Powered by Blogger.

Sikiliza Live

Tuesday, 14 May 2013

Wakenya wapinga mishahara mikubwa ya Wabunge

                         


 

Polisi nchini Kenya wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokusanyika nje ya Majengo ya Bunge mjini Nairobi kupinga matakwa ya wabunge ya kutaka waongezewe mishahara yao.
Makundi ya kijamii yamesema kuwa, maandamano hayo yanaakisi hasira za Wakenya kuhusu wanasiasa ambao wanataka mishahara mikubwa baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Machi 4. Waandamanaji waliwapa nguruwe hai damu kama nembo ya wabunge walafi, wanaojitakia makuu na wasiojali wananchi na ambao wanafyonza damu ya walipa kodi Kenya. Hivi karibuni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alitoa wito kwa wabunge kutafakari kuhusu kuwahudumia wananchi badala ya kufikiria kujishughulisha na mkakati wa kujiongezea mishahara. Rais Kenyatta amesema Kenya haiwezi kumudu gharama kubwa za mishahara.  Amesema huenda Kenya ikapoteza nafasi yake ya kiuchumi barani Afrika kutokana na bajeti kubwa ya mishahara. Tume ya Mishahara Kenya SRC ilipunguza mishahara ya wabunge kutoka Shilingi 851,000 hadi 532,400 jambo ambalo limewakasirisha wabunge wapya. Tume hiyo imeshikilia msimamo wake na kusema wabunge kamwe hawatapata nyongeza ya mishahara kwenye kipindi hiki kigumu katika uchumi wa Kenya. Wabunge wa Kenya ni kati ya wabunge wanaopata mshahara mkubwa zaidi duniani.

0 comments:

Post a Comment