Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Thursday 23 May 2013

Watakaofanya vizuri kidato cha nne kwenda China

Serikali ya Tanzania na China zimekubaliana kutoa fursa kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne na kufaulu vizuri   kujiunga na elimu ya vyuo vikuu nchini China.

Lengo la makubaliano hayo ni kupunguza wimbi kubwa la vijana wanaoendelea na vidato vya juu, ili kutoa fursa kwa baadhi ya vijana wenye uwezo wa kuendelea na masomo ya elimu ya juu lakini huwa wanakosa.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa katika maonyesho ya vyuo vikuu yanayofanyika nchini kwa siku mbili.

Waziri Kawambwa alisema vijana waliowengi wanahitimu masomo ya kidato cha nne na kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu kutokana na kushindwa kuendelea na masomo ya kidato cha sita.

“Katika maonyesho hayo ya vyuo vikuu nchi ya China imeleta vyuo 34 na kuonesha fani wanazotoa katika vyuo hivi wametushauri vijana wetu watakapohitimu kidato cha nne wapate fursa ya kujiunga na vyuo vikuu vilivyo nchini kwao,” alisema.

Alisema nchi ya China wapo tayari kupokea wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo ya kidato cha nne.

Makamu wa Rais,Dk Mohamed Gharib Bilal, alisema hadi kufikia mwaka 2015/16 serikali itakuwa imeongeza udahilli wa wanafunzi kutoka 40,000 ilivyo hivi sasa hadi kufikia 80,000.

Pia alisema maonyesho hayo yanatoa fursa kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Sifuni Mchome, alisema jumla ya vyuo vikuu 120 kutoka ndani na nje ya nchi vinashiriki maonyesho hayo.
Alisema kuwa lengo la maonyesho hayo ni kukuza umoja wa vyuo vikuu mbalimbali, ili kujengeana uwezo.

0 comments:

Post a Comment