
Chenge alisema pamoja na kukubaliana kimsingi kuongeza fedha katika baadhi ya maeneo, aliitaka Serikali kuhakikisha fedha hizo zinatumika katika vipaumbele vilivyoombewa fedha hizo. Alisema kuwa Kamati ilipokea hoja 70, kati ya hizo 32 zilikuwa na maombi ya ziada na hoja 39 zilihitaji fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na malipo ya madeni.
Hata hivyo, alisema baadhi ya mafungu yaliidhinishwa na Bunge bila kupitia kwenye kamati ikiwemo; Maji Sh184.5 bilioni, Uchukuzi Sh30 bilioni, Viwanda na Biashara Sh30 bilioni na Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Sh9 bilioni.
Mafungu mengine kwa waendesha mashtaka ni Sh10 bilioni na Mahakama Sh20 bilioni na kufanya nyongeza hizo kufikia Sh283.5 bilioni. Jumla ya fedha zilizoombwa ni Sh370.71 bilioni wakati Serikali imeridhia kutoa Sh229.5 bilioni kati ya hizo. Maeneo mengine yaliyotaka nyongeza za fedha na kuridhiwa na kamati na baada ya mashauriano na Serikali ni; Wizara ya Kazi na Ajira Sh350 bilioni, Kilimo na Chakula kwa ajili ya ruzuku ya mbolea Sh21.15 bilioni.
Fedha nyingine ni Sh2 bilioni kwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sh186 bilioni kwa ajili ya Wizara ya Nishati kwa ajili ya Mpango wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (Rea), Mifugo na Uvuvi Sh20 bilioni ambazo zinafanya jumla kuwa Sh654.21 bilioni.
 

0 comments:

Post a Comment