Siku chache baada ya mtu mmoja kujeruhiwa sehemu ya jicho
katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani jijini Arusha, mtu mwingine
amevamiwa na kukatwa na shoka mdongoni.
Aliyekatwa shoka ni Amos Ibrahim mfuasi wa
Chadema, ambaye hadi jana, alikuwa amelazwa katika hospitali ya Mkoa ya
Mount Meru. Mtu wa kwanza kujeruhiwa katika kampeni hizo ni Mwenyekiti
wa Vijana wa CCM Kata ya Engutoto, Joseph Laizer aliyejeruhiwa akiwa
katika Kata ya Themi.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa, akizungumza na Mwananchi alisema Ibrahim alivamiwa usiku wa kuamkia leo.
“Kijana huyu, alivamiwa na vijana wa CCM waliokuwa
wanapiga kampeni za nyumba kwa nyumba usiku na walipofika kwenye chumba
chake eneo la majengo alisema yeye ni Chadema na hivyo hatawapa kura na
ndipo walimpiga,” alisema Golugwa.
“Baada ya tukio hili, tulitoa taarifa polisi
tukapewa RB namba AR/RB/7134/2013 na tukapewa hati ya matibabu lakini
wahusika hawajakamatwa” alisema Golugwa.
Alisema kutokana na vurugu ambazo sasa zimeanza
kushamiri, wafuasi wa Chadema watakuwa wakijilinda wenyewe na
watawakamata watuhumiwa na kuwashughulikia na baadaye ndiyo watapelekwa
Polisi.
“Tutawakamata watuhumiwa, tutawashughulikia na baadaye ndiyo tutawapeleka Polisi” alisema Golugwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Dk
Wilfred Soileli alikana kuwa wafuasi wa CCM kutenda kosa hilo na
kueleza vijana wa Chadema ndiyo wamekuwa wakifanya uvamizi.
“Sisi hatuna taarifa za vijana wetu kufanya
uhalifu huo, ila sisi ndiyo tumekuwa tukipigwa na kuzomewa mara kwa mara
na vijana wa Chadema,” alisema Dk Soileli.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema, jeshi hilo linafanya uchunguzi wa matukio ya vurugu na wahusika
watakamatwa.
“Tunataka kampeni ziwe za amani na utulivu, sasa kama kuna wakorofi hatua za kisheria zitachukuliwa tu” alisema Kamanda Sabas.
Uchaguzi wa udiwani wa kata nne za Kaloleni,
Themi, Kimandolu na Elerai, utafanyika Juni 16 mwaka huu, baada ya
waliokuwa madiwani kufukuzwa uanachama na Chadema.
0 comments:
Post a Comment