Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday 28 May 2013

Wananchi wengi wanatumia tiba za asili




 Licha ya kuwepo kwa dawa nyingi za  kisasa nchini, lakini imeelezwa kuwa asilimia 60 ya wananchi wanatumia tiba za asili katika kukabiliana na maradhi mbalimbali yanayowasumbua.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Kaimu Mganga Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Mohamed Ally Mohamed, wakati wa mdahalo wa kutathmini maendeleo ya tiba asili kwa miaka 50 iliyopita.

“Kiasi hiki cha wananchi si kidogo na wala hakitakiwi kupuuzwa, hivyo serikali imeamua kuanzisha kitengo na baraza linaloshughulikia masuala ya tiba asili nchini,” alisema.

Dk. Mohamed aliyekuwa akimwakilisha Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dunford Makala, alisema licha ya kuwepo na kitengo hicho, pia Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu na Taasisi ya Utafiti wa Tiba Asili Muhimbili (Muhas) inashughulikia masuala ya dawa asili.

Hata hivyo, Dk. Mohamed alisema licha ya idadi kubwa ya wananchi kutumia tiba asili, lakini baadhi ya waganga wa tiba hizo wanajihusisha na ushauri wa kishirikina ama matambiko kwa wagonjwa wanaowapa tiba.

“Hiyo haitakiwi kabisa, kwani wengine wanashiriki katika mauaji ya albino, vikongwe, uchunaji ngozi za binadamu ama mauaji ya watoto wachanga na kupoteza maana ya tiba asili,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa wizara hiyo, Dk. Paulo Mhame, alisema madaktari wengi hawaelewi maana ya tiba asili na wale wa tiba za asili hawaelewi tiba za kisasa, hivyo ushirikiano kwao umekuwa mgumu,” alisema Dk. Mhame.

Alisema serikali imekuwa ikirekodi tiba za asili pamoja na za kisasa kwa ajili ya matumizi ya kimataifa, hivyo kuwepo kwa taasisi za utafiti kutasaidia kuboresha tiba hizo.

0 comments:

Post a Comment